Miongoni mwa changamoto kubwa kwenye maisha ni kuendeshwa na hisia badala ya watu kuendesha hisia zao.
Pale tunaporuhusu hisia zetu zitutawale, uwezo wetu wa kufanya maamuzi unaondoka yaani fikra inakuwa chini sana. Fikra zikiwa chini hisia zinakuwa juu na uwezo wa kufanya maamuzi unakuwa chini.
Hisia kali na fikra ni vitu ambavyo haviwezi kukaa pamoja hata siku moja.
Kwa msaada wa falsafa ya ustoa, hisia ni kitu ambacho tunakitengeneza sisi wenyewe na hakuna anayetupa.
Kumbe basi, tunaweza kuchagua kutoruhusu hisia zitawale maamuzi yetu.
Aliyekuwa Mwanafalsafa wa Ustoa, Mwanafalsafa Epictetus ana ushauri mzuri wa kutuambia kuhusu hisia.
It isn’t the things themselves that disturb people, but the judgments that they form about them.
Death, for instance, is nothing terrible, or else it would have seemed so to Socrates too; no, it is in the judgment that death is terrible that the error lies.
Accordingly, whenever we are impeded, disturbed or distressed, we should never blame anyone else but only ourselves, that is, our judgements. It is an act of a poorly educated person to blame others when things are going badly for him; one who has taken the first step towards being properly educated blames himself, while one who is fully educated blames neither anyone else nor himself. – Epictetus, handbook, 5
Kinachotusumbua siyo kile kinachotokea, bali ni ile tafsiri yetu kwa kile kinachotokea. Kwa mfano kifo, siyo kitu cha kutisha, kama ingekuwa hivyo wanafalsafa kama Socrates wangekiogopa. Ni tafsiri yetu kwamba kifo ni kitu kibaya ndiyo inatusumbua. Hivyo hivyo, tunapokuwa tumekwazika, tumesumbuka au kupata msongo, hatupaswi kumlaumu mtu yeyote bali sisi wenyewe, kwa sababu hivyo vinatokana na tafsiri zetu wenyewe. Kwa asiyekuwa na elimu, huwalaumu wengine pale mambo mabaya yanapomtokea, anayeanza kujifunza hujilaumu mwenyewe wakati yule aliyeelimika hamlaumu yeyote wala hajilaumu yeye mwenyewe.
Kwa mfano, ili uweze kuelewa vizuri hili la kudhibiti hisia, pata picha kati ya vitu hivi viwili,
Moja, kuna mwendesha farasi
Mbili, kuna farasi.
Kati ya farasi na mwendesha farasi nani anatakiwa kumwongoza mwingine?
Chukulia kwamba, farasi ndiyo hisia, na mwendesha farasi ndiyo akili.
Katika kufanya maamuzi, unatakiwa uwe mwendesha farasi, usikubali farasi akuongoze bali wewe yaani akili ndiyo uiongoze hisia.
Huwezi kudhibiti hisia kwenye maisha yako kwa sababu sisi binadamu ni viumbe vya hisia, ruhusu kabisa hisia zije lakini usikubali hisia zikutawale, zikusukume kufanya kitu ambacho siyo sahihi wewe kuwa mwendesha farasi mara zote kwa kuendesha hisia na siyo hisia ikuendeshe wewe.
Pale unapokutana na msongo au kujisikia vibaya hatupaswi kumlaumu mtu yeyote bali sisi wenyewe kwa sababu hivyo vinatokana na tafsiri zetu wenyewe.
Kwenye falsafa ya ustoa hakuna kusema nimeumizwa bali kuumizwa ni kuchagua mwenyewe kadiri ya maoni yako juu ya kile kilichotokea kwako.
Kuwa mtu aliyeelimika baada ya kujifunza falsafa hii, usiwalaumu watu wengine pale mambo mabaya yanapokutokea, bali mtu aliyeelimika hamlaumu yeyote wala hajilaumu yeye mwenyewe kwani mambo huwa yanatokea kama jinsi yalivyopangwa kutokea, kujilaumu au kuwalaumu wengine ni kutaka dunia iende kadiri ya matakwa yako.
Kitu kimoja zaidi, unapaswa kukumbuka kwamba, kinachotusumbua sisi siyo kitu kingine bali ni tafsiri yetu kuhusu kile kilichotokea.
Dhibiti hisia zako kwani ni kitu ambacho unakitengeneza wewe mwenyewe na hakuna anayekupa hisia hivyo huyo ni farasi wako, usikubali akuendeshe bali wewe ndiyo umwendeshe farasi kwa sababu wewe ni muendesha farasi.
Hisia yoyote ile ikija, tulia, vuta pumzi usiweke tafsiri yoyote ile, kwani utakapoanza kuingiza hisia ndiyo mambo yanaanza kukusumbua, kwa mfano, hata katika mahusiano ya kimapenzi, hakuna mtu anayemsumbua mtu bali tafsiri zetu wenyewe juu ya wale tunaohusiana nao na maana tunayoiweka au kuitoa kupitia kile kilichotokea. Mtazamo wako ndiyo chaguo lako.
Kutoka kwa rafiki na Mstoa mwenzako,
Mwl Deogratius Kessy