3109; Tarehe ya mwisho wa matumizi.

Rafiki yangu mpendwa,
Kila kitu huwa kina tarehe ya mwisho wa matumizi yake (expire date).
Hiyo ni tarehe ambayo baada ya hapo kitu hicho hakiwezi kutumika tena.

Inaanza na maisha yetu wenyewe, huwa yanaanza pale tunapozaliwa na kuisha matumizi pale tunapokufa.
Kila mtu anayo tarehe ya mwisho wa maisha yake, japo siyo rahisi kuijua.
Ila ambacho tuna uhakika nacho ni hatutaishi milele.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye vitu vyote ambavyo vimetengenezwa.
Huwa vina kipindi ambacho vinaweza kutumika vizuri, halafu vinafikia ukomo wake.
Vitu hivyo huwa vinafanya kazi vizuri sana pale vinapokuwa ndani ya muda wake wa matumizi.
Lakini muda unapoisha, vinakuwa havifai tena kutumia.
Ipo hivyo kwa vyakula, mavazi, mashine na vitu vingine vyote tunavyotumia.

Lakini sasa, kwa namna ya kushangaza, kuna vitu ambavyo tumeamua havipaswi kuwa na tarahe ya mwisho wa matumizi.
Na sehemu kubwa ni sababu na visingizio tunavyotumia kama kikwazo cha kufanikiwa.

Kwa mfano, mtu anayetumia sababu ya kuzaliwa masikini kama kikwazo kwake kufanikiwa, atatumia sababu hiyo maisha yake yote.
Kadhalika, anayetumia sababu ya kukosa mtaji kama kikwazo kwake kufanikiwa, anaitumia kipindi cha maisha yake yote.

Kwa kuangalia mifano ya asili na maeneo mengine ya maisha yetu, haiwezi kuwa sahihi.
Hivyo basi, pale mtu anapoendelea kutumia kitu bila mwisho wa matumizi, tunakubaliana kwamba siyo sababu halisi, bali ni kitu anachotumia kuficha uzembe wake.

Tukubaliane hapa ya kwamba, sababu yoyote ya kwa nini hujafanikiwa, mwisho wa matumizi yake iwe ni miaka 10 tangu unapokuwa umeanza kujitegemea au tangu umeanza kuitumia.
Hapo inategemea kipi kimeanza mapema.

Kama umeanza maisha ya kujitegemea ukiwa na miaka 20, basi sababu zako zote kwa nini hujafanikiwa, utaweza kuzitumia mpaka unapofika miaka 30.
Baada ya hapo sababu hizo zinakuwa zimefika mwisho wa matumizi yake na hapo sasa unakuwa uzembe wako.

Kadhalika, kama umekuwa unatumia sababu ya kukosa mtaji wa kuanzisha au kukuza biashara ukiwa na miaka 25, utaweza kutumia sababu hiyo mpaka miaka 35. Baada ya hapo huo sasa ni uzembe wako.

Unaweza kujiuliza kwa nini miaka 10?
Na jibu ni kwa sababu hicho ndiyo kipindi ambacho tafiti nyingi za mafanikio zinaonyesha watu huweza kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yao, kama wamejitoa kweli kweli.
Kila aliyefanikiwa sana, maisha yake yakichunguzwa inaonekana aliweka kazi kwa kipindi cha wastani wa miaka 10.

Kama unatumia sababu ya kutoka familia masikini kwa miaka 10, tayari na wewe utakuwa umeshakuwa na familia.
Sasa hapo tatizo haliwi tena familia uliyotoka, bali linakuwa wewe, maana tayari una familia.
Kama kwa miaka 10 ungelivalia njuga swala lako, ungeweza kulitatua kabisa.

Hivyo pia kwenye kuanzisha na kukuza biashara. Kama kwa miaka 10 unaimba wimbo ule ule wa kukosa mtaji, tatizo ni wewe mwenyewe.
Ni uhakika kwamba kama umeweza kuishi miaka 10, kuna shughuli mbalimbali unazokuwa unafanya za kukuingizia kipato.
Sasa unataka kuniambia kwa miaka 10 umeshindwa kabisa kuweka hata kiasi kidogo cha fedha kwa msimamo na kuweza kuanza nacho kama mtaji?
Haya, hata kama umeshindwa kwenye kujidunduliza, kwenye miaka yote 10 umeshindwa kujenga sifa ya kuaminika na wengine bila ya shaka kiasi cha wao kuwa tayari kukupa au kukudhamini upate mtaji?

Rafiki, naamini unapata picha ya kile ninachokueleza hapa.
Ndiyo maana hii safari yetu ya ubilionea tumejipa miaka 10.
Hiyo ni miaka 10 ya kupambana kwa kila namna kufikia ubilionea.
Tunaweza kutumia sababu zozote tunazotaka kwa nini mpaka sasa hatujawa mabilionea.
Lakini baada ya miaka hiyo 10 kuisha, hakuna sababu yoyote tutakayotumia ambayo itakuwa na uhalali.
Sababu itakuwa ni moja tu; ujinga, uvivu na uzembe wetu wenyewe.

Sababu yoyote unayojipa kwa nini hujafanikiwa, mafanikio yakiwa chochote unachotaka, ina uhalali wa wewe kutumia kwa miaka 10.
Baada ya muda huo sababu hiyo inakuwa imemaliza muda wake wa matumizi.
Na hapo sababu inayokuwa imebaki ni wewe mwenyewe, kwa ujinga, uvivu na uzembe wako mwenyewe.

Hilo likupe msukumo wa kupambana na kuweka sawa yale yote unayoona yanakukwamisha.
Miaka 10 ni muda wa kutosha kubadili chochote kwenye maisha yako.
Hivyo changua kama kweli unataka kuyabadili maisha yako au unataka kutafuta visingizio.
Huwezi kufanya vyote kwa pamoja, chagua kimoja na ukipe kazi ya uhakika na kitaleta matokeo ya uhakika kwenye maisha yako.

Kumbuka, una miaka 10 tu ya matumizi ya sababu au visingizio vyovyote ulivyonavyo.
Baada ya hapo, sababu ni wewe mwenyewe.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#HakunaKingineMuhimu