3101; Kushindwa mbele na nyuma.

Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi huwa wanaona kushindwa ni kushindwa tu.
Pale wanapopanga kufanya au kupata kitu fulani na wasikipate, hapo ndiyo wanaona wameshindwa.

Lakini hilo siyo sahihi,
Kushindwa huwa hakufanani.
Kwa uhakika ni kuna aina mbili za kushindwa, ambazo ni kushindwa mbele na nyuma.

Kushindwa nyuma ni kule ambapo kunasababishwa na uzembe. Hapo mtu anakuwa anajua anachopaswa kufanya, lakini hakifanyi.
Mambo mbalimbali yanamzuia mtu asichukue hatua kabisa.
Kwa kutokufanya, mtu anashindwa vibaya mno.

Kushindwa mbele ni pale ambapo mtu anakuwa amechukua hatua kubwa na za tofauti na vile alivyozoea.
Kwa kufanya mambo mapya na makubwa, hata kama hutapata matokeo uliyotegemea, unakuwa umepiga hatua kuelekea kwenye mafanikio unayoyataka.

Kushindwa nyuma ni kujirudisha nyuma na kwenda mbali zaidi na mafanikio unayokuwa unayataka.
Kushindwa mbele ni kujisogeza karibu na mafanikio ambayo umeyapanga.

Maisha huwa yanaendelea kuwa bora kadiri unavyokuwa unaendelea kuyafanyia kazi.
Kadiri unavyoendelea kuchukua hatua mpya na kubwa ndivyo unavyojiweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya kupata unachotaka.

Maisha huwa yanakuwa hovyo pale ambapo hakuna hatua mpya, kubwa na za tofauti zinazochukuliwa.
Pale mtu anapopanga lakini asichukue hatua ni tatizo.
Na pale mtu anapoacha kuchukua hatua mpya baada ya kupata matokeo fulani mazuri pia ni tatizo.

Ni kawaida yetu binadamu kulinda kile ambacho tayari kimeshapatikana.
Lakini inapokuja kwenye safari ya mafanikio makubwa, mashambulizi ni muhimu kuliko kulinda.
Kuendelea mbele hata baada ya kupata ushindi fulani ni hitaji muhimu sana kwenye safari hiyo ya mafanikio.

Mafanikio mara zote huwa yapo kwenye mwendo.
Hata kwenye asili, maji yanayotiririka ni bora kuliko maji yaliyotuama.
Kaa kwenye mchakato na ushindwe kwa kufanya kuliko ushindwe kwa uzembe.

Jisukume mpaka ukamue tone la mwisho la uhai wako kwenye kufanya.
Na hata kama utashindwa, kitu ambacho ni kwa muda mfupi tu, utakuwa umejifunza mengi, hivyo utakarudia tena kufanya, haitakuwa kama ndiyo unaanza, badala yake utatumia uzoefu ambao tayari ulishaupata na kuepuka makosa ya nyuma.

Sasa hebu fikiria mtu anayejisukuma kuwa bora kwa kujaribu vitu vipya na vikubwa kila mara bila kuchoka hata kama matokeo siyo mazuri.
Kitendo cha kuwa tayari kuendelea kufanya bila ya kujali matokeo yanayopatikana, ni uhakika wa mafanikio.

Shindwa kwa kufanya makubwa na kupata matokeo madogo kuliko kushindwa kwa kutokufanya kabisa.
Unaweza kuboresha kitu ambacho kimeshaanza kufanyika, huwezi kuboresha kitu ambacho hakijafanyika kabisa.

Fanya vitu vipya, vikubwa na vya tofauti kila siku bila kuacha,
Matokeo utakayoyapata ni makubwa sana.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe