3105; Anasa za watu wa kawaida.

Rafiki yangu mpendwa,
Watu wa kawaida, ambao ndiyo wengi, huwa hawapati mafanikio makubwa kwenye maisha yao.
Na sababu kubwa kabisa inayozuia watu hao wa kawaida wasipate mafanikio ni kusumbuliwa na anasa nyingi ambazo zinahamisha sana umakini wao.

Watu hao huwa wanaridhika sana haraka na vitu ambavyo hata havina tija kwenye maisha yao.
Kuwa na kazi au biashara inayowapa kipato cha kuweza kuendesha maisha yao kwa ngazi ya kawaida huwa kunawavimbisha sana kichwa.
Utawasikia kabisa wakijivunia kwamba maisha yao yanaenda.

Kwa kuweza kuingiza kipato cha kuendesha maisha, wanahamishia umakini wao kwenye vitu vingine vya kuyakamilisha maisha yao ya kawaida, badala ya kuweka juhudi kwenye kupata mafanikio makubwa kuliko waliyokwisha kufikia.

Watahakikisha wanafanya mambo wanayoyaita ya kufurahia maisha, kama kuwa na mapumziko na kutumia vilevi mbalimbali.
Hawatataka kupitwa na kitu chochote, hivyo watafuatilia kila aina ya habari na kutaka kujua yanayoendelea kwenye maisha ya wengine.
Halafu wanakuwa washauri wazuri kwa wengine, hata pale wanapokuwa hawajaombwa ushauri.

Hatua ndogo wanazokuwa wamepiga, kama hakuna mwingine katika wanaowazunguka wamezipiga, huzidi kuvimba kichwa kwa kuona wameshafika mbali sana na hivyo hawahitaji kuhangaika sana.
Wakiona jinsi ambavyo wale wanaowazunguka wako nyuma, wanaona wamefika mbali sana.

Ni watu hawa ndiyo utawasikia wakisema hawapo tayari kuweka juhudi kubwa kwenye kazi kwa sababu watapata hali ya uchoshi.
Na kwa sehemu kubwa wanakuwa sahihi kwa sababu ndani yao wanakuwa hawana tena ile kiu ya kupata makubwa.
Wanakuwa wamesharidhika na walichopata, hivyo chochote cha ziada kwao ni kujichosha kusikokuwa muhimu.

Kuelewa vizuri hilo, angalia mfano huu; umechoka baada ya kazi zako za siku na umepata muda wa kupumzika, halafu unaambiwa kuna mfuko wa simenti (wenye kilo 50) unaotakiwa kuubeba kutoka ndani kwenda nje. Kwanza hizo habari tu zitakuchosha zaidi na kuubeba mzigo huo kutakuwa kazi ngumu zaidi.
Lakini kwenye hali hiyo hiyo ya kuwa umechoka, ghafla mtu wako wa karibu akaanguka na unahitaji kumbeba kumpeleka kwenye gari ili kumwahisha hospitali, utapata nguvu kubwa ya kufanya hivyo, hata kama mtu huyo ana uzito unaozidi kilo 50.

Kwenye mfano huu tunapata funzo kubwa kwamba hali ya uchovu mara nyingi siyo ya kimwili, bali ya kifikra. Kama kitu siyo muhimu kabisa, hali ya uchovu itakuwa kikwazo kwako kukifanya.

Kubwa zaidi ni baadhi ya kauli ambazo huwa zinatumiwa na watu wa kawaida, ambazo ukishazisikia tu, unajua mafanikio makubwa kwao yatabaki kuwa ndoto.
Pale unaposikia mtu anasema analitafuta kusudi la maisha yake ndiyo aweze kujituma zaidi, unajua kabisa huyo ameshafikia hali ya kuridhika. Ukiwa na njaa kali, hufikiri kuhusu kusudi, unafikiri ni jinsi gani utapata chakula ule, njaa haina masihara na haijali kuhusu kusudi.
Kama unakwama kujituma zaidi kwa sababu hujajua kusudi la maisha yako, maana yake ni huna njaa kubwa ya mafanikio.
Njaa ya mafanikio makubwa sana ndiyo kusudi la wewe kuanza nalo, ukishakuwa na njaa hiyo, huhitaji kingine chochote ndiyo ujisukume.

Halafu kuna vitu ambavyo ukiviona au ukivisikia kwa mtu, unajua hayupo makini na wala hajajitoa vya kutosha ili kupata mafanikio makubwa.
Unaposikia mtu anaomba ushauri ni biashara gani inayolipa sana na ambayo haitamsumbua kwenye kuifanya, hapo unajua tayari hakuna mtu mwenye kiu ya mafanikio makubwa. Anataka muda mwingi wa anasa kuliko muda wa kuwekeza kwenye kujenga biashara sahihi kwake.

Kadhalika kwenye mikwamo ya vitu kama mtaji, mauzo na kupata wafanyakazi wazuri. Ukiona mtu anakata tamaa kwenye hayo maeneo, ni dalili huyo ni mtu wa kawaida ambaye mafanikio makubwa kwake yatakuwa ndoto.
Kama mtu anataka kupata mtaji mkubwa na kwa haraka ndiyo apige hatua kwenye biashara, kama anashindwa kufanya mauzo na kama analalamika hawezi kupata wafanyakazi wazuri, unajua kabisa ni mtu wa kawaida ambaye alitaka urahisi kwenye biashara ili aweze kuendelea na anasa zake nyingine.

Dalili ya uhakika zaidi ya mtu wa kawaida anayehangaishwa zaidi na anasa za maisha kuliko mafanikio makubwa ni kutaka kupendwa na kukubalika na kila mtu.
Hawa huwa ni watu wa kuiga yale wengine wanafanya, kuchukua ushauri wa kila mtu, hata kama hawajawaomba watu hao ushauri na pale wanapokosolewa wanakimbilia kujitetea.
Wakisemwa vibaya, wanakimbilia kubadilika ili wawaridhishe wengine, hata kama hilo litapelekea wasijiridhishe wao wenyewe.

Ukiwa na njaa ya mafanikio makubwa hakuna chochote kinachoweza kuwa kikwazo kwako. Mawe unayokutana nayo kwenye safari unayatumia kujenga msingi imara zaidi wa mafanikio. Na mawe ambayo wengine wanakurushia, unayatumia kuimarisha msingi wako.

Umewahi kuona moto mkali unaowaka, chochote unachoweka kwenye moto huo kinauchochea zaidi!
Hata maji ambayo yana nguvu ya kuzima moto mdogo, yamwage kwenye moto mkubwa na mkali na yatachochea zaidi moto huo.

Hivyo ndivyo wewe unavyopaswa kuwa kama unataka kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Unapaswa kuwa hatari, unapaswa kuwa na njaa na kiu kali, ambavyo haviwezi kutulizwa na chochote isipokuwa hatua unazopiga kuelekea kwenye mafanikio makubwa unayoyataka.

Nimekuwa nasema na nitarudia tena hapa, kama kuna kitu chochote kinachokupa raha zaidi nje ya mchakato wako wa mafanikio, sahau kuhusu mafanikio makubwa.
Kama unakazana kumaliza majukumu yako ili uende kwenye mapumziko yako, tayari umeshajikwamisha.
Mchakato wa mafanikio makubwa ndiyo unapaswa kuwa anasa pekee kwako kama unataka kweli kuyafikia mafanikio hayo makubwa.

Na jambo la muhimu sana la kuondoka nalo hapa ni hili; kwa vyovyote iwavyo, usikubali kuwa mtu wa kawaida.
Kataa hilo jina, kataa kuambatana na watu wa aina hiyo na zikatae kabisa tabia zote za aina ya watu hao.
Sehemu kubwa ya hii safari inaanzia kwenye fikra na mtazamo, ukiweza kuanza na ushindi hapo, ushindi kwengine unakuwa ni wa uhakika.

Mchakato wa mafanikio makubwa ndiyo unapaswa kuwa anasa kuu kwako, kiasi cha kutokuridhishwa au kuyumbishwa na chochote nje ya mchakato huo.
Ukishapata ushindi huu, kufikia mafanikio makubwa unayoyataka linakuwa swala la muda tu.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe