3122; Kukosa tatizo ni tatizo.

Rafiki yangu mpendwa,
Kuna watu huwa wanajipa matumaini hewa na ambayo yamekuwa kikwazo kikubwa kwenye maisha yao.

Moja ya matumaini hewa ambayo yamewapoteza wengi ni kusubiri mpaka matatizo waliyonayo yaishe ndiyo waweze kufanya yale wanayotaka kufanya.

Wanachokuja kugundua ni kwamba pale tatizo moja linapotatuliwa, matatizo mengine yanazaliwa.
Yaani hata tu suluhisho la tatizo lililopo tayari ni chanzo cha matatizo mengine.

Mtu yeyote anayekuambia hana tatizo huenda hajawa na uelewa wa kutosha kwenye kitu husika ili kuweza kuyatambua matatizo yaliyopo.
Au mtu huyo anakudanganya kuhusu matatizo aliyonayo.


Matatizo na changamoto unazokuwa nazo ni sehemu ya maisha.
Hivyo ndivyo vinavyofanya maisha yawe na maana kuyaishi.
Ni kupitia kutatua matatizo na changamoto ndiyo mtu anayafurahia maisha yake.

Kama maisha yako yanakwenda sawa bila tatizo au changamoto zozote, hilo ni tatizo kubwa sana.
Huenda kuna namna unavyowadanganya wengine na hata kujidanganya wewe mwenyewe pia.
Huwa ni rahisi sana kujidanganya wewe mwenyewe na huwa wengi wanafanya hivyo.

Inahitaji umakini wa hali ya juu sana kuweza kuyaona matatizo kabla hata hayajawa na madhara makubwa. Hilo linawapa fursa ya kupiga hatua kubwa na kwa haraka.
Lakini kwa wale waliokosa umakini kwenye chochote wanachofanya, huwa hawayaoni matatizo mapema kabla hayajawa makubwa.
Na hilo hupelekea kuingia gharama kubwa kutatua matatizo hayo yakiwa yameshaleta madhara makubwa.

Pale unapojiona huna tatizo lolote, pata wasiwasi, hakuna namna ukawa huna kabisa tatizo lolote lile.
Kila wakati jitafakari kwa kina na jua kwa undani kila unachofanya ili uweze kuyaona matatizo kabla hayajawa wazi kabisa.
Pia kutatua matatizo unayokuwa nayo haimaanishi ndiyo umeyamaliza kabisa, bali jua umezalisha matatizo mengine kutoka kwenye suluhisho ulilopata.

Usiogope wala kuhofia matatizo unayokutana nayo kwenye maisha.
Hayo ni sehemu ya kuyafanya maisha kuwa na maana.
Yajue, yapende, yapokee na yatatue matatizo mbalimbali kwenye maisha yako na utaweza kupiga hatua kubwa sana.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe