3093; Ugumu usio na ulazima.

Rafiki yangu mpendwa,
Maisha na mafanikio huwa ni rahisi,
Lakini watu wamekuwa wanayafanya kuwa magumu bila ya ulazima wowote.

Watu huwa wanatengeneza ugumu huo kwa kuhangaika kutafuta njia za mkato na ambazo hazihusishi kufanya kazi.

Ni jambo la kushangaza, lakini ndivyo ukweli ulivyo.
Watu wanayafanya maisha kuwa magumu pale wanapokuwa wanatafuta njia za mkato ili kukwepa kuweka kazi.

Kwa kukwepa kazi, watu wanayafanya maisha yao kuwa magumu zaidi.
Lakini kwa kukubali kuweka kazi, kwenye mambo ya msingi kwa kurudia rudia bila kuchoka, maisha yanakuwa rahisi.

Tuangalie mfano wa eneo la fedha. Ili kujiweka vizuri kwenye eneo la fedha, unahitaji kufanya mambo mawili tu rahisi; kuongeza kipato na kudhibiti matumizi.
Hayo ni rahisi kabisa ambayo kila mtu anaweza kuelewa na kufanya.
Lakini sasa, angalia vitu watu wanafanya kwenye eneo la fedha.
Mara kucheza sijui michezo gani, mara kuhangaika na aina za uwekezaji ambazo mtu mwenyewe hawezi kuelezea.
Yote hayo yanafanya zoezi zima kuwa gumu na hata kupelekea watu kupoteza fedha zaidi.

Kadhalika kwenye eneo la afya, unahitaji kufanya mambo rahisi tu ili kujenga afya bora; kula kwa usahihi na kufanya mazoezi.
Lakini unapoangalia mambo ambayo watu wanahangaika nayo kwenye eneo la afya, utashangaa kwa nini wanafanya mambo kuwa magumu zaidi ya yanavyopaswa kuwa.

Kinachofanya watu watafute ugumu kwenye maeneo mengi ya maisha yao ni kupenda vitu vipya kila wakati.
Urahisi wa maisha na mafanikio upo kwenye kufanya vitu vya msingi, kwa kurudia rudia kwa muda mrefu bila kuacha.
Wengi huwa hawana uvumilivu wa kurudia rudia yale ya msingi kwa muda mrefu. Huwa wanachoka haraka na kujikuta wamekimbilia kwenye mambo yanayoonekana ni mapya na ya kusisimua.
Huko ndiko wanafanya mambo kuwa magumu na kujichelewesha kupata matokeo waliyopaswa kuyapata.

Kwenye kila eneo la maisha yako, mafanikio hayatokani na kufanya mambo mapya na magumu, bali yanatokana na kufanya mambo ya msingi kwa msimamo bila kuacha.

Urahisi wa safari ya mafanikio upo kwenye kukubali kuweka kazi kwa muda mrefu bila kuchoka wala kukata tamaa.

Safari ya mafanikio huwa ngumu sana pale mtu anapoanza kutafuta njia za mkato na ambazo hazihusishi kufanya kazi.
Kwa kukwepa kazi na kutaka kurahisisha safari, wanaishia kufanya mambo kuwa magumu na marefu zaidi.

Kwenye kila eneo la maisha yako, jiulize mambo yapi ndiyo ya msingi kabisa kisha chagua kuweka kazi kwenye maeneo hayo kwa muda mrefu bila kuacha.
Mambo ya msingi bado yanafanya kazi na ni sahihi kwenye safari ya maisha na mafanikio.
Tukomae na hayo na kuacha kupoteza muda na nguvu kwenye njia za mkato.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe