Hapo zamani za kale, jamii ya kiyahudi ilikuwa na misingi na sheria inayowaongoza na walikuwa amri mia sita kumi na tatu.

Ilikuwa ni ngumu kwa binadamu wa kawaida kuzishika zote.

Baadaye wakalalamika, ndipo mtume na nabii wao Musa alipoenda kuongea na Mungu katika mlima Sinai akawapunguzia amri kutoka amri zaidi ya mia sita, akapewa amri kumi tu.

Bado amri kumi ikawa ni shida kwao tena kuziishi. Lakini baadaye alipokuja Yesu, akazikusanya amri zote na kuwa amri moja tu ili kama mtu anashindwa kushika zote basi akisha moja ni rahisi.

Ndipo Yesu akaja akawaachia amri moja tu na ndiyo amri kuu kuliko zote nayo ni upendo. Ukiweza kuishi amri ya upendo ,basi umeweza kushika amri zote.

Katika falsafa ya Ustoa, tunayo misingi ambayo tukiweza kuiishi vizuri, basi tutapata matokeo mazuri.

Moja ya misingi rahisi sana kwenye falsafa ya Ustoa ,ambayo ukiishika hiyo tu unakuwa umeshika yote kwenye falsafa ya Ustoa, Marcus Aurelius anatushirikisha siku hii ya leo kutoka kwenye nukuu yake ni ;

Kama kitu siyo sahihi usifanye, na kama kitu siyo kweli, usiseme.
Nukuu,
If it is not right, don’t do it,
If it is not true, don’t say it
Marcus Aurelius

Mwanafalsa Marcus Aurelius anaposema, kama siyo sahihi usifanye maana yake anatuambia kuwa tunapaswa kufikiri kwa umakini kwa kitu chochote kile kabla hatujatenda au kufanya.
Kwa mfano, kwa chochote kile ambacho unafanya, unajiuliza, je hiki nachofanya ni sahihi?
Kama ni sahihi endelea kufanya ila kama unaona siyo sahihi usifanye wala kuendelea.

Tunajua kabisa sisi kama mabilionea mafunzoni, tunapaswa kukaa kwenye mchakato kila siku. Pale unapokuwa hukai kwenye mchakato, unajikamata wewe mwenyewe, na kujiambia hiki ninachofanya siyo sahihi.
Hivyo basi unaacha mara moja kutokukaa kwenye mchakato na kuanza kukaa kwenye mchakato.

Kama mtu anakushirikisha dili zuri lakini unahisi dili halipo sawa kadiri ya misingi unayoishi, maadili, sheria za asili na sheria za nchi kwa ujumla usifanye.

Kwa mfano, kwenye kisima cha maarifa tunayo misingi yetu ambayo tunaisimamia, ambayo ni nidhamu, uadilifu na kujituma. Kama unajikuta unaishi kinyume na misingi hiyo na unaona siyo sahihi, usifanye.

Kila wakati, swali lako unapaswa kujiuliza je, hiki nachofanya ni sahihi kweli? Na kama siyo sahihi usifanye, acha mara moja na fanya kile kilicho sahihi.

Kama una kitu unakifanya nje ya mchakato na haukupatii vitu hivi vitatu kama vile hekima, utajiri na afya acha mara moja.

Je, hiki ninachofanya hapa kinanipa hekima?
Kinanipa afya?
Kinanipa utajiri? Ukiona hakuna hata kimoja unapata, sema hapana mara moja kwa kutokufanya.

Kama kitu unachokifanya hakikupi hekima, utajiri na afya basi siyo sahihi usifanye. Unahangaika na vitu ambavyo viko nje ya mchakato wa BILIONEA MAFUNZONI, CHUO CHA MAUZO,

Ukija kwenye mahusiano, unajua kabisa uaminifu ndiyo msingi wa mahusiano, unakuwa na michepuko lakini, unajizima data kama vile hujui nini kinaendelea, kabla hujawa na michepuko au kutaka kumfanyia ubaya mwenzako, jiulize je hiki ni kitu sahihi kumfanyia mwenzangu? Ukiona unaumia, jua siyo sahihi usifanye.

Maisha ni mazuri kama una kitu cha kufurahia, ni kweli tunapaswa kufurahia maisha lakini unafanya kwa kiasi? Kwa mfano, unakunywa pombe kupindukia je, ni sahihi kufanya?
Unawapa watoto kila wanachotaka bila kuwafundisha kukosa je, ni sawa?

Wewe kama mwajiri hukai kwenye mchakato, halafu unalalamika kwamba timu yako haikai kwenye mchakato je, ni sahihi? Kama siyo sahihi usifanye.

Kama unataka kufanya kitu nje ya falsafa ya upendo, unapaswa kujiuliza, je, ni sahihi? Kuwapenda wangine wakati wewe mwenyewe hujipendi?unaona siyo sahihi usifanye, anza kujipenda wewe mwenyewe kwanza.

Mwanafalsa Marcus Aurelius anatuambia, tunapaswa kusema ukweli, anasema kama kitu siyo kweli usiseme, je wewe unasema mangapi ambayo siyo kweli?

Mpaka sasa umeshawaumiza na kuwajeruhi wangapi kwa kusema tu uongo?

Tunapaswa kuongea ukweli mara zote, na kama siyo kweli tusiseme.

Epuka sana kusambaza habari za uongo kwani habari za uongo zinakwenda kuharibu siyo tu maisha yetu hata maisha ya wengine.
Tunashiriki mara nyingi kwenye kushirikisha habari tunazopata bila hata kuhoji, kama ni kweli au siyo kweli.

Mwanafalsa wa Ustoa wa zama hizi Nassim Nicholaus Taleb anasema, kama unaona ulaghai na husemi na wewe ni mlaghai.

Nukuu, if you see fraud, and do not say fraud, you are fraud. Nassim Nicholaus Taleb.

Kuna mambo mengi ambayo yanaendelea kwenye jamii, na siyo sahihi, wewe kama unayashabikia basi na wewe unakua sehemu ya mambo hayo.

Unaona hali ya watu kutokuwa waaminifu wanadanganya kwenye mchakato na wewe upo, na wewe unakuwa miongoni mwa watu ambao siyo waaminifu.

Kitu kimoja cha kuondoka nacho hapa leo ni;

Moja, kama siyo sahihi usifanye.

Mbili kama siyo kweli usiseme.

Kwa hiyo, ukiweza kuishi misingi hii miwili tu kwenye maisha yako, utakua na maisha bora sana.
Kwa sababu matatizo yote duniani yanaanzia sehemu mbili moja ni kwa kufanya na mbili kwa kusema. Ukiwa makini na vitu hivyo viwili utakua na maisha bora sana.

Mwanafalsa wa Ustoa wa zama hizi,
Mstoa ,Mwl Deogratius Kessy