Mpendwa mstoa mwenzangu,
Tuko katika zama za ujuaji, kila mtu ni mtaalamu kwa msaada wa mtandao wa intaneti. Kila mtu ni daktari, mwalimu, mwanasheria na vile vingine vyote unavyovijua wewe.
Watu wamekuwa wajuaji, kiasi kwamba hawataki tena kujifunza, watu wamejikuta ni wajuaji lakini hawana kitu hata wanachojua, mtu ambaye hapati hata nafasi ya kujifunza kila siku kwenye siku yake halafu anajiita anajua, anaona ameumaliza mwendo kwenye kujifunza.
Kadiri ya mwanafalsa Epictetus, mtu ambaye hawezi kujifunza ni yule mtu ambaye tayari anajua kila kitu.
Kwenye nukuu yake mwanafalsa Epictetus anasema hivi; ni ngumu kwa mtu kujifunza kile ambacho huwa anafikiri tayari anajua.
It is impossible for a man to learn what he thinks he already knows.
Epictetus.
Anguko la watu wengi liko katika ujuaji, wanajifanya wanajua wanajiona tayari wanajua kila kitu hivyo hawana haja ya kujifunza tena. Mtu ambaye amefunga akili yake kwa anajua hawezi kuwa mnyenyekevu wa kutaka kujifunza.
Wote ambao wanasema wanajua, hawajui kitu, mtu ambaye inasemekana alikuwa anachukuliwa mjuaji na mwenye hekima sana alikuwa ni mwanafalsa Socrates, yeye alionekana kama ni mtu anayejua lakini alipoulizwa alijibu kwamba, kitu pekee anachojua ni kwamba hajui kitu. Au hekima pekee aliyonayo ni kwamba hajui kitu.
Kama Socrates alikuwa ndiyo mtu mwenye hekima na anayejua zama hizo wewe ni nani leo unayesema kwamba unajua sana?
Watoto wadogo ni watoto ambao wanapenda kujifunza kutoka kwetu kwa unyenyekevu. Watoto hata kama wanajua, hawakuambii wanajua ila wanakuwa tayari kujifunza tena kwa unyenyekevu. Je, wewe unyenyekevu wako uko wapi?
Tuwe tayari kujifunza hata kwa watoto wetu, haijalishi umri ulionao, kipato au mali kuwa mnyenyekevu na jione hujui.
Watu ambao wamefanikiwa na wako kwenye orodha ya mabilionea kama Charles Munger na Warren Buffett wana umri mkubwa sana na kiwango cha mafanikio makubwa na ya juu waliyofikia wangeweza kusema ya nini kujifunza? Mbona nina kila kitu?
Lakini cha ajabu, ndiyo watu ambao wanajifunza sana mpaka leo licha ya kuwa wazee wenye zaidi ya miaka 90 na watu wanalipa kwenda kuwasikiliza hekima zao kwenye mikutano ya mwaka. Je, wewe ujuaji wako umekufikisha wapi?
Rafiki yangu mstoa, kujifunza hakuna mwisho, siku yako ya mwisho kujifunza ni pale unapokuwa hauko duniani. Kwa kuwa bado unaishi, endelea kujifunza.
Mtu ambaye amefanya makubwa Leonard Da Vinci wakati anakufa alimuomba Mungu MSAMAHA kwa kutotumia uwezo wake, na hakuna mtu ambaye amemfikia mpaka sasa kwa uwezo wake mkubwa wa akili sasa wewe ambaye hauko hata kwenye rekodi ya wajuaji duniani unasemaje unajua?
Haijalishi umefikia hatua gani kwenye maisha yako, bado kuna wigo mpana wa kuendelea kujifunza na kuwa bora zaidi kwenye kile unachofanya.
Kumbuka, kujifunza ni kama namba na namba hazina mwisho.
Mtu mwingine ambaye amefanya makubwa duniani ni Henry Ford, yeye aliwahi kunukuliwa akisema, mtu yeyote anayeacha kujifunza anakuwa mzee- haijalishi kama ana miaka 20 au 80.
Yeyote anayeendelea kujifunza anabaki kuwa kijana. Kitu muhimu kabisa kwenye maisha ni kubaki na akili ambayo haijazeeka.
Usijifunge kupata zaidi kwa kujiambia kwamba unajua kila kitu. Maisha ni kama sanaa chochote ambacho tayari unacho bado unaweza kukiboresha kwani sanaa haina ukomo.
Usiwe kama bahari mfu, bahari ambayo inapokea tu bila kutoa mwisho wa siku utakuja kujikuta haufai kwenye kila eneo la maisha yako.
Mazoea na ujuaji ndiyo yanayoua wengi. Kumbuka, kilichokufikisha hapo ulipo, ndicho kitakachokuangusha. Usiache kujifunza na usiweke mazoea na kuona kwamba umeshayapatia maisha.
Hatua ya kuchukua leo;
Moja, fungua milango ya akili yako na jione hujui na unataka kujifunza. Kujifunza ni kama kusali, hakuna siku utaacha kusali kwa sababu umesali sana, ukiacha kusali kinachofuata ni anguko la kiroho.
Mbili, kila wakati kuwa na falsafa ya unyenyekevu, jione hekima pekee ambayo unayo, ni kwamba hujui kitu.
Tatu, kubali kwamba hujui ili uweze kufundishwa. Mwalimu huwa anamwacha mwanafunzi mjuaji.
Nne, wasikilize wenye mamlaka au wale wanaokupa mafunzo ,fanya na ishi kile wanachokuambia.
Tano, jifunze umuhimu wa kuwa na kocha na rudia kusoma kitabu chako cha BILIONEA MAFUNZONI.
Rafiki na mstoa mwenzako,
Mwl Deogratius Kessy.
ASANTE sana
LikeLike
Sitaacha kujifunza kwasababu bado sijuw vingi
LikeLike
Ujuaji ni sumu ya maisha yangu
LikeLike
Kujifunza ni hitaji muhimu sana kwangu,hivyo sitaacha kujifunza
LikeLike