3120; Omba unapojua utakataliwa.

Rafiki yangu mpendwa,
Hofu imekuwa inawazuia sana watu wengi kuchukua hatua kubwa kwenye maisha yao.
Hizo ni hatua ambazo mtu anapaswa kuchukua ili kuweza kupata kile anachotaka.

Moja ya hofu ambazo zimewazuia watu wengi ni hofu ya kukataliwa.
Watu wanahofia kuomba kitu wanachokitaka kwa watu, kwa sababu wanajua kwenye kuomba wanaweza kukatakiwa.
Na hilo linapelekea waache kabisa kuomba.

Tunaijua kanuni ya kupata kile tunachotaka kutoka kwa wengine ni kuomba.
Kwa hiyo kama tutaruhusu hofu iwe kikwazo kwetu, ikatuzuia kabisa tusiombe, matokeo tunayokuwa na uhakika nayo ni kutokupata kile tunachotaka.

Njia kuu ya kuvuka hofu mara zote imekuwa ni kufanya kile ambacho mtu unahofia kufanya.
Hivyo inapokuja kwenye hofu ya kukataliwa, njia kuu ya kuishinda ni kuomba.
Na siyo tu kuomba kawaida, bali kuomba pale unapojua kabisa utakataliwa.
Hiyo inamaanisha uombe vitu vikubwa zaidi kwa wengine, ambavyo ndivyo unahofia zaidi.

Kusema tu uombe, inaweza isiwe na tija, maana utaendelea kuomba vile ambavyo umezoea kuomba, ambavyo ni vidogo na unaona kuna uwezekano mkubwa wa kuvipata.
Kwa kuomba vikubwa ambavyo unajua kabisa kwamba huwezi kuvipata, kunakuwa na ushindi mkubwa zaidi kwenye hofu yako ya kukataliwa.

Kuomba pale ambapo unajua kabisa utakataliwa kuna faida kuu tatu;
Faida ya kwanza ni kuishinda hofu ya kukataliwa. Kama ambavyo tumeshaona kwamba dawa ya hofu ni kufanya kile unachohifia.
Kadiri hofu inavyokuwa kubwa na ukafanya, ndivyo pia kuishinda kunakuwa kukubwa.
Kuvuka hofu na kuchukua hatua ni ushindi mkubwa sana, hata kama hujapata kile ulichotaka.

Faida ya pili ni kuzoea kupata majibu ya hapana. Kinachohofia tusiombe ni pale tunapoona tutajibiwa hapana. Tunaona hapana kama ni neno kali ambalo litatuumiza sana.
Lakini ni hofu isiyo na tija, kwa sababu hapana haiwezi kukuua, wala kukudhuru.
Hivyo kwa kuomba pale unapojua kabisa kwamba utakataliwa, unalizoea jibu la hapana, hasa baada ya kulipata mara kadhaa na kuona halina madhara makubwa kama ulivyodhani.
Kupata hapana nyingi kunakuimarisha uweze kupokea hapana nyingi zaidi bila maumivu.

Faida ya tatu ni kuongeza nafasi yako ya kupata kile unachotaka.
Huwa kuna kanuni kwamba ili upate ndiyo moja, lazima upate hapana nyingi kwanza. Na pale ndiyo unayotaka ni kubwa, ndivyo hapana kubwa nyingi zaidi unatakiwa kuzipata.
Hivyo kwa kuomba pale unapojua kabisa kwamba utakataliwa, ni kujiweka kwenye nafasi ya kukubaliwa pia.
Kwa sababu kupitia kuomba kwa wengi zaidi, kuna uwezekano mkubwa wa kukutana na ambao watakubaliana na wewe.

Rafiki, huwa kuna kauli inayosema mambo mazuri yapo upande wa pili wa hofu unayokuwa nayo.
Na kauli nyingine inasema hofu ni kiashiria kwamba upo kwenye njia sahihi, kwamba unachotaka kufanya ndiyo chenye ukuaji wako.
Kwa mantiki hiyo basi, kwa kila hofu unayokuwa nayo, ikabili kwa kufanya hicho unachohofia.
Kupitia kufanya unachohifia unaishinda hofu, kuzoea neno hapana na kujiweka kwenye mafasi kubwa ya kupata ndiyo.

Ni kitu gani kikubwa ambacho umekuwa unakitaka sana, ila unashindwa kukiomba kwa sababu ya kuhofia kuambiwa hapana? Karibu ushirikishe kwenye maoni hapo chini na hatua unazokwenda kuchukua ili hofu hiyo isiwe kikwazo kwako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe