3094; Kuchukiwa kwa unachopenda.

Rafiki yangu mpendwa,
Ili uweze kupata mafanikio makubwa sana, lazima upende sana kile unachofanya.
Ni kwa kupenda unachofanya ndiyo utaweza kukifanya kwa ukubwa na msimamo bila kuacha.
Kwa kupenda unachofanya, hakiwi tena kazi kwako, bali kinakuwa kama mchezo.
Na hilo ndiyo linalokupa mafanikio makubwa kwa uhakika.

Kupenda sana unachofanya kunapelekea kukiamini, kukikubali na kuwa tayari kukisimamia kwa kila namna.
Unakuwa tayari kwenda hatua ya ziada ili kupata matokeo ambayo ni bora.
Husikilizi yeyote anayekukatisha tamaa juu ya kitu hicho.
Kwa jinsi unavyokuwa unapenda na kukubali kile unachofanya, unashindwa kuelewa iweje baadhi ya watu washindwe kwenye kitu hicho.

Na hapo sasa ndiyo unapotengeneza changamoto ya kuchukiwa na wale ambao hawapendi kile unachofanya.
Kwa kuwa hawakipendi, hawakifanyi kwa kujituma zaidi.
Wanakifanya juu juu na wanapokutana na magumu huwa ni rahisi kwao kukata tamaa na kuacha.

Sasa kitendo cha wewe kupenda na kufanikiwa kwenye kile ambacho wao hawakipendi na wameshindwa, kinawafanya watu wahamishie chuki zao kwako.

Hilo linaweza kukuumiza sana,
Unaweza kutamani watu wangekuelewa na kukukubali kwenye kile unachofanya.
Lakini hilo lipo nje ya uwezo wako na hakuna chochote unachoweza kukifanya kubadili hilo.

Mafanikio yako kwenye kile unachofanya vizuri na unachopenda, yataleta wivu kwa wale ambao hawafanyi vizuri kwenye mambo hayo.
Wivu huo huwa unajenga chuki dhidi yako.
Wewe huna cha kufanya juu ya chuki hiyo, zaidi ya kukubaliana nayo na kusonga mbele.

Kwenye haya maisha, huwezi kuwa huru kama haupo tayari kuchukiwa kwa kile unachopenda.
Kutokuhangaika na wale wanaokuchukia kwa sababu unafanya vizuri kwenye kile unachopenda ni nguvu kubwa sana kwenye mafanikio yako.

Kwa kuwa huna cha kuwafanya watu ambao wamechagua kukuchukia, unaachana nao na kuwapotezea kabisa.
Hujali wanachukuliaje kile unachofanya.
Na unajua siyo wajibu wako kuwafurahisha watu wengine.
Hivyo unaendelea kufanya kwa ubora mkubwa kile unachopenda na kuwaachia wengine wakuchukulie vile wanavyoona inafaa kwao.

Watu wanaokuchukia kwa kile unachopenda ni watu ambao hupaswi kuwapa uzito sana.
Hiyo ni kwa sababu wanakuwa hawana lolote kubwa wanalofanya kwenye maisha yao.
Wangekuwa na makubwa wanayofanya, wasingepata muda wa kujenga chuki kwao.
Wangekuwa na ushindi kwenye maisha yao, wangetumia muda wao kufurahia ushindi huo na siyo kuchukia wengine.

Hivyo badala ya kuumizwa na wanaokuchukia kwa kile unachopenda kufanya, unatakiwa kuwaonea huruma.
Unapaswa uwaonee huruma kwa jinsi maisha yalivyo magumu kwao kiasi kwamba mafanikio pekee kwao ni kuwachukia watu waliofanikiwa.
Hebu fikiria jinsi ambavyo hayo maisha ni magumu kwa upande wao.

Pamoja na kuwaonea huruma, huna cha kuwafanya ili kuwasaidia.
Hakuna kitu utakachowaeleza wakakuelewa.
Chuki zao zitakuwa zimepelekea waamini mambo mengi kuhusu wewe ambayo siyo sahihi.
Mambo ambayo hutaki hata kuyasikia kwa sababu hakuna namna unaweza kuyabadili.

Badala ya kuhangaika na watu ambao wamekosa mwelekeo kwenye maisha yao kiasi kwamba mafanikio kwao ni kuwachukia waliofanikiwa, unatakiwa kuwapuuza na kuhangaika na mafanikio yako.

Kamwe usifikirie kupunguza mapenzi na mafanikio yako kwenye kile unachofanya ili kuwaridhisha wengine na kukubaliwa nao.
Mafanikio ni yako na siyo ya mtu mwingine yeyote.

Waache watu wahangaike na mambo yao bila kuwasumbua na usikubali kusumbuka kwa mambo ya wengine ambayo hayakufanyi wewe ufanikiwe zaidi.

Kama kuna watu ambao wamechagua mafanikio kwao ni kuwachukia wale waliofanikiwa zaidi yao, wewe ni nani mpaka uwapangie mafanikio ya tofauti kwao?
Wewe fanikiwa kwenye kile unachopenda kufanya.
Na waache wengine wakuchukie kwa kupenda kile unachofanya.
Kila mtu ashinde mechi zake.

Fanya kile unachopenda,
Simamia kile unachoamini,
Na ishi maisha yenye maana kwako.
Wengine wanakuchukuliaje kwenye hayo, siyo wajibu wako, bali wao wenyewe.
Unapofika hatua hii ya kutokujali, mafanikio na uhuru unakuwa mkubwa kwako.
Na huo unakuwa ndiyo ushindi kamili kwenye maisha yako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe