Barua ya XI; Kuhusu tabia za asili.

Rafiki yangu Mstoa,
Watu huwa tuna tabia mbalimbali ambazo tunakuwa nazo.
Baadhi ya tabia hizo huwa ni za asili kwetu, yaani tumezaliwa nazo, wakati tabia nyingine huwa tunaziiga.

Kuna wakati tabia tunazokuwa nazo zinakuwa kikwazo kwetu na hivyo kutaka kuzibadili.
Kwa tabia za kuiga, huwa ni rahisi kubadili. Lakini kwa tabia za asili huwa ni vigumu kuziondoa kabisa.

Mwanafalsafa Seneca kwenye barua yake kwa rafiki yake Lucilius alieleza juu ya hili la tabia za asili na jinsi ya kwenda nazo.
Karibu tujifunze jinsi ya kuwa na maisha bora kupitia falsafa hii ya Ustoa.

1. Tabia za asili zinaweza kupunguzwa ila siyo kuondoshwa kabisa.

Seneca anaianza barua akieleza mazungumzo aliyoyafanya na rafiki wa Lucilius juu ya tabia yake ya hofu anapozungumza mbele ya watu.
Anamweleza kwamba siyo kwamba hajui cha kuzungumza, anamsemea kwamba ana uwezo mkubwa. Ila kwa asili ana aibu anapokuwa mbele ya watu wengine.
Seneca anamwambia tabia ya rafiki huyo ataenda nayo kwa maisha yake yote.
Lakini anampa habari njema kwamba anaweza kupunguza madhara ya tabia hiyo kupitia mafunzo, ila hawezi kuiondoa kabisa.

Hatua ya kuchukua;
Zijue tabia ambazo ni za asili kwako kisha pata mafunzo ya kuzipunguza zisiwe na madhara kwako.
Usijiumize pale unaposhindwa kuziondosha kabisa tabia hizo, jua huwezi kuziondoa kabisa, ila unaweza kuzizuia zisiwe kikwazo kwako.

Nukuu;
“That which is implanted and inborn can be toned down by training, but not overcome.” – Seneca

“Kilichopandwa na asili kinaweza kupunguzwa na mafunzo, ila hakiwezi kuondolewa kabisa.” – Seneca

2. Tabia zetu za asili ni njia ya asili kudhihirisha ukuu wake kwetu.

Tabia tunazozaliwa nazo, ambazo kwa sehemu kubwa hatuna udhibiti nazo, ni njia ya asili kudhihirisha ukuu wake kupitia kwetu.
Seneca anatumia mifano ya wanenaji wazoefu ambao kabla ya kuongea mbele ya watu lazima kwanza watokwe na jasho wakati wengine hutetemeka.
Seneca anaeleza tabia hizo haziwezi kuondolewa kabisa kwa sababu ni njia ya asili kudhihirisha ukuu wake kupitia watu.
Kwa maneno mengine, udhaifu wowote unaokuwa nao siyo kwa sababu wewe ni dhaifu kuliko wengine, bali kwa sababu asili ina nguvu kuliko wewe.
Na asili inakukumbusha nguvu na ukuu wake kupitia udhaifu tunaokuwa nao.
Ndiyo maana hakuna namna unaweza kuondoa kabisa udhaifu wako.

Hatua ya kuchukua;
Udhaifu ulionao usikuumize ukajiona hufai. Badala yake hakikisha hauwi kikwazo kwako. Na kila udhaifu huo unapojitokeza kwako, jikumbushe jinsi asili ilivyo na ukuu.

Nukuu;
“Training and experience can never shake off this habit; nature exerts her own power and through such a weakness makes her presence known even to the strongest.” – Seneca

“Mafunzo na uzoefu haviwezi kuondoa kabisa tabia ya asili; asili inadhihirisha mamlaka yake kupitia madhaifu hayo na kuhakikisha nguvu yake inakulikana hata na walio imara.” – Seneca

3. Kuwa na mtu wa kujipima naye.

Seneca anaeleza umuhimu wa kuwa na mtu unayemheshimu ambaye unajipima naye.
Mtu huyo anakuwa ni ambaye amepiga hatua fulani ambazo ungependa na wewe kuzifikia pia.
Mwone mtu huyo akiwa pembeni yako muda wote na jiulize angesemaje kwa kila unachofanya.
Kama unachotaka kufanya siyo ambacho uliyemchagua kujipima naye anakubaliana nacho, basi usikifanye.

Hatua ya kuchukua;
Kuwa na mtu wa mfano kwenye maisha yako, ambaye amefika unakotaka kufika wewe kisha jipime naye kwa kila unachofanya. Kama kisingekuwa sahihi kwake, usikifanye.

Nukuu;
“For we must indeed have someone according to whom we may regulate our characters; you can never straighten that which is crooked unless you use a ruler.” – Seneca

“Tunapaswa kuwa na mtu ambaye tunajipima naye tabia zetu; huwezi kunyoosha kilichopinda bila ya kutumia rula.” – Seneca

Mstoa mwenzangu, kupitia barua hii tunajifunza kwa nini baadhi ya tabia tunazokuwa nazo zinakuwa ngumu sana kubadili, hata baada ya kuweka juhudi kubwa.
Ni muhimu tutambue kama ni tabia za asili basi hatuwezi kuziondoa kabisa.
Lakini hilo halimaanishi tuvumilie uzembe au kuendeshwa kwa tamaa za mwili, hivyo ni vitu ambavyo tuna udhibiti navyo.
Na kama falsafa hii ya Ustoa inavyotufundisha mahali pengine, tunapaswa kudhibiti vilivyo ndani ya uwezo wetu na kukubali vilivyo nje ya uwezo wetu.
Tuhakikishe hatukubali kitu chochote kuwa kikwazo kwenye maisha tunayotaka kuyaishi.

Kutoka kwa Mstoa mwenzako,
Kocha Dr Makirita Amani.