3074; Utekelezaji ni muhimu zaidi.

Rafiki yangu mpendwa,
Kuna watu wanadhani kwamba kinachowazuia wasifanikiwe ni hawajawa na wazo bora kabisa linaloweza kuwapa mafanikio makubwa.

Wengine wengi wanadhani kinachowakwamisha ni hawajapata mtaji kwa ajili ya kuanzisha au kukuza biashara.
Wengine ni ujuzi, koneksheni au kukosa rasilimali muhimu ambazo wanahitaji.

Kuna mengi watu wanaweza kujiambia yanawakwamisha wasifanikiwe, lakini yote siyo sahihi.
Watu wanaofanikiwa huwa wanapata sababu ya kufanikiwa, licha ya mengi wanayokuwa wamekosa.
Na watu wanaoshindwa huwa wanapata sababu ya kushindwa, licha ya mengi wanayokuwa nayo.

Kitu kikubwa sana kinachowakwamisha watu wengi kufanikiwa ni kwenye utekelezaji.
Mawazo ni rahisi sana, kila mtu anayo mazuri.
Ni kutekeleza mawazo hayo ndiyo shida inapoanzia.

Kwenye utekelezaji wa mawazo kuna vikwazo vikuu viwili;
Cha kwanza ni ugumu ambao upo kwenye safari yoyote ya mafanikio.
Wengi huanza vizuri na mawazo wanayokuwa nayo, lakini wanapokutana na ugumu, wanaacha kufanya kwa kuona hayawezekani kabisa.
Cha pili ni usumbufu ambao unatokana na mawazo mengine yanayoweza kuonekana ni mazuri zaidi. Kila wakati kuna mawazo huwa yanakuja ambayo yanaonekana ni mazuri na rahisi kupata mafanikio. Watu wanashawishika kuachana na mawazo waliyokuwa nayo na kwenda kwenye mawazo hayo mapya. Kwa kwenda hivyo wanaishia kuwa wamejaribu mawazo mengi ila hakuna chochote wanachokuwa wamekamilisha.

Mafanikio yanatokana na utekelezaji wa yale ambayo watu wanawaza na kupanga.
Ingekuwa kuwaza peke yake ndiyo kunaleta mafanikio, wengi wangekuwa nayo.
Ingekuwa kupanga ndiyo kunaleta mafanikio, wengi sana wangekuwa nayo.
Lakini vyote hivyo havina mchango mkubwa kwenye mafanikio. Ndiyo maana wengi wanavyo na hawafanikiwi.

Mafanikio makubwa yapo kwenye utekelezaji.
Ni utekelezaji wa tofauti na wa kimsimamo ndiyo unapfanya watu kuweza kuzalisha matokeo tofauti na makubwa, ambayo ndiyo yanaleta mafanikio.

Kinachowapa watu mafanikio siyo kile walichonacho, bali jinsi wanavyotumia hicho walichonacho.
Ndiyo maana watu wawili wanaweza kufanya kazi ya aina moja na wanalipa mshahara unaolingana, lakini mmoja akafanikiwa wakati mwingine akashindwa.
Siyo walichonacho, bali jinsi wanavyokitumia.

Mafanikio ni kutumia vizuri kile ulichonacho ili kuweza kupata kile unachotaka.
Kushindwa ni kusubiri mpaka upate unachotaka.
Uzuri ni kwamba, kila binadamu aliye hai, kuna vitu vingi sana ambavyo anavyo ndani yake.
Mtu akiweza tu kuvitumia vile ambavyo tayari vipo ndani yake, hakuna namna atashindwa kufanikiwa.

Hii safari ya mafanikio hakuna mtu anayeweza kukukwamisha isipokuwa wewe mwenyewe.
Kataa kuwa kikwazo kwako kwa kuwa mtekelezaji mzuri wa yale unayofikiria na kupanga.
Ungepunguza muda unaofikiria kuja na mawazo mapya na kuyapangilia na ukapeleka muda huo kwenye utekelezaji wa wazo lolote ulilonalo, utavuna manufaa makubwa zaidi.

Acha kuhangaika na mawazo,
Acha kuhangaika na mipango,
Acha kuhangaika na uliyokosa,
Anza kuhangaika na utakelezaji.
Tumia vizuri kila ulichonacho sasa ili kuweza kupata yale yote unayoyataka.
Hakuna anayeweza kukuzuia isipokuwa wewe mwenyewe.

Na ufanyaji wenye matokeo siyo ule tu wa kufanya mara moja na kuacha pale matokeo yanapochelewa, bali ni ufanyaji wa msimamo bila kuacha hata kama matokeo ni ya aina gani.
Ukiamua kufanya na ukasema unafanya kweli bila kukwamishwa na chochote, utaweza kufanya makubwa sana.
Usiendelee tena kujizuia kupata matokeo makubwa zaidi ya ambayo unayo sasa.
Nenda hatua ya ziada kwenye utekelezaji na utaweza kufanya makubwa sana.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe