3076; Kubadilika na kutokubadilika.

Rafiki yangu mpendwa,
Hendry Ford, aliyekuwa mwanzilishi wa magari, alikuwa mtu mbishi sana kubadilika.
Baada ya kuja na gari ambalo lilipendwa sana na watu, hakutaka kubadili chochote, badala yake aliendelea kuzalisha gari hilo hilo kwa muundo ule ule.
Licha ya kushauriwa sana kubadilika, aliendelea kubaki kwenye kile alichoamini ndiyo sahihi.
Moja ya majibu ya kibabe sana ambayo aliwahi kuyatoa pale alipoambiwa wateja wanataka kuchagua rangi ya gari wanayotaka, alijibu; ‘mteja anaweza kupata rangi yoyote anayotaka, kama tu ni rangi nyeusi.’

Tunaweza kumcheka Ford kwa ubishi wake wa kijinga, ambao kweli ulimgharimu, maana aliacha upenyo kwa washindani kuja na magari bora zaidi.
Lakini pia ni msimamo ambao ulimsaidia kunufaika na kitu kwa muda mrefu.

Kuna changamoto kubwa sana kibiashara inapokuja kwenye mabadiliko.
Kutokana na maendeleo makubwa yanayotokea kwenye sayansi na teknolojia, biashara zimeathirika kwenye pande mbili.
Upande wa kwanza ni biashara ambazo zimekuwa zinabadilika kila wakati na kushindwa kujenga kitu chochote cha msingi.
Upande wa pili ni biashara ambazo zimekuwa zinagoma kabisa kubadilika na kuishia kuachwa nyuma na mabadiliko yanayoendelea.

Ili biashara ifanikiwe kwenye zama hizi za mabadiliko, inapaswa kuwa maono na misingi ambayo haibadiliki huku pia ikiwa na mchakato unaoendelea kuboreshwa kadiri inavyokwenda.

Biashara inatakiwa kusimamia maono na misingi yake kwa uhakika na bila kuyumbishwa na chochote kile.
Hizo ndiyo nguzo zinazoitofautisha biashara yoyote ile na nyingine.
Nguzo hizo zikiwa zinabadilishwa kila mara, biashara inakuwa dhaifu na kuanguka vibaya.

Mchakato wa utekelezaji wa mambo mbalimbali kwenye biashara unapaswa kuwa unaboreshwa kadiri muda unavyokwenda.
Hiyo ni kutokana na mabadiliko yanayoathiri ufanyaji wa baadhi ya mambo.
Teknolojia inapoleta njia rahisi za kufanya mambo, inatakiwa kutumiwa ili kurahisisha ufanyaji.

Kwa kusimamia maono na misingi bila kuyumba kuna wakati kunaweza kuonekana kama unakosea.
Ni kweli kuna fursa ambazo mtu unaweza kuzikosa kwa kusimamia maono na misingi ya biashara.
Lakini manufaa yanayopatikana kwa kusimamia hayo ni makubwa kuliko fursa zinazopotea.
Kila wakati unapaswa kujiuliza ni mambo gani ambayo biashara yako inasimamia na ambayo yanaitofautisha na biashara nyingine.
Kama kila wakati biashara yako inabadilika kwenye mambo hayo, siyo dalili nzuri.

Kwenye mchakato wa utekelezaji, kutokubadilika ni kujichelewesha kupiga hatua kubwa kwa urahisi unaokuwepo.
Kila jambo linalofanyika kwenye biashara yako, kadiri muda unavyokwenda linaweza kufanyika kwa gharama ndogo zaidi na muda mfupi zaidi.
Maendeleo ya teknolojia mara zote huwa yanaokoa gharama, muda na hata kurahisisha ufanyaji wa vitu, ambapo vitu vilivyokuwa vinahitaji mtu mwenye ujuzi mkubwa kufanya, vinaweza kufanyika na hata asiye na ujuzi kabisa.
Kila wakati unapaswa kujiuliza kama ufanyaji wa mambo kwenye biashara unarahisishwa na maendeleo ya teknolojia. Kama jibu ni hapana, biashara inaachwa nyuma kiushindani.

Simamia yasiyobadilika na badili yanayobadilika ili kuweza kujenga biashara imara na inayofanikiwa sana.
Hayo yote yanawezekana kwa kuelewa na kusimamia maono na misingi ya biashara huku mchakato wa utekelezaji wa mambo ukiboreshwa kulingana na mabadiliko ya kiteknolojia yanayoendelea.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe