3106; Kitu cha kwanza kufanya kila unapoamka asubuhi.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye zama tunazoishi sasa, zama za teknolojia ambapo simu zetu janja (smartphones) zimeshika sehemu kubwa ya maisha yetu, huwa ndiyo kitu ambacho tunakigusa mara nyingi zaidi.

Huwa natania kwamba mtu anaweza kuamka asubuhi, kabla hata hajajua kama anaweza kutembea au la, tayari anakuwa ameshashika simu yake.
Na simu hizo watu wanazishika mara nyingi kuliko hata baadhi ya viungo vya miili yao.

Kwa kuwa simu hizo zina mambo mengi, mtu unaposhika ni rahisi kwenda kwenye mambo yasiyokuwa na tija kwako.
Ni rahisi kujikuta umeshaenda kwenye mitandao ya kijamii au kufuatilia habari mbalimbali.
Sasa hakuna njia mbaya ya kuianza siku yako kama kwa kufuatilia mambo ya wengine, kama mitandao ya kijamii au habari.

Hivyo basi, hata kama kila unapoamka utaishika simu yako mapema, kuna kitu nashauri kiwe cha kwanza kukifanya kwenye hiyo simu yako, ambacho kitakupa msukumo wa tofauti siku nzima.

Kitu hicho ni kuzihesabu fedha zako zote ulizonazo.
Utafanyaje hilo kwa kutumia simu nitakuambia, lakini kwanza tuanze na umuhimu wa kufanya zoezi hilo.

Wakati naanza kujifunza mambo haya ya maendeleo binafsi, nilimsoma mwandishi mmoja aliyeshauri mtu utembee na kiasi fulani cha fedha na uwe unakihesabu mara kwa mara.
Tunajua nguvu ya fikra zetu, kwamba huwa tunakuwa kile tunachofikiri kwa muda mrefu.
Hivyo kwa mtu kuhesabu fedha mara kwa mara, unakuwa unafikiri fedha kwa muda mrefu na hivyo kufanya fikra zako kukaa na mawazo hayo ya fedha, kitu chenye nguvu ya kukufanya uone fursa nyingi zaidi za kuzipata kwa wingi.

Inaweza isiwe rahisi kwako kuwa na kiasi fulani cha fedha unachohesabu kila mara.
Lakini hizi simu zetu janja, zina njia rahisi ya kuhesabu fedha zetu kila mara kwa urahisi.
Unafanya hivyo kwa kutumia aplikesheni mbalimbali za maeneo yote ambayo fedha zako zipo.

Hivyo anza kwa kuweka aplikesheni hizo kwenye simu yako kama bado hujafanya hivyo.
Kwa benki zote ambapo una akaunti, weka aplikesheni zake kwenye simu yako.
Kwa mitandao yote ya simu unayotumia huduma zake za kifedha, weka aplikesheni zake.
Halafu pia weka aplikesheni za uwekezaji wa masoko ya mitaji unayofanya. Kwa upande wetu ni UTT (vipande) na DSE (hisa na hatifungani).
Kwa kuwa na hizo aplikesheni ambapo akaunti zako zipo, ni rahisi kuangalia kiasi cha fedha kilichopo kwenye kila akaunti yako.

Hivyo basi, unapoamka asubuhi, cha kwanza kufanya unaingia kwenye hizo aplikesheni na kuangalia ni fedha kiasi gani unazo, kwenye kila akaunti na jumla.
Kwa kila akaunti, kuwa na lengo ni kiasi gani unataka kiwe huko.
Kisha kila siku angalia na kama ni pungufu, ianze siku yako kwa kujiuliza unaongezaje kiasi hicho na kufikia lengo?
Jiulize ni nini unatakiwa kwenda kuuza siku hiyo na kwa kiasi gani ili uweze kufikia lengo unalotaka?
Hapo utaianza siku kwa mtazamo tofauti kabisa.

Kama utakwama popote kwenye utekelezaji wa hilo, wasiliana na kule ambapo una akaunti zako na watakupa maelekezo sahihi ya kukamilisha hilo.
Kwa baadhi ya akaunti za benki, hasa za biashara unaweza ukashindwa kuona kwa aplikesheni, lakini ukaweza kuingia kwa mtandao na kuona, anza na hilo pia kila siku.

Usiianze siku yako kwa habari,
Usiianze siku yako kwa mitandao ya kijamii.
Usiianze siku yako kwa kufuatilia mambo ya wengine.
Bali anza siku yako kwa kuhesabu fedha zako zote (ukwasi) ulionao.
Na hapo ni kwa upande wa ukwasi zaidi, unaweza kuwa na uwekezaji mwingine uliofanya wa mali kama ardhi na majengo.
Huo siyo rahisi kuhesabu kila siku.
Unachotaka kuhesabu ni kile ambacho ni rahisi kugeuza kuwa fedha.

Kwenye ukurasa wa mbele wa simu yangu janja nina aplikesheni za Tigo pesa, Mpesa, NMB, CRDB na UTT. Nikishafungua mtandao kitu cha kwanza kufanya ni kuangalia salio kwenye akaunti zote hizo.
Na mara kwa mara kwa siku narudia kufanya hivyo, hata kama hakuna fedha mpya imeingia au nategemea iingie.
Lengo ni kuhakikisha kila wakati nafikiria malengo ya kifedha niliyonayo na pale nilipo kuyafikia.

Fanya zoezi hili kila unapoianza siku yako na mara kwa mara, lina nguvu kubwa ya kuweka fikra na mtazamo wako wa kifedha sawa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe

Aplikesheni za kifedha zilizopo ukurasa wa mbele wa simu yangu.