3130; Hata usipofanya, bado yatatokea.

Rafiki yangu mpendwa,
Sababu nyingi tunazojipa kwa nini tumeshindwa kufanya mambo ya tofauti na makubwa siyo sahihi.
Huwa ni visingizio tu vya kujifariji kwa namna ambayo hatutaumia kwa uzembe wetu wenyewe.

Hivi karibuni nilikuwa natoa mafunzo ya mauzo kwenye moja ya timu tunazozifundisha.
Nilichowafundisha ilikuwa ni dhana ya kuwasiliana na wateja kiurafiki.
Katika kukamilisha hilo niliwaelekeza kuanza mazungumzo yao kwa maelezo; “Nilikuwa nakufikiria…”
Kuanza mazungumzo kwa maelezo ya aina hiyo kunaondoa hali ya kupingwa na wateja na kuweza kuimarisha mahusiano ya muuzaji mteja.

Baada ya kueleza kwa kina kuhusu mpango huo wa mawasiliano na wateja, mmoja wa wauzaji ambaye ni mwanamke alisema hataweza kutumia mkakati huo, hasa kwa wateja wake ambao ni wanaume.
Aliendelea kueleza kwamba akiwaambia wanaume alikuwa anawafikiria, basi watadhani wanataka nao mahusiano na hivyo watawatongoza.

Ukiangalia sababu ambayo muuzaji huyo alitoa, ni ya kweli kabisa.
Lakini je hiyo inatosha kuamua kutokufanyia kazi kabisa mkakati huo?

Nilimuuliza muuzaji huyo ni mara ngapi ametongozwa na wanaume, nje kabisa ya mchakato wa mauzo?
Alijibu ni mara nyingi tu hilo hutokea.
Hivyo nikahitimisha kwa kumwambia, kitendo cha wewe kuwa mwanamke, kinamaanisha mara kwa mara utakutana na watu ambao watakutongoza. Hiyo ni nje ya mauzo kabisa.
Hivyo kama hata nje ya mauzo mtu atatongozwa, ya nini ahofie ndani ya mauzo?
Nilichowaeleza ni kwamba wafanyie kazi mkakati huo bila kuhofia hilo la kutongozwa, kwa sababu linawatokea hata nje ya mauzo.
Niliwasisitizia kufanya kile kilicho sahihi mara zote.

Hilo limenifanya nifikiri ni mara ngapi watu wanajizuia kufanya vitu, kwa hofu ya vitu ambavyo bado vinamtokea mtu hata kama hachukui hatua hizo ambazo anazikwepa.
Kwa mfano mtu ambaye anaacha kufanyia kazi mikakati ya kujenga mafanikio makubwa kwa sababu hataki kujitesa. Lakini ukweli ni maisha tu yanaendelea kumtesa mtu huyo, nje kabisa ya mkakati huo wa mafanikio.
Sasa kama maisha tu yataendelea kukutesa, kwa nini mtu usiwe tayari kujitesa zaidi ndani ya muda mfupi ili uweze kujenga maisha ya tofauti?
Siyo kwamba maisha hayo ya tofauti yataondoa mateso, yatayabadilisha tu. Naamini unapata kile ninachojaribu kukuambia.

Mfano mwingine ni watu ambao huwa wanakataa kufanyia kazi ushauri wa kufanya kazi kwa muda mrefu zaidi ili kuweza kukamilisha mengi.
Watu hao hutumia kisingizio cha afya, kwamba kufanya kazi kupitiliza kutaharibu afya zao.
Lakini unapoyaangalia maisha yao kwa karibu, unaona wazi jinsi ambavyo tayari wanafanya vitu vingi vinavyoathiri afya zao.
Utakuta wanakula vyakula visivyo vya kiafya, wanatumia vilevi, wanajiweka kwenye mazingira hatarishi ya kupata magonjwa au ajali.
Yaani unapomwangalia mtu, unaona jinsi ambavyo maisha yake ya kawaida tu ni hatarishi kwa afya yake. Lakini ni mtu huyo huyo ambaye atakataa kuchukua hatua inayomwezesha kupiga hatua kubwa zaidi, kwa kisingizio hicho cha afya.

Wapo watu ambao wanaepuka kuchukua hatua kubwa mpya za kimafanikio, kwa kuhofia kwamba wakishindwa basi watu watawacheka.
Ambacho wanajisahaulisha ni kwamba tayari watu wanawacheka na kuwadharau kwa pale walipo sasa.
Wengine watakataa kujisukuma zaidi kwenye kazi zao kwa kisingizio cha kutaka kuwa na mlinganyo wa kazi na maisha (work life balance) wakati watu hao hao hawana hata hayo maisha ya kuyawekea mlinganyo.

Rafiki yangu mpendwa, kitu kimoja kikubwa sana ninachotaka uondoke nacho hapa ni hiki; usikubali kujizuia kuchukua hatua za kimafanikio unazojifunza. Kwani sababu yoyote unayojipa, tayari inakuathiri hata bila ya kuchukua hatua hizo unazohitajika kuzichukua.
Hivyo basi, kila hatua nzuri unazojifunza kwenye safari yako ya mafanikio, ziweke kwenye utekelezaji mara moja. Usikubali kukwamishwa na kitu chochote kile.

Matokeo ambayo unayakwepa kwa kutokufanya, tayari unayapata hata kabla hujafanya.
Suluhisho pekee ni kufanya kwa ubora na uhakika ili kuweza kupata matokeo mapya na bora.
Sababu na visingizio havijawahi kumpa mtu yeyote mafanikio.
Usiwe mtu wa sababu na visingizio, kuwa mtu wa kufanya.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe