3059; Ahadi yangu kwako.

Rafiki yangu mpendwa,
Tangu nilipoanzisha huduma ya ukocha ya KISIMA CHA MAARIFA mwaka 2014, sikuwa naichukulia huduma hii kama biashara, kwa maana ya kuwaangalia washiriki kama wateja.

Badala yake nimekuwa naichukulia kama huduma ninayoijenga na washiriki nimekuwa nawachukulia kama bidhaa ambayo ipo ndani ya huduma.
Ndiyo maana gharama za huduma hii zimekuwa chini mara zote, ili zisiwe kikwazo kwa wale wanaoihitaji kweli.

Mpango ukiwa ni kupitia washiriki waliopo sasa, tujenge sifa bora kabisa ya huduma hii na sifa hiyo bora iweze kuiuza huduma kwa wengi na kwa gharama kubwa zaidi.

Sasa nakwenda kubadili hilo, kwa kuifanya huduma kuwa biashara kamili na washiriki siyo tena bidhaa, bali ni wabia wa kibiashara.

Nimeacha mambo mengi sana kwenye maisha yangu kwa ajili ya kuijenga hii huduma.
Hivyo basi, kila anayeshiriki kwenye huduma hii, ninakuwa mbia wake kwenye biashara anayoijenga.

Hiyo ni kuhakikisha kwamba kila anayeshiriki huduma hii anapata manufaa makubwa na kufikia malengo makubwa aliyonayo.
Na kwa sasa lengo letu kuu ni kufikia ubilionea mwaka 2030, nitahakikisha kila mtu anajisukuma kweli kufikia lengo hilo.

Ahadi yangu kwako wewe kama mshiriki wa huduma hii ni kama ifuatavyo; KAA KWENYE MCHAKATO KAMILI WA HII HUDUMA KWA KIPINDI CHOTE TUNACHOFANYIA KAZI LENGO KUU.
NA KAMA UTASHINDWA KULIFIKIA LENGO PEKE YAKO, BASI NITAKUPA FURSA BORA ZAIDI YA KULIFIKIA LENGO KWA UHAKIKA.

Ninachosema ni kwamba, wajibu wako wewe ni kukaa kwenye huu mchakato wetu kwa msimamo na uhakika.
Na kama kwa sababu zozote zile umeshindwa kulifikia lengo la ubilionea, utapata fursa ya kuingia kwenye biashara za wengine ambazo zimeweza kufanya vizuri na kukuwezesha kulifikia lengo.

Iko hivi rafiki, tuna biashara nyingi sana na za tofauti zinazofanyika na washiriki wa huduma hii.
Kwa kanuni tu ya wastani, kuna biashara ambazo zitafanya vizuri sana na baadhi hazitafanya vizuri.

Zile ambazo zitafanya vizuri zitahitaji zaidi watu ili kuendelea kukua na kuleta manufaa makubwa.
Na hapo ndipo patakapokuwa na fursa nzuri kwa wale ambao tayari wapo kwenye huduma hii na wanauelewa vizuri mchakato kamili.

Hilo ndiyo ninalokuahidi kama mshirika na mbia wako wa kibiashara. Kaa kwenye mchakato kwa msimamo na uhakika kwa kipindi chote na kama biashara yako haitaweza kukufikisha kwenye lengo, utapata nafasi kwenye biashara nyingine zenye fursa ya kukufikisha kwenye lengo.

Rafiki, ili ushirika na ubia wowote uweze kufanya kazi, lazima ujengwe kwenye msingi mkuu wa uaminifu.
Ni lazima tuaminiane sana, kwa kusimamia misingi sahihi na kukaa kwenye mchakato muda wote.
Kwa kuwa safari ina vikwazo mbalimbali, lazima tuwe na imani kwamba vikwazo anavyopitia mtu ni vya kimazingira au kiuchumi na siyo vinasababishwa na uvivu na uzembe wa mtu mwenyewe.

Ahadi yangu itakuwa sahihi na ambayo lazima niitimize kama tu utakamilisha sehemu yako ya ahadi hii, ambayo ni kuwa mwaminifu na kukaa kwenye mchakato.
Kama utashindwa na wakati huo huo hukai kwenye mchakato na wala huna uaminifu, unakuwa umeivunja ahadi mwenyewe.

Kama umeshindwa kwa sababu ya uvivu na uzembe wako mwenyewe, sitaweza kukupeleka mahali pengine napo ukaue biashara ambayo mwenzako amepambana sana kuijenga.

Eneo hili la uaminifu na kukaa kwenye mchakato ni nyeti sana.
Kama kutakuwa na mazingira yoyote yanayotilia shaka juu ya uaminifu wako na ukaaji wako kwenye mchakato, unakuwa umeivunja ahadi yetu.
Kama utaonyesha viashiria vya kukosa uaminifu na kutokukaa kwenye mchakato mapema, hutapata nafasi ya kuendelea na huduma hii.

Hilo ni eneo ambalo nimekuwa nalisimamia kwa ukali na umakini mkubwa, kwa sababu bila ya hivyo hakuna kitu tutakachoweza kujenga.
Tutaishia kudanganyana kwa kupeana matumaini hewa.

Hii safari ya ubilionea ni ngumu kuliko kitu chochote kile kwenye maisha yako.
Inakutaka ujitoe sana, uwe tayari kuteseka na kutengwa na wengine.
Huku pia ukiwa huna uhakika sana wa kulifikia lengo.
Lakini kupitia huduma hii, nakwenda kukupa uhakika wa kulifikia lengo.
Kwani kama utalishindwa peke yako, kama utakuwa mwaminifu na mkaaji kwenye mchakato bila shaka yoyote, utapata fursa nzuri kwenye biashara zitakazofanikiwa.

Watu wengi hudhani ubilionea ni mpaka ujenge biashara yako mwenyewe.
Ni kweli kujenga biashara ni hitaji muhimu, lakini siyo lazima iwe yako mwenyewe.
Mabilionea wengi duniani ni zao la ubia wa kibiashara au kupata nafasi za juu kwenye biashara kama kuwa mkurugenzi mkuu.

Hicho ndicho ninachokuahidi hapa.
Kama utakaa kwenye huu mchakato kwa uaminifu mkubwa, kama biashara yako itashindwa, ufapata nafasi ya kuwa mbia au kufanya kazi kwenye nafasi za juu kwenye biashara ambazo zitafanya vizuri ndani ya hii huduma.

Kwa sababu kama ambavyo tunaendelea kuona, kupata watu sahihi ni changamoto kubwa sana kwenye kujenga timu ya kibiashara.
Kwa wewe kuwa mtu sahihi, utaweza kufanyia kazi kwa ubora fursa ya kuwa nafasi za juu kwenye biashara za watu wengine.

Wajibu wako mkubwa kwenye haya makubaliano yetu ni kukaa kwenye mchakato kwa ukamilifu na msimamo bila kuyumba.
Iishi misingi yetu yote kwa uaminifu mkubwa.
Jifunze kila wakati.
Jenga biashara.
Fanya uwekezaji.
Weka fokasi kwenye haya mambo muhimu.

Kama utatimiza hayo, kwa matendo yanayojionyesha na siyo tu maneno, nakuhakikishia utalifikia lengo lako kuu la ubilionea.
Kama utashindwa kulifikia peke yako, utapata fursa ya kulifikia kwa kushirikiana na wengine.

Kama utashindwa kukaa kwenye mchakato au utakosa uaminifu, huo ndiyo unakuwa mwisho wa ubia na ushirika wetu.
Hatutahitaji kuwa na mazungumzo yoyote ya mapatano, ushahidi ulio wazi wa kukosa uaminifu au kutokukaa kwenye mchakato ndiyo yatakuwa maamuzi ya mwisho.

Naamini sana kwenye huu mchakato kiasi kwamba naweza kuwa tayari kumlipa mtu aliyekaa kwenye mchakato huu kwa uhakika na asipate matokeo.
Ninajipa uhakika kwenye hilo kwa sababu najua mchakato huu unafanya kazi, kama utafanyiwa kazi.
Ndiyo maana nipo tayari kukudhamini kwa namna yoyote ile kama kweli utastahili dhamana, kwa kuwa mwaminifu na kukaa kwenye mchakato kwa uhakika na msimamo.

Karibu twende pamoja kwenye hii safari rafiki yangu.
Nimejitoa hasa kuhakikisha unapata maarifa na miongozo yoyote unayohitaji.
Nimejitoa kukusukuma zaidi ya ulivyozoea.
Na nimejitoa kukuwajibisha hasa pale unapoyumba kwenye mchakato.
Wajibu wako ni kuwa mwaminifu na kukaa kwenye mchakato.
Mengine yote yatakwenda sawa.
Na ubilionea utaufikia kwa uhakika.

Haya siyo matumaini hewa ninakupa.
Hii ni fursa ya wewe kupambana mpaka tone la mwisho ili kulifikia lengo.
Na kama utapambana kweli, nakuhakikishia utalifikia lengo, kama siyo peke yako, basi kwa kushirikiana na wengine.

Pambana uwezavyo uendelee kubaki ndani ya huduma hii.
Kwani mazuri na makubwa sana yapo mbele yetu kwa uhakika.
Usijinyime hayo kwa kukosa uaminifu na kushindwa kukaa kwenye mchakato kwa uhakika na msimamo.

Nimalizie kwa kusema;
Wewe siyo mteja wangu,
Wewe siyo bidhaa yangu,
Wewe ni mshirika na mbia wangu kwenye hii safari ya kujenga ubilionea.
Kamilisha sehemu yako na mimi nikamilishe sehemu yangu na kwa uhakika tutalifikia lengo hili kubwa.
Karibu sana tuendelee kuwa pamoja.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe