3136; Ukatili wa asili.

Rafiki yangu mpendwa,
Asili huwa inafanya maamuzi yake kwa namna yake yenyewe.
Maamuzi yanayofanywa na asili huwa hayaangalii matakwa ya watu.

Kama asili ingekuwa ni mtu kwenye hayo maeneo yote yanayofanyiwa maamuzi, angeonekana kuwa mtu mwenye roho mbaya sana na asiyejali.
Hiyo ni kwa sababu watu watakuwa na maelezo mengi na mazuri ambayo wanajua yatamnasa mtu akubali, lakini asili huwa haifanyi mambo yake kwa kuangalia watu wanataka au wanafikiria nini.

Ili kuelewa zaidi fikiria mifano hiyo hapo chini.

1. Panda juu ya mti mrefu au jengo refu kisha jiachie uelee hewani kama ambavyo ndege huwa wanafanya, kisha upime matokeo yake. Utaishia kuwa na anguko kubwa na litakalokuumiza sana. Hata kama wewe ungejali kiasi gani, asili haijali, kuna nguvu ya mvutano ambayo inavuta vitu vyote kwenda chini, bila ya kujali ni kitu au mtu gani.

2. Misitu huwa inashika moto mara kwa mara na kuunguza mimea na viumbe wengine wengi. Hii ni njia ya asili ya kusafisha mazingira yake pale yanapokuwa hayajasafishwa kwa muda mrefu.
Moto unaowaka kwenye misiti hiyo unaweza kuwa na madhara makubwa, lakini asili haijali, inakuwa inahitaji zaidi kujisafisha.

3. Ukiwaangalia wanyama simba na swala unapata picha ya jinsi ukatili wa asili ulivyo dhahiri.
Simba huwa wanawala swala, ni chakula muhimu kwao.
Unapoona simba wengi wakiwa hai, maana yake hapo ni swala wengi wamegeuzwa kuwa chakula kwa simba hao.
Kadhalika unapowaona swala wengi wakiwa hai, kuna simba ambao hawajapata chakula.
Haijalishi swala atatamani kiasi gani kuishi, simba anapotokea kitakachomwokoa ni mbio zake.
Pale simba anapokuwa anamkimbiza swala, kila mmoja anakimbia kwa ajili ya uhai wake. Simba anamkimbiza swala ili kupata chakula, wakati swala akimkimbia simba ili kunusuru maisha yake.

Kwa mifano hiyo michache, tumejionea dhahiri jinsi asili inavyofanya mambo yake bila kujali.
Asili inafanya kile kilicho sahihi kwa wakati sahihi, bila kujali kama watu wanataka au hawataki.

Hivyo pia ndivyo unavyopaswa kufanya kama unataka kujenga na kutunza mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Mara zote fanya kile kilicho sahihi.
Kwa muda mfupi kuna fursa unaweza kuzipoteza kwa kusimamia yale yaliyo sahihi, lakini utapata fursa nyingine kubwa na nyingi baadaye kwa kusimamia yaliyo sahihi.

Nyooka kama asili ilivyonyooka na utajiepusha na changamoto nyingi ambazo watu huwa wanazitengeneza pale wanapofanya maamuzi kwa kutumia hisia badala ya fikra.
Binadamu tunajua kudanganyana kwa kutumia hisia, ila asili huwa haidanganyiki kwa hisia zetu.

Unapotaka mambo makubwa na muhimu yafanyike, unajua wazi kwamba lazima ufanye kile kilicho sahihi mara zote.
Huwa kunakuwa na mwingiliano mwingi unaogusa hisia katika maamuzi hayo, lakini wajibu wetu ni kuvuka hisia hizo ili kufanya maamuzi sahihi.

Unapoamua kunyooka kama asili ilivyonyooka, unapoamua kufanya yaliyo sahihi mara zote bila kujali watu wanataka au kujisikiaje, utaonekana kama mtu mwenye roho mbaya sana.
Kama haupo tayari kuchukuliwa kama mtu mbaya na mwenye roho mbaya, tayari unakuwa umepishana na mafanikio makubwa.

Kama unataka kupata mafanikio makubwa, halafu pia hutaki kuonekana una roho mbaya, tayari unakuwa umeshashindwa.
Mafanikio makubwa huwa hayaendani na matakwa ya walio wengi.
Kwa sababu wengi ni wavivu na wazembe na huwa wana sababu na visingizio vingi kwenye kila jambo.
Ukisikiliza na kupokea sababu na visingizio hivyo, hakuna hatua yoyote kubwa utakayoweza kupiga.

Chagua kwenda kama asili inavyoenda, nyooka kwenye mambo yako yote, hakikisha maamuzi unayofanya hayaathiriwi na hisia zako binafsi.
Kwa kwenda hivyo utaweza kufanya makubwa sana, lakini inahitaji ngozi ngumu ya kuvumilia maneno mengi mabaya yatakayosemwa kuhusu wewe.
Asili inaendelea kufanya mambo yake wakati wote bila kujali tunaichukuliaje.
Hivyo ndivyo tunavyopaswa kuwa pia.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe