Barua ya II; Usumbufu Kwenye Usomaji.

Rafiki yangu Mstoa,
Maisha ni darasa ambalo halina kuhitimu. Hiyo ina maana kwamba kila wakati mtu unapaswa kuwa unajifunza.

Zipo njia nyingi za kujifunza, na moja iliyo kuu na ambayo imedumu kwa miaka mingi zaidi ni kusoma vitabu.

Tangu enzi na enzi, maarifa yamekuwa yanashirikishwa kwa njia ya maandishi.
Kabla ya kuja kwa karatasi, maandishi yaliwekwa kwenye mawe, miamba, ngozi na hata magome ya miti.

Ugunduzi wa karatasi na mashine za kuchapa vitabu kumerahisisha sana kusambaa kwa maarifa kwa njia ya maandishi.
Katika uvumbuzi ulioleta mapinduzi makubwa duniani, uchapaji ni moja wapo.

Leo hii kuna maandiko mengi sana ambayo hata kama mtu atatumia kila dakika ya maisha yake kusoma, hawezi kumaliza hata asilimia 0.01 ya maandiko yote yaliyopo.
Na hapo bado maandiko zaidi yanaendelea kuzalishwa kwa kila namna.

Kwa kifupi ni kwamba tupo kwenye bahari kubwa sana ya maarifa, tukiwa tumezungukwa na maarifa mengi sana.

Lakini unajua nini cha kushangaza? Watu wengi wanakufa kwa kiu ya kukosa maarifa ili hali wakiwa wanazungukwa na maarifa mengi sana.

Yaani licha ya kuwepo kwa maarifa mengi sana, watu wengi wanakosa maarifa na hilo kupelekea maisha yao kuwa magumu.

Tunawezaje kuelezea mtego huu mkubwa uliopo, kwamba maarifa ni mengi na yanapatikana kwa urahisi, ila watu hawana maarifa?

Hicho ni kitu ambacho Mstoa Seneca alikiona zaidi ya miaka elfu 2 iliyopita, wakati bado hata hakujawa na maarifa mengi kama sasa.

Seneca aliita hali hiyo usumbufu kwenye usomaji. Na kwenye barua yake ya pili kati ya barua nyingi alizomwandikia rafiki yake Lucillius, alishirikisha mambo sita kuhusu hali hiyo ya usumbufu kwenye usomaji na hatua za kuchukua ili kuondokana na changamoto hiyo.

Karibu tujifunze mambo haya ili tuweze kuwa na utulivu wa kunufaika na maarifa mengi yanayopatikana kwenye zama hizi tunazoishi.

1. Kuwa na utulivu.

Watu wengi wamekosa utulivu na kuwa na mahangaiko mengi kwenye maisha yao.
Hilo limepelekea kujikuta wakihangaika na kila kitu na kushindwa kufurahia chochote.

Seneca anasema hali hiyo ya kukosa utulivu ni dalili za kuchafukwa kwa roho.
Anashauri tuwe na utulivu wa ndani yetu wenyewe, tuweze kukaa wenyewe na fikra zetu.

Hatua ya kuchukua;
Tenga muda ambao utakuwa unakaa peke yako kwa utulivu ili kuweza kuyatafakari maisha yako.

Nukuu;
‘The primary indication, to my thinking, of a well-ordered mind is a man’s ability to remain in one place and linger in his own company.’ – Seneca

‘Kwa fikra zangu, kiashiria cha msingi cha akili iliyotulia ni uwezo wa mtu kukaa peke yake na fikra zake.’ – Seneca

2. Usisome waandishi wengi.

Kutokana na wingi wa maarifa, watu wamekuwa wanajikuta wakiwasoma waandishi wengi na vitabu vingi, kitu ambacho kinawakosesha utulivu na kuwazuia kujifunza kitu chochote kwa kina.

Seneca anashauri mtu uchague waandishi wachache ambao utasoma kazi zao  kwa kina, kuzielewa na kuchukua mawazo ambayo utayafanyia kazi.

Seneca anaenda mbali zaidi na kutumia mfano wa mtu ambaye kila mara anasafiri. Mtu huyo atakutana na watu wengi, lakini hatakuwa na marafiki wa kina.

Hatua ya kuchukua;
Chagua waandishi wachache ambao unawakubali sana na usome kazi zao kwa kina kisha kutoka na mawazo unayokwenda kuyafanyia kazi kwenye maisha yako.

Nukuu;
‘You must linger among a limited number of master-thinkers, and digest their works, if you would derive ideas which shall win firm hold in your mind.’ – Senca

‘Kama unataka kupata mawazo ambayo yatadumu kwenye akili yako, chagua waandishi wachache ambao utasoma kazi zao kwa kina.’ – Seneca

3. Kipe kitu muda, usiwe na haraka.

Changamoto kubwa kwenye zama tunazoishi sasa ni wingi wa mambo na tamaa ya watu kutokutaka kupitwa.
Kutaka kupitia mambo yote bila kupitwa imefanya watu kuwa na haraka kwenye kila jambo.
Haraka hiyo inawakosesha subira na kushindwa kufurahia chochote wanachokuwa nacho.

Seneca anaeleza hilo kwa kutumia mfano wa chakula. Anasema chakula hakiwezi kufyonzwa mwilini kama kitapita tumboni kwa haraka. Na hilo liko wazi, mtu akiwa anaharisha mwili haupati virutubisho vilivyo kwenye chakula anachokula.

Mfano mwingine ambao Seneca anatumia ni mti ambao unapandwa na kuhamishwa kila mara. Mti wa aina hiyo hauwezi kushika mizizi na kuota. Ili mti uweze kuota, unatakiwa kuachwa pale ulipopandwa kwa muda mrefu.

Hatua ya kuchukua;
Kila kitu unachofanya kipe muda, usiwe na haraka wala papara ya kutaka mambo hapo kwa hapo.
Mambo yote mazuri yanahitaji muda, kuwa na subira.

Nukuu;
‘Nothing hinders a cure so much as frequent change of medicine; no wound will heal when one salve is tried after another; a plant which is often moved can never grow strong.’ – Seneca

‘Hakuna kitu kinachozuia uponyaji kama kubadili matibabu mara kwa mara.; mti unaohamishwa kila mara hauwezi kuota na kuwa imara.’ – Seneca

4. Rudia kusoma vitabu bora.

Kutokana na wingi wa vitabu vipya vinavyotoka kila siku, mtu unaweza kushawishika kutaka kusoma vitabu hivyo, kwa kuona kuna kitu kipya cha kujifunza.

Seneca hashauri hivyo, anasema hata kwa kurudia kusoma vitabu bora, bado kuna mengi mapya utakayoweza kujifunza.
Ukweli ni kwamba, huwezi kujifunza kila kitu kwa kusoma kitabu mara moja.
Kila mara unaporudia kusoma kitabu, kuna vitu vipya unavyojifunza.

Hatua ya kuchukua;
Badala ya kukimbilia kusoka vitabu vingi na vipya, rudia kusoma vitabu bora ulivyochagua. Kuna mengi mapya utakayojifunza kwa kurudia kusoma vitabu bora.

Nukuu;
‘So you should always read standard authors; and when you crave a change, fall back upon those whom you read before.’ – Seneca

‘Mara zote soma waandishi uliowachagua na pale unapotaka mabadiliko, rudia wale ambao umeshawasoma.’ – Seneca

5. Tamaa ndiyo umasikini.

Kuna kitu kingine ambacho Seneca anakigusia kwenye mada hii, ambacho pia kinagusa maeneo mengine ya maisha.
Anasema umasikini siyo kutokuwa na fedha au mali, bali ni kuwa na tamaa ya kupata zaidi hata unapokuwa umeshapata fedha na mali.

Ni muhimu sana mtu ukaridhika na vitu ulivyonavyo, kwani hilo linakupa utulivu mkubwa.
Dhibiti tamaa zako ili ufurahie yale ambayo tayari unayo.

Hatua ya kuchukua;
Usiangalie nini umekosa na kuumizwa nacho, badala yake angalia nini unacho na ukitumie vizuri.
Utajiri ni kuweza kutumia vizuri vile ulivyonavyo.

Nukuu;
‘It is not the man who has too little, but the man who craves more, that is poor.’ – Seneca

‘Aliye masikini siyo yule mwenye vichache, bali yule aliye na tamaa ya vingi zaidi.’ – Seneca

6. Anza na yaliyo muhimu, kisha yanayokutosha.

Seneca anamalizia na swali la msingi sana ambalo tunakwenda kulipata moja kwa moja. Anauliza; ‘Do you ask what is the proper limit to wealth? It is, first, to have what is necessary, and, second, to have what is enough.’
Akiwa anamaanisha; ‘Unauliza nini kikomo sahihi cha utajiri? Ni, kwanza, kuwa na kile kinachohitajika, na pili, kuwa na kile kinachotosha.’

Hatua ya kuchukua;
Jua mahitaji yako ya msingi na uyakamilishe, kisha nenda kwa yale yanayokutosha. Usikubali kuwa mtumwa wa kitu chochote kile.

Rafiki yangu Mstoa, tumejifunza jinsi ya kuepuka usumbufu kwenye usomaji na hata maisha kwa ujumla.
Tuyazingatie haya ili tuweze kuwa na maisha bora na tulivu.

Kocha Dr. Makirita Amani.