3121; Nioge au nisioge?

Rafiki yangu mpendwa,
Kuna vitu ambavyo huwa unavifanya kwenye maisha yako bila ya kuwa na mjadala kama uvifanye au la.

Fikiria kuoga, ukifika wakati wa kufanya hivyo huwa hujiulizi iwapo uoge au usioge, huwa unaoga.
Kadhalika kupiga mswaki, haina mjadala, unapofika wakati wa kufanya hivyo, unafanya.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye kula, unaposhikwa na njaa, utafanya kila namna uweze kula.

Cha kushangaza sasa, wewe ambaye vitu kama kula, kuoga na kupiga mswaki unavifanya bila kuhoji, ndiye ambaye vitu vya msingi kabisa unavyopaswa kufanya bila kuhoji, unaishia kuhoji mpaka unashindwa kuvifanya.

Hebu fikiria kwenye kujenga na kukuza biashara yako, kuandaa mfumo wa kuendesha biashara au kujenga wateja waaminifu kwenye biashara yako.
Hayo ni majukumu muhimu mno kwenye ukuaji wa biashara yako, lakini cha kushangaza huwa ndiyo majukumu ambayo inakuchukua muda mrefu sana kuyafanya, kama hata utayafanya.

Kinachokukwamisha kwenye majukumu hayo siyo kwa sababu ni magumu sana kufanyika.
Bali ni kwa sababu hujaweza kuyageuza kuwa sehemu muhimu ya maisha yako ya kila siku.
Hujayageuza kuwa tabia ambayo unaifanya moja kwa moja.
Unakuwa huna haraka yoyote ya kuyakamilisha kwa wakati.
Na unakuwa hujayafanya yasiwe na mjadala bali kuyafanya.

Ili uweze kufanya yale unayopaswa kufanya ufanikiwe, unapaswa kuyajengea vitu hivi vinne;
Kwanza yafanye kuwa sehemu ya maisha yako ya kila siku, usiyaone kama ni kitu cha nje.
Mbili yageuze kuwa tabia unayoifanya moja kwa moja, bila hata ya kufikiria sana. Inapofika wakati wa kufanya unafanya bila ya mjadala.
Tatu weka hali ya haraka kwenye kuyafanya, usiwe mtu wa subira au kuahirisha kufanya, unapofika wakati wa kufanya, unafanya kwa haraka.
Nne ondoa mjadala iwapo ufanye au usifanye, inapofika kwenye kufanya, unachukua hatua mara moja bila ya mjadala wowote ule.

Kwa kuzingatia hayo manne, hakuna namna ambayo utakwama kufanya yale muhimu unayopaswa kufanya ili kupata kile unachotaka kwenye maisha yako.
Mafanikio kwako yanakuwa ni kama pumzi, ambayo hujishauri bali kuivuta.
Unachotaka zaidi kwenye maisha yako ni uhuru, hivyo unaupambania mpaka uupate kwa uhakika.

Unaporuhusu mjadala kwako binafsi iwapo ufanye kitu au usifanye, kwa sehemu kubwa hutakifanya.
Mafanikio yanajengwa pale unapofikia ngazi ya kufanya kitu bila ya kuwa na mjadala wa aina yoyote ile.
Inapohitajika kufanya, unafanya, kwa haraka na uhakika bila mjadala wala kufikiria.
Ukiweza kufikia ngazi hiyo ya ufanyaji, hakuna kinachoweza kukuzuia kufanikiwa.

Bado hatujafikia ngazi ambayo unaweza kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako bila kufanya.
Hivyo weka kipaumbele kikubwa kwenye kufanya.
Ni kupitia kufanya ndiyo unaweza kuzalisha matokeo yoyote yale unayoyataka kwenye maisha yako.

Ni vitu gani umeshafikia ngazi ya kufanya kila siku bila mjadala? Karibu ushirikishe kwenye maoni hapo chini.
Kwangu mimi uandishi ni namba moja.
Kama bado hujawa na kitu ambacho umeshaweza kufanya kwa aina hiyo, kipi ambacho ungependa kufanya kila siku bila ya mjadala? Shirikisha na uweke mpango wako wa kuhakikisha unaweza kukifanya kila siku bila ya mjadala.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe