3128; Kazi na muda.

Rafiki yangu mpendwa,
Kuna vitu ambavyo huwa havijali kabisa kuhusu wewe na unafanya nini.
Vitu hivyo huwa vinataka mtu kuvichukulia hatua mara moja kama anataka kunufaika navyo.
Na kama mtu hatakuwa tayari kuchukua hatua kwenye vitu hivyo, haviwezi kumsubiri, bali vinasonga mbele.

Vitu vyenye sifa hizo ni vingi, lakini hapa tunakwenda kuangalia viwili ambavyo vina nguvu kubwa sana kwako. Viwili hivyo ni kazi na muda.

Kazi ndiye rafiki wa kweli.
Ni kupitia kazi ndiyo tunapata fursa ya kupata chochote tunachotaka.
Kazi huwa haijali kama unaipenda au unataka kuifanya.
Kazi inataka kufanyika.
Bila juhudi kuwekwa, hakuna matokeo yanayopatikana.
Unaweza kuikwepa kazi kadiri utakavyotaka wewe mwenyewe, lakini jua kwa uhakika hiyo kazi hakuna mahali inakwenda, inakusubiri uweze kuifanya.

Wakati wa ujana, watu wengi sana huhangaika na njia za mkato za kupata kile wanachotaka bila ya kuweka kazi.
Wanahangaika sana na njia hizo, lakini mwisho wa siku wanarudi kwenye msingi wa kuweka kazi ndiyo wafanikiwe.
Kazi haijali sana unataka au hutaki nini, yenyewe inataka ifanyike.
Kama haitafanyika, haitaondoka, itaendelea kusubiri mpaka mtu aamue kweli kuifanya.

Muda ndiyo sarafu tunayopima nayo maisha yetu.
Kadiri muda unavyokwenda, ndivyo tunavyopunguza muda wetu wa kuishi hapa duniani.
Muda huwa unaendelea kwenda bila ya kujali. Pale unapoona unapaswa kusubiri kwa sababu huna maandalizi ya kutosha, muda unaendelea kwenda.
Muda utaendelea kwenda bila ya kujali ni nini wewe unafanya au unashindwa kufanya.
Dunia haitasimama kukusubiri wewe mpaka uwe tayari, itaendelea kwenda kwa kasi yake yenyewe.
Kuchwa na kuchea, kila siku, ndiyo mwendo wa dunia.
Kadiri unavyoelewa mapema umuhimu wa muda na kufanyia kazi, ndivyo unavyojiweka kwenye nafasi nzuri ya kupata kile unachotaka.

Muda utaendelea kwenda, utake au usitake, muda unakwenda.
Kazi inahitajika kufanywa, upende au usipende.
Yazingatie sana hayo mawili ili uweze kuyatumia vizuri kwenye kupata kile unachotaka.
Weka kazi na muda kwa msimamo mkali, na utaweza kujipa uhakika wa kupata chochote unachotaka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe