3116; Kutokuaminika na wengine.

Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi huwa wanadhani ili waaminike na wengine basi wanapaswa tu kuwa waaminifu.
Wanaona kama hawaibi, hawadanganyi au kumdhulumu mtu yeyote basi ni waaminifu.

Ni mpaka pale mtu anapokosa kitu anachokitaka sana kutoka kwa wengine ndiyo anagundua kuaminika ni zaidi tu ya kuwa na matendo ya uaminifu.

Inapokuja kwenye safari ya mafanikio makubwa, ili uaminike na wengine, lazima uwe umejitoa sana kwenye kile ambacho umechagua kufanya.
Lazima uwe unaweka juhudi kubwa kuliko ilivyozoeleka.
Lazima uwe unajua kwa kina kile unachofanya.
Na pia unapaswa kuwa na uvumilivu na ung’ang’anizi kwa muda mrefu.

Watu wanakuheshimu na kukuamini pale wanapoona wazi ya kwamba unajisukuma zaidi ya uwezo wako na mazoea.
Pale unapofanya zaidi ya ilivyozoeleka kufanyika na ukazalisha matokeo makubwa, watu wanakuheshimu na kukuamini zaidi.

Wanaweza wasikupende, hasa pale unapokuwa umefanikiwa kuliko wao.
Lakini lazima wakuheshimu kwa jinsi ulivyojitoa kwenye kile ulichofanya.

Tuchukue mfano wa mauzo.
Huwa tunasema, kama unauza kitu ambacho mteja anakihitaji na anaweza kukimudu, lakini asiwe tayari kununua, tatizo ni hakuamini.
Na kutokuamini hakutatokana sana na sifa zako, bali kutatokana na matendo yako.

Kwa mfano kama unataka kumuuzia mtu kitu, ambacho unaona kabisa anakihitaji na unajua anaweza kukimudu, mara ya kwanza utakapomwambia atakujibu hapana au hataki.
Kama utaishia hapo na kuamini kweli kwamba hataki, mauzo yako yanakuwa yamefia hapo.

Kinachokuwa kinahitajika ni uendelee kumfuatilia mteja huyo bila ya ukomo.
Uendelee kumwonyesha jinsi ambavyo kile unachouza ni muhimu kwake.
Mfanye aone anafanya makosa makubwa kwa kutokununua.
Kadiri unavyoweka kazi na ung’ang’anizi bila kuchoka wala kukata tamaa, ndivyo mtu huyo anavyozidi kukuamini.
Inafika hatua ambayo mtu anaamua kununua kwa kuheshimu na kuthamini juhudi kubwa unazokuwa umeziweka.

Siri moja ninayotaka kukupa leo, ambayo huwa haisemwi wazi ni kwamba watu waliofanikiwa huwa wanatumia hapana kama njia ya kupima kama wanaweza kumwamini mtu au la.
Pale unapokuwa kuna kitu unakitaka kutoka kwa mtu mwenye mafanikio zaidi yako, huwa jibu lake la kwanza ni hapana, hata kama kitu anakitaka kweli.
Lengo lake la kusema hapana ni kutaka kukupima una ung’ang’anizi kiasi gani.
Anataka kuona umejitoa kiasi gani kuwajibika kwenye kile unachomtaka akifanye.
Ukiishia kwenye hapana yake moja, unakuwa umepoteza heshima na imani yake kwako.
Lakini pale unapoendelea kung’ang’ana bila kukata tamaa, unajenga heshima na kuaminika ambako kunamfanya mtu huyo huyo ajibu ndiyo.

Hivyo basi rafiki yangu, ujumbe mkubwa tunaoupata hapa ni kama unataka kweli kuheshimika na kuaminika, basi unahitaji kufanya mambo mawili kila wakati kwa msimamo; kuweka KAZI kubwa na kuwa na UNG’ANG’ANIZI usiokuwa na ukomo.
Hivyo ni vitu ambavyo ukivifanya kwa uwazi kabisa, matokeo yake yanajidhihirisha kwa watu kitu ambacho kinafanya uaminike zaidi.

Inapokuja kwenye safari ya mafanikio makubwa, watu hawatakuamini kwa sababu tu unasema ukweli na una tabia njema.
Watu watakuheshimu na kukuamini pale unapoweka KAZI KUBWA na UNG’ANG’ANIZI usio na ukomo kwenye kila kitu unachochagua kufanya.

Kama kuna maeneo ambayo huheshimiki na kuaminika,
Kama kuna watu ambao hawakuheshimu na kukuamini,
Unajua wapi unakosea; huweki kasi kubwa na huna ung’ang’anizi usio na ukomo.
Ni hayo tu.

Kumbuka, siyo lazima watu wote wakupende.
Na kwa hakika, kadiri unavyofanikiwa ndivyo wengi wanakuwa hawakupendi.
Unachotaka wewe ni watu wakuheshimu na kukuamini.
Na heshima na imani vinatoka kwenye kazi na ung’ang’anizi unaokuwa nao.
Usipoteleza kwenye maeneo hayo mawili, lazima utapata mafanikio makubwa sana.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe