3138; Malengo potoshi.

Rafiki yangu mpendwa,
Kila mtu kwenye maisha ana malengo.
Wanaofanikiwa wanakuwa na malengo.
Kadhalika pia kwa wale wanaoshindwa, huwa wanakuwa na malengo pia.

Hapa unaweza kujiuliza tofauti ya watu inatokea wapi kama wote wana malengo?
Jibu ni kwamba tofauti inaanzia kwenye ubora wa malengo.
Watu wanaofanikiwa huwa wanakaa chini na kuweka malengo sahihi kwao, kisha kuyafanyia kazi mpaka yanakuwa halisi.
Wakati wale wanaoshindwa huwa hawakai chini na kuweka malengo, badala yake wanafanyia kazi yale ambayo wengine pia wanafanyia kazi.

Hayo ndiyo ninayoyaita malengo potoshi.
Ni malengo yanayompotosha mtu, anaona kama kuna mahali anaenda, lakini kiuhalisia hakuna.
Mtu anaweza kuweka juhudi kubwa kwenye hayo malengo, lakini hakuna mahali anakwenda.
Ni sawa na mbio za panya, ambazo hata akipata ushindi, bado anabaki kuwa panya.

Malengo potoshi ni mengi sana kwenye zama tunazoishi sasa.
Mengine watu wanayaweka wao wenyewe, bila ya kujua kwamba wanajipotosha na kujipoteza.
Na mengine watu wanaiga na kufuata mkumbo, kitu kinachowachosha sana, lakini hawapigi hatua yoyote kubwa.

Moja ya maeneo ambayo malengo potoshi yamewapoteza wengi ni kwenye biashara.
Kuna watu wengi wapo kwenye biashara kwa miaka mingi, wanajituma sana kwenye biashara hizo, lakini hakuna hatua kubwa wanazokuwa wanapiga.
Tatizo kubwa linakuwa ni malengo potoshi wanayokuwa nayo.

Moja ya malengo potoshi kwenye biashara ambayo yanawapoteza wengi ni kudhani mafanikio kwenye biashara ni kuwauzia wateja wengi zaidi.
Hivyo wanachofanya ni kukimbilia kupunguza zaidi bei pamoja na kuwapa wateja mkopo.
Wanapima mafanikio kwa wingi wa wateja wanaokuwa wanawauzia.
Na hapo wanaweza kuwa wanawauzia wateja wengi sana, lakini bado hawafanikiwi kwenye biashara.
Zaidi wanachoka sana na kusumbuka na wateja hao wengi ambao wanakuwa na kazi kubwa ya kuwafuatilia.

Malengo mengine potoshi kwenye biashara ni kufanya mauzo makubwa iwezekanavyo.
Hapa watu wanakazana sana kuuza, bila kujali ubora wa mauzo wanayofanya.
Wanauza kweli kwa wingi, lakini biashara hazipigi hatua, badala yake zinakuwa zinarudi nyuma zaidi.
Wanakuwa wanauza kwa bei ya punguzo sana ambayo mtu akiweka gharama zote hakuna faida inayobaki.
Na mbaya zaidi, wanauza kwa mikopo kwa wateja ambao hawana hata uwezo wa kulipa kwa wakati.
Kinachotokea ni biashara kuwa inapoteza fedha kwenye kila mauzo, kitu kinachopelekea biashara kushindwa na kuanguka.

Kwa kuwa watu wanakuwa hawajui jinsi malengo wanayokuwa nayo yanavyokuwa potoshi, wanashindwa kuelewa kwa nini biashara zao zinashindwa licha ya juhudi kubwa wanazoweka.
Hapo ndipo watu hujikuta wakiamini mambo ya kishirikina kama ‘chuma ulete’ na mengine yanayoendana na hayo.

Wengi huhangaika sana na hali hizo za kibiashara, lakini wanashindwa kuzitatua, kwa sababu hawagusi chanzo kikuu, ambacho ni malengo potoshi.

Mafanikio makubwa kwenye eneo lolote la maisha yanaanza na malengo sahihi, ambayo yanafanyiwa kazi kwa usahihi na matokeo kupatikana.
Malengo sahihi kwenye biashara ni kutengeneza fedha nyingi zaidi na siyo kuuza kwa wateja wengi zaidi.
Na fedha nyingi ambayo biashara inatengeneza siyo kwenye mauzo, bali kwenye faida.

Hivyo basi, ili biashara iweze kupata mafanikio makubwa, sharti kuu ni moja, lazima itengeneze faida kubwa zaidi iwezekanavyo.
Faida ndiyo pumzi ya biashara.
Ikiwepo biashara inaendelea kuwa hai na kukua.
Ikikosekana biashara inadhoofu na kufa.

Hivyo kwenye biashara unapaswa kuanza na lengo la faida halisi unayotaka kutengeneza na hiyo ndiyo itaamua uuzie wateja wa aina gani na wangapi na uuze kwa kiasi gani.

Hii ni hesabu ngumu ambayo wengi hawapendi kuipiga, lakini urahisi haujawahi kumpa mtu mafanikio makubwa.
Wengi huenda na safari ya mafanikio kama ndege mbuni anavyoenda na maisha yake.
Pale anapokutana na hatari au kitu asichoelewa, anafukia kichwa chake kwenye mchanga.
Kadhalika kwenye maisha ya wengi, pale wanapokutana na magumu au changamoto, wanajifanya kuzipuuza kama vile zitapotea.
Kinachotokea ni magumu na changamoto hizo kukua na kuleta madhara makubwa.

Kama hujakaa chini na kujiwekea malengo kwa kukokotoa hatua zote unazopaswa kuchukua na magumu na changamoto unazopaswa kuvuka, unachofanyia kazi siyo malengo halisi.
Hayo ni malengo potoshi, ambayo ni usumbufu mkubwa sana kwako.
Malengo potoshi ni usumbufu kwa sababu yanakuweka ‘bize’ unajiona kama kuna hatua unazopiga, kumbe unajipoteza tu wewe mwenyewe.

Malengo sahihi ya biashara kwako yanapaswa kuanzia kwenye fedha nyingi kiasi gani unachotaka kutengeneza kwenye biashara hiyo kupitia faida halisi.
Kama kwa kuanza tu kufikiria hivyo unajisikia vibaya, unaona siyo sahihi kufikiria fedha nyingi kiasi gani unaweza kutengeneza kwenye biashara basi jua upo kwenye biashara kimakosa.
Ni biashara inayoingiza faida ndiyo inayoendelea kuwepo na hata kukua.
Unaweza kusali, kutambika na kuzindikwa utakavyo, lakini kama huna hesabu kamili za kutengeneza faida kwenye biashara yako, upo tu kwenye mbio za panya.
Unafanyia kazi malengo potoshi ambayo ni usumbufu kwako, hakuna mahali yanakupeleka.

Kama upo kwenye biashara na huna hesabu kamili za jinsi gani unaingiza faida kubwa iwezekanavyo, hujui unachofanya.
Unafuata tu mkumbo kama kondoo wanaoelekea kwenye machinjio na utaishia kwenye kifo cha kibiashara.
Acha kila unachofanya leo na rejea kwenye meza ya mchoro wako wa biashara na kupitia hesabu yako ya kutengeneza faida kubwa iwezekanavyo.
Kisha hakikisha hatua zote unazochukua kwenye biashara, zinaendana na lengo hilo.
Hiyo ni kuanzia kwenye aina ya wateja unaochagua kuwauzia, bei unayouza na gharama ambazo biashara inaingia.

Kwenye kila eneo la maisha yako epuka sana malengo potoshi.
Utayajua ni malengo potoshi kama unaweka juhudi kwa muda mrefu ila badala ya kwenda mbele unabaki pale ulipoanzia au kurudi nyuma kabisa.
Malengo sahihi kwako yanakupeleka mbele kadiri unavyoweka juhudi kubwa kwenye kuyafanyia kazi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe