3054; Uhakika wa ushindi.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye safari ya maisha ya mafanikio, ushindi ndiyo kitu ambacho kila mtu anakitaka.
Lakini pia kimekuwa ndiyo kitu adimu sana. Ni watu wachache mno ndiyo wamekuwa wanapata mafanikio wanayoyataka.

Kwa jinsi ambavyo mafanikio yamekuwa adimu, yanaonekana kama ni kitu cha kubahatisha, ambacho mtu hawezi kuwa na uhakika nacho kwenye maisha yake.
Ni kweli kwamba hatuwezi kuwa na uhakika kwenye mambo mengi.
Lakini inapokuja kwenye safari ya mafanikio, tunaweza kujitengenezea uhakika wa ushindi.

Njia pekee ya kujihakikishia ushindi kwenye safari yako ya mafanikio ni kuwa tayari kukamua mpaka tone la mwisho la uwezo uliopo ndani yako na kuuleta kwenye uhalisia.
Hapo ni kujitoa kwa kila namna kwenye safari yako ya mafanikio na kutokujihurumia kwa namna yoyote ile.

Kwa kujua mafanikio unayoyataka na kuwa tayari kuyapambania kwa kila namna bila ya kuchoka wala kukata tamaa ndiyo ushindi wa uhakika.
Hiyo ni kwa sababu kama utaendelea na mapambano bila kuchoka, ni uhakika kwamba utayapata mafanikio au utakufa ukiwa unayapambania.

Hicho ni kitu ambacho hakipo kwa walio wengi.
Wengi huanza safari ya mafanikio, lakini wanapokutana na magumu na vikwazo, wanakata tamaa haraka.
Hilo ndiyo limekuwa likisababisha wengi kushindwa kwenye maisha.

Kama utaendelea na safari ya mafanikio bila kukata tamaa licha ya magumu unayokuwa unayapitia, kama utaendelea kukamua kila tone la uwezo uliopo ndani yako, ushindi ni swala la muda tu.
Ni lazima utafanikiwa na hata kama hutafanikiwa, utakufa ukiwa unapambania ushindi wako, ambayo pia ni mafanikio, ukilinganisha na wengi wanaokata tamaa na kuacha haraka.

Kama bado upo hai, hupaswi kukata tamaa na kuiacha safari ya mafanikio.
Hupaswi kukubali magumu na changamoto unazokutana nazo kuwa kikwazo kwako kuendelea na safari.
Umeshaianza safari, hakuna kusimama, ni ushindi mbele kwa mbele.

Kumbuka ulipokuwa shuleni, ulipokuwa na mitihani lakini humafanya maandalizi mazuri. Ulipofeli mitihani hiyo ulikuwa na majuto kwako mwenyewe. Ukijiambia kama ungeweka jitijada zaidi, huenda ungefaulu.
Na kama uliweka kila jitihada ulizoweza kuweka na ukafeli, unajua kwamba ulifanya kila ulichoweza, hivyo hukuumia sana.

Kadhalika ndivyo ilivyo kwenye safari ya mafanikio kwenye maisha. Kama utaikatia tamaa safari, utajilaumu pale utakaposhindwa kufanikiwa.
Lakini kama utaendelea na mapambano bila kuchoka wala kukata tamaa, hata kama utashindwa hutajilaumu. Na huo ndiyo uhakika wa ushindi wenyewe.

Mafanikio yako yanapimwa na jinsi ulivyojitoa kuyapambania bila ya kukubali kukwamishwa na kitu chochote.
Swali muhimu sana unalopaswa kujiuliza ni kama umefanya kila kinachopaswa kufanyika.
Watu wamekuwa wanajiuliza swali lisilo sahihi, ambalo ni kama wamefanya kila kilicho ndani ya uwezo wao.
Uwezo wa kila mtu ni mkubwa kuliko anavyoweza kupima.
Kuwa na uhakika wa ushindi ni kuwa tayari kufanya kila kinachohitajika kufanya, kujitoa kwa hali ya juu sana bila ya kukata tamaa.

Kipimo pekee cha mafanikio ni kama mtu umekamua mpaka tone la mwisho la uwezo wako.
Ambalo pia huwezi kujua kama ni tone la mwisho, hivyo ni kukamua bila ya ukomo.

Ukiangalia wale wanaokamua miwa kupata juisi, kuna funzo kubwa sana utakalopata.
Pale unapodhani kwamba maji kwenye miwa yameisha, ndivyo ikikamuliwa kwa nguvu zaidi kuna matone ya maji yanatoka kwenye miwa hiyo.
Wakati miwa imejaa maji, nguvu kidogo tu zinakamua maji hayo.
Lakini kadiri maji yanavyozidi kuisha ndivyo nguvu kubwa zaidi zinavyohitajika ili kukamua maji.
Kupata tone la mwisho kabisa kwenye miwa, nguvu kubwa sana inahitajika.

Hivyo ndivyo safari ya mafanikio ilivyo. Kupata mafanikio madogo madogo, nguvu kidogo tu inahitajika.
Lakini kupata mafanikio makubwa, hasa unapokuwa unakabiliana na magumu na changamoto, nguvu kubwa zaidi inahitajika.
Kama upo tayari kuendelea kuweka nguvu kubwa kwenye safari yako ya mafanikio, ushindi ni wa uhakika kwako.

Wengi hukata tamaa kwenye safari yao ya mafanikio na kuona haina uhakika.
Lakini kama utakuwa tayari kukamua mpaka tone la mwisho, huo pekee ni ushindi mkubwa sana kwako.

Kamwe usikate tamaa na kuona mafanikio hayawezekani kwa sababu tu umechelewa kuyapata au umekutana na magumu na changamoto.
Kama upo tayari kuendelea kupambana, bado ipo fursa kubwa ya wewe kufanikiwa.
Kushindwa ni pale unapokuwa umekata tamaa na kuacha kuendelea na mapambano.

Kama utakuwa tayari kuendelea na mapambano kwa nguvu kubwa bila ya kukata tamaa, huo pekee ni ushindi mkubwa sana kwako.

Uhakika wa ushindi upo kwenye juhudi unazoweka bila ya kukatishwa tamaa na chochote.
Kama utakuwa tayari kukamua mpaka tone la mwisho, kama utaacha kujihurumia na kuweka juhudi kwa namna inavyopaswa tayari unakuwa umejihakikishia ushindi.

Hebu fikiria umechagua kufanya biashara ya aina fulani na kuamua kuweka umakini wako wote kwenye biashara hiyo kwa miaka 10 bila kuacha wala kuyumba.
Kwa hakika utapata mafanikio makubwa sana kwenye biashara hiyo.
Na hata kama hutayapata mafanikio unayotaka kwenye miaka hiyo 10, ukiongeza mingine 10 huku ukikamua zaidi, ushindi unakuwa mkubwa na wa uhakika.
Na hata kama kwenye hiyo 10 mingine bado unakuwa hujapata unachotaka, ukiongeza miaka mingine 10, kuna makubwa zaidi utafanya.
Nadhani unapata picha hapo.

Kwenye safari ya mafanikio, kilicho muhimu siyo nini unachopata, bali nini unachofanya.
Unachopata ni matokeo tu, ambayo hayapo ndani ya udhibiti wako kamili na hivyo kutokuwa na uhakika nayo.
Unachofanya ndiyo kipo ndani ya udhibiti wako kamili na hivyo kuweza kuwa na uhakika nacho.

Jipe uhakika wa mafanikio kwa kuwa tayari kukamua mpaka tone la mwisho la uwezo mkubwa ulio ndani yako.
Hata pale unapoona umeshafanya kila kitu, jua unaweza kufanya zaidi.
Hilo ndiyo litakusukuma kuendelea kufanya na kukuhakikishia mafanikio makubwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe