3090; Nipe namba, nikupe hadithi.

Rafiki yangu mpendwa,
Watu huwa wanapenda sana kuongea.
Hiyo ni kwa sababu kupitia maongezi ni rahisi kuficha mambo ambayo wameshindwa kuyakamilisha.
Ukiwa mtu wa kusikiliza kila sababu unazopewa na kuziamini, utapewa sababu nyingi sana ila kamwe hutapewa matokeo.
Kama unataka watu waache kukupa sababu na wakupe matokeo, anza kwa kukataa hadithi wanazokupa.

Kataa hadithi ambazo watu wanakupa na watake wakupe namba ambazo wamefanyia kazi.
Waambie wakupe namba kavu kama zilivyo, kisha baada ya kupata namba, ndiyo unaweza kuzitumia kupata hadithi yoyote ile.
Namba wanazokupa watu ziwe na ushahidi wa kuonyesha ni kweli kwamba zimefanyika.

Namba huwa hazidanganyi kama zimetunzwa na kuripotiwa kwa usahihi.
Jinsi namba zilivyo zinaweza kutengeneza hadithi nyingi kuhusu namba hizo.

Kwa mfano kama mtu ameshindwa kufanya mauzo ya kufikia lengo alilo nalo, anaweza kuja na hadithi nyingi kwa nini ameshindwa kufikia lengo.
Lakini unachohitaji kwa mtu wa aina hiyo siyo hadithi kwenye mauzo hayo ya chini, bali namba zake kwenye hayo mauzo.
Kama utamtaka mtu huyo aripoti namba zake kwa usahihi, kuanzia wateja ambao wamepigia simu, waliotembelea, waliofanyiwa uwasilishaji na ambao wamekamilisha mauzo.
Kwa kuziangalia namba hizo, utaona wazi kwa nini mauzo ni madogo kuliko lengo.
Kwa haraka sana, mauzo madogo yanakuwa yanaendana na udogo wa namba za michakato muhimu ya mauzo.

Hivyo ndivyo unavyopaswa kwenda na watu wote unaojihusisha nao.
Mazungumzo yenu yasimamie kwenye namba ambazo zimefanyika, kisha kupitia namba hizo ndiyo maelezo yaweze kueleweka.
Ukiruhusu watu wakupe sababu kwenye kila jambo, utapokea sababu nyingi sana.
Lakini ukitaka watu wakupe namba zao za ufanyaji, maelezo hayatakuwa mengi na hatua za kuchukua zinaonekana wazi.

Uzuri ni kwamba kila jukumu linalotekelezwa kwenye biashara yako linaweza kugeuzwa kuwa namba.
Hivyo yageuze majukumu yote ya biashara yako kuwa namba zinazoweza kufanyiwa kazi.
Kisha kila unayempa jukumu, mpe na namba za kupima ufanisi wake.
Kuanzia hapo, mazungumzo yenu yanapaswa kusimamia kwenye namba zaidi kuliko maelezo na sababu.

Watu hawakupi kile unachotaka, bali wanakupa kile unachopokea.
Kama unapokea sababu na visingizio, hivyo ndivyo utakavyopewa na kila unayejihusisha naye.
Lakini unapokataa sababu na visingizio na kutaka upewe namba, utapewa namba hizo.
Muhimu ni namba ziwe zimechukuliwa na kuripotiwa kwa usahihi na ushahidi wa ufanyaji wa namba hizo uwepo.

Haijalishi namba ni ndogo kiasi gani, kama mtu ataziona wazi, ataweza kuchukua hatua na kuboresha zaidi matokeo yake.
Lakini kama mtu atajipa sababu na visingizio, anaweza kujikuta hata yeye mwenyewe anadanganyika na maelezo yake mwenyewe na hivyo kutokujisukuma kuzalisha matokeo bora zaidi.

Kataa watu kukupa hadithi na watake wakupe namba ambazo wamefanyia kazi.
Kwa hakika utaona mambo mengi ya kuboresha zaidi.

Na hivyo ndivyo mimi na wewe tunaendelea kwenda.
Usinipe maelezo mengi kuhusu matokeo uliyoyapata.
Wewe nipe namba zako na kupitia hizo nitaweza kupata hadithi yoyote ninayotaka.
Namba zinakupa nafasi ya kuwa bora kuliko maelezo.
Zipende namba,
Mambo yako yote yafanye kwa kupima kwa namba.
Na mazungumzo yako yote yafanye kwa namba.
Namba zinakuonyesha ukweli na ukweli unakuweka huru.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe