3083; Piga kelele.
Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye kitabu cha CHUO CHA MAUZO nimeandika; ustaarabu pekee kwenye biashara ni kuuza.
Nimeandika hivyo kwa sababu kuna baadhi ya watu wanajiona ni wastaarabu sana hivyo kuna baadhi ya mambo hawawezi kufanya kwenye biashara.
Halafu kwa bahati mbaya sana, wanakuwa hawauzi.
Yaani mtu anajifanya mstaarabu, wakati hafanyi mauzo anayopaswa kuwa anafanya.
Hivyo basi, hakuna ustaarabu kwenye biashara kama huuzi.
Moja ya vikwazo vikubwa kwenye mauzo ni kutokujulikana.
Yaani unakuwa na bidhaa au huduma ambayo watu wanaihitaji sana, lakini hawajui kama unayo.
Hivyo wewe unakwama huna mauzo, huku wateja unaowalenga nao wanakwama hawana suluhisho wanalotaka.
Ili kuvunja kikwazo hicho cha kutokujulikana, unapaswa KUPIGA SANA KELELE.
Kupiga kelele ni kufanya mambo ambayo wale unaowalenga wanajua kwamba upo.
Na hapo ndipo wengi hukwama, kwa kuona hawawezi kufanya mambo hayo, kwa sababu itakuwa ni kukosa ustaarabu.
Unaweza kupiga kelele kupitia maneno au vitendo.
Kwenye maneno unaweza kufanya matangazo, kutoa elimu na hata kuwa na mazungumzo yatakayowafanya watu wajue kile unachouza.
Kwenye vitendo unaweza kutoa mfano au kufanya maonyesho ya kile unachouza na pia unaweza kuwa mtumiaji ili watu wakuone na wao kutaka kuwa nacho.
Kupiga kelele ni kuhakikisha kila mtu anayekujua anajua kile unachouza.
Ni kuhakikisha kila anayejua unachouza anawafanya wale wanaomzunguka nao kujua unachouza, hata kama hujawafikia moja kwa moja.
Ni kuhakikisha kila anayepita ilipo biashara, anajua kuhusu uwepo wa biashara. Maana unaweza kushangaa ni watu kiasi gani wanapita pale ilipo biashara lakini hawajui kama biashara hiyo ipo.
Kuna njia nyingi za kupiga kelele kwenye biashara, hapa ni chache muhimu unazopaswa kutumia mara zote.
1. Weka spika eneo la biashara ambayo inatangaza biashara hiyo. Maelezo yanapaswa kuwa ya kumnasa mtu anayepita hata kwa mbali.
2. Panga bidhaa kwa nje ili watu wanaopita waone na kuvutiwa kutaka kuzipata.
3. Weka TV eneo la biashara na onyesha video za vitu unavyouza ili watu wavutiwe kuwa navyo.
4. Pita na gari la matangazo kwenye maeneo yote yanayoizunguka biashara ili kuhakikisha wanajua.
5. Mara zote vaa mavazi yenye nembo ya biashara yako ili watu waone tofauti na kuuliza au kujua moja kwa moja.
6. Lipia matangazo ya vyombo vya habari ili yawafikie wengi zaidi. Haya lazima yawe kwa mwendelezo ili yawe na matokeo mazuri.
7. Lipia matangazo kwenye mitandao ya kijamii na kuwafikia wengi unaowalenga. Matangazo hayo pia yanapaswa kuwa ya mwendelezo ili yawe na tija.
8. Toa masoko elimishi, kwa kuwaelimisha watu kwenye mambo mbalimbali yanayoendana na kile unachouza. Hili kinapaswa kuwa zoezi endelevu na kuwafikia wengi zaidi na zaidi.
9. Kuwatembelea watu na kukutana nao ana kwa ana na kuwaeleza kile unachouza na jinsi kina manufaa kwao.
10. Kuwapigia simu wateja, wale wanaokujua na hata wasiokujua, kuhakikisha wanajua kuhusu uwepo wa biashara yako na jinsi inavyoweza kukusaidia.
11. Kuweka matangazo na kusambaza vipeperushi kwa wingi kwenye maeneo yote yenye watu unaowalenga.
12. Kuwa na wapambe na wapiga debe wengi ambao wanaiongelea biashara yako kwa watu wengi zaidi.
13. Kuiongelea biashara yako kila unapokuwepo. Kuwakumbusha watu wote unaojuana nao kuhusu biashara yako mara kwa mara.
Kwa njia za masoko elimishi na matangazo, watu wote unaowalenga wanapaswa kusikia au kuona kuhusu biashara yako kila siku. Ndiyo, KILA SIKU WAKUSIKIE AU KUKUONA, tofauti na hapo huna ustaarabu.
Kwa njia ya kuwapigia simu na kukutana nao, unapaswa kuwafikia watu wote unaowalenga (ambao wameshanunua na ambao bado) kila wiki. Ndiyo, KILA WIKI UWAGUSE MOJA KWA MOJA, tofauti na hapo huna ustaarabu.
Kwa bahati mbaya sana tunaishi kwenye zama ambazo watu wamevurugwa na kelele nyingi zinazoendelea kwenye maisha yao.
Hivyo kama wewe hutaweza kupiga kelele za kibunifu na za mara kwa mara, hutaweza kuwafikia watu hao.
Wafanyabiashara wote ambao hawafanyi mauzo makubwa, huwa wanaona hawataki kuwasumbua watu kwa kupiga kelele ambazo zitawafikia.
Mwishowe wanapuuzwa kwa kutokujulikana.
Kwenye biashara na hata maisha kwa ujumla, hakuna kitu kibaya kama kupuuzwa. Unapopuuzwa hakuna hata anayekuongelea na hivyo unapotea kabisa.
Ni bora kuwasumbua watu, uwakere na hata kuwafanya wakuchukie. Watu wanapokuchukia wewe au biashara yako, wataiongelea kwa wengine wengi na hiyo inakuwa njia ya kujulikana na wengi zaidi.
Hivyo basi, usiache kupiga kelele kwa wingi na ukubwa kila wakati kwa kuona unawakera watu.
Ni bora kuwakera watu kuliko kutokujulikana kabisa.
Weka ustaarabu pembeni na piga sana kelele kuhusu biashara yako.
Kama yupo mtu yeyote unayemlenga kwenye biashara yako na hajasikia au kujua kuhusu uwepo wako na biashara yako basi jua umeshindwa, hujapiga kelele za kutosha.
Ustaarabu pekee kwenye biashara ni kuuza.
Piga sana kelele ili uweze kujulikana na kuwashawishi watu wanunue kile unachouza.
Uzuri ni kwamba hilo ni rahisi sana kwa zama tunazoishi sasa.
Kama hufanyi ni kwa sababu tu una uvivu mkubwa na siyo kwa sababu haiwezekani.
ACHA UVIVU, PIGA KELELE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe
Ustaarabu pekee ni kuuza, piga kelele.
LikeLike
Kelele hasa.
LikeLike
Asante Sana kocha. Nitaendelea kupiga kelele Kila SIKU bila kuacha.
LikeLike
Kila la kheri.
LikeLike
Ustaarbu pekee kwenye biashara yangu ni kuuza,nitauza kwa kujulikana na wale wenye uhitaji wa ninachouza kwa kuwapigia simu,kukutana nao ana kwa ana na kutangaza biashara kwa njia ya mtandao ,vyombo vya habari ,marafiki na masoko elimishi.
LikeLike
Kila la kheri.
LikeLike
Ahsante sana kocha, nitaendelea kupiga kelele hadi wale ambao hawaijyi biashara yangu waweze kuijua
LikeLike
Safi sana.
LikeLike
Kazi ni moja tu, kupiga kelele ili biashara yangu ijulikane na watu. Asante sana kocha.
LikeLike
Kila la kheri.
LikeLike
Kupiga kelele ni kuhakikisha kila mtu anayekujua anajua kile unachouza.
Asante sana
LikeLike
Hakika
LikeLike
Asante sana Kocha,
Nitapiga kelele za kibunifu na mara kwa mara ili biashara na shughuli zangu ziwafikie walengwa.
LikeLike
Vizuri sana.
LikeLike
Kup[ga kelele ni kuhakikisha kila mtu anayekujua anajua kile unachouza
Kutokupiga kelele ni uzembe na uvivu
LikeLike
Kabisa.
LikeLike
Ni bora kuwa msumbufu kuliko kuwa kimya na kutokujulikana na wale wasiokujua ustaarabu pekee ni kujulikana
LikeLike
Kabisa, kupuuzwa ni kaburi.
LikeLike
Ni bora kuwakera watu kuliko kutojulika kabisa.
LikeLike
Kabisa.
LikeLike
Kweli ustaarabu pekee kwenye biashara ni kuuza,kupiga kelele kila mtu akusikie,kama leo nilikuwa hospital bado nikampata mteja na akaweza kuja kununua
LikeLike
Hongera sana.
Tusiache kuongea na watu, bila kujali tuko wapi.
LikeLike