Barua ya XIV; Kuhusu kujitenga na dunia.

Rafiki yangu Mstoa,
Inapokuja swala la kuishi kifalsafa, watu wengi wanaweza wasikuelewe.
Unapochagua kuishi maisha ambayo ni ya tofauti na wengine, inaleta hali ya kushindwa kuelewana nao.

Hilo linaweza kupelekea mtu kutamani kujitenga na dunia ili kuondokana na hali hiyo ya usumbufu.
Lakini hilo siyo sahihi, kwa sababu pamoja na kuishi kwa misingi unayochagua, bado unahitaji kuendelea kushirikiana na watu wengine.
Lakini pia unapaswa kuwa na tahadhari ili watu hau wasikushawishi kuwa tofauti na misingi unayoiishi.

Hapo ndipo penye mtego mkubwa ambapo wengi wamenasa, kushindwa kushirikiana na wengine bila kuvunja misingi yao.
Wachache huamua kujitenga kabisa na dunia ili isiwaathiri na wengi huishia kufuata mkumbo na kuwa kama kila mtu.

Kwenye barua ya 14 ambayo Seneca aliandika kwa rafiki yake Lucilius, alimshirikisha namna bora ya kukwepa mtego huo, ili kuweza kuishi misingi ya falsafa huku akishirikiana na wengine bila kuathiriwa nao.

Karibu tujifunze mambo ya kuzingatia ili tuishi misingi yetu ya falsafa kwa utulivu mkubwa huku tukishirikiana na wengine kwenye mambo yote muhimu.

1. Tusiwe watumwa wa miili yetu.

Seneca anasema huwa tunaipenda sana miili yetu na hivyo kuitunza kwa kila namna.
Anaeleza hakuna ubaya wowote kwenye kuitunza miili, lakini hatupaswi kuwa watumwa wa miili yetu.
Anasema mtu anayekubali kuwa mtumwa wa mwili wake, anaishia kuwa mtumwa wa watu wengi.
Anasisitiza mapenzi yaliyopitiliza kwa miili yetu yamekuwa chanzo kikubwa cha hofu na wasiwasi ambao watu wanakuwa nao, kitu kinachoathiri maisha yao.
Seneca anamalizia kwenye hili akisema kwamba tunapaswa kuithamini miili yetu, lakini pale inapohitajika kuitoa kafara kwa sababu za msingi, tuwe tayari kufanya hivyo.

Hatua ya kuchukua;
Mwili wako ni nyumba ya nafsi yako, hupaswi kuithamini nyumba kuliko wewe mwenyewe. Hivyo utunze vizuri mwili, lakini usiwe mtumwa wa mwili wako, usiendeshwe na mambo ya kimwili.
Starehe za mwili zimekuwa kikwazo kwa wengi, ukiweza kuzikwepa utakuwa na utulivu mkubwa.

Nukuu;
“We should conduct ourselves not as if we ought to live for the body, but as if we could not live without it.” – Seneca

“Tunapaswa kuyaendesha maisha yetu siyo kama tunaishi kwa sababu ya mwili, bali kama hatuwezi kuishi bila ya mwili.” – Seneca

Nukuu hiyo inaonyesha nafasi sahihi ya mwili kwetu, siyo ndiyo kitu pekee, bali ni kitu muhimu. Tukielewa na kuishi hilo, tutaenda vizuri sana.

2. Aina tatu za hofu.

Seneca anasema watu wanapenda kuepuka usumbufu na hatari ndiyo maana huwa wanaamua kujitenga na dunia, kwa kudhani wanapofanya hivyo wanaondokana na hofu zote.
Anaeleza kuna aina tatu za hofu; hofu ya matakwa, hofu ya maradhi na hofu ya ukatili wa wengine.
Katika hizo, hofu ya ukatili wa wengine ndiyo kubwa na inayosumbua zaidi, hasa kutoka kwa wale wenye nguvu au mamlaka makubwa.
Hofu ya ukatili ndiyo huwa inawasukuma watu wengi kutaka kujitenga na dunia, ili kuepuka kusumbuliwa na kuteswa na wale wenye nguvu kuliko wao.
Lakini hata kwa kufanya hivyo bado huwa haisaidii.

Hatua ya kuchukua;
Ni muhimu kujua ni aina ipi ya hofu inayokusumbua zaidi na kukusukuma kwenye maamuzi unayofanya.
Hofu ya matakwa na maradhi zinaanzia ndani, lakini hofu za ukatili zinahusisha wengine. Hivyo unapaswa kuzikabili hofu hizo kwa utofauti.

Nukuu;
“If I am not mistaken, there are three main classes of these: we fear want, we fear sickness, and we fear the troubles which result from the violence of the stronger.” – Seneca

“Kama sijakosea, zipo za aina tatu; hofu ya matakwa, hofu ya maradhi na hofu ya ukatili wa wenye nguvu.” – Seneca

3. Epuka kutengeneza maadui.

Kwenye kuepuka hofu ya tatu, ya ukatili wa wale wenye nguvu, Seneca anashauri tuepuke sana kutengeneza maadui.
Hiyo inaanza kwa kuepuka kuwakosea wengine, hasa wale ambao wana nguvu na mamlaka.
Seneca anasema mtu mwenye hekima huwa hachochei hasira kwa wale wenye mamlaka, bali huwa anahakikisha anakwepa hilo.
Anasisitiza siyo lazima kujenga urafiki na watu hao, kwani ni jambo litakalochosha, muhimu ni kutokujenga nao uadui.
Lakini pia kwenye kuepuka kujenga nao uadui, hupaswi kuonekana wazi wazi unawakwepa watu hao. Kwani kitendo hicho kinaweza kuibua hasira kwao na kupelekea kukuumiza kwa mamlaka waliyonayo.
Kama ambavyo nahodha hawezi kuelekeza chombo kwenye dhoruba, ndivyo pia hupaswi kuyaelekeza maisha yako kwenye matatizo.

Hatua ya kuchukua;
Ili kuvuka hofu ya ukatili wa wengine, epuka kujenga uadui na watu, kwa kutokuchochea hasira kwao. Lakini pia usionekane kama unawakwepa wale ambao hutaki kujenga uadui nao, kwani hilo linaweza kuchochea hasira kwao na kuishia kwenye uadui.

Nukuu;
“It is burdensome to keep the friendship of all such persons; it is enough not to make enemies of them. So the wise man will never provoke the anger of those in power.” – Seneca

“Ni kazi kujenga urafiki na watu wote; inatosha tu kutokujenga nao uadui. Hivyo ntu mwenye hekima kamwe hachochei hasira kwa wale wenye mamlaka.” – Seneca

4. Kujilinda na wengine, usiwe na kitu wanachoweza kukunyang’anya.

Kwenye mwendelezo wa kuvuka hofu ya ukatili wa wengine, hasa wale wenye mamlaka au kundi kubwa la watu, Seneca anashauri tusiwe na kitu ambacho wanaweza kutunyang’anya, yaani chenye manufaa kwao.
Seneca anasisitiza kwanza tusiwe na tamaa kama zao, maana hizo ndiyo huleta migogoro.
Halafu sasa tusiwe na kitu chochote ambacho wanaweza kutunyang’anya, ambacho kinakuwa na manufaa kwao.
Anatupa mfano kwamba mtu anayepita njiani usiku akiwa mikono mitupu, hakuna anayeweza kumpora. Lakini yule anayepita akiwa amebeba kitu chochote, anakaribisha wahalifu kumpora na hata kumuumiza.

Hatupaswi kutafsiri hili kama kuishi maisha ya kutokuwa na kitu chochote, bali tunapaswa kuendesha maisha yetu kwa namna ambayo hatuweki kila kitu chetu wazi.
Kwa sababu mara nyingi sana watu hukaribisha matatizo kwao wenyewe kupitia kuweka mambo yao wazi.
Pale watu wanapojua kila kitu kuhusu wewe, ndivyo wanavyoweza kukusumbua na kukuharibia.

Hatua ya kuchukua;
Kuwa na tahadhari kubwa ya mambo yako yanakuwa wazi kwa watu gani. Tunza taarifa zako nyingi kwako binafsi ili kuepuka wengine kuzipata na kuzitumia kukudhuru.
Ishi maisha yanayoonekana ya kawaida ili kuepuka watu wenye hila kukuwinda kwa kuona wanaweza kunufaika kupitia wewe.

Nukuu;
“Again, let us possess nothing that can be snatched from us to the great profit of a plotting foe. Let there be as little booty as possible on your person.” – Seneca

“Hatupaswi kumiliki chochote ambacho tunaweza kunyang’anywa na wenye hila kwa manufaa yao. Kuwa na umiliki mdogo iwezekanavyo wa vitu unavyoweza kunyang’anywa.” – Seneca

5. Vitu vitatu vya kuepuka kwa nguvu kubwa.

Kuhakikisha hutujengi uadui na watu, ambao wanaweza kutudhuru, kuna vitu vikubwa vitatu ambavyo Seneca anatushauri tuviepuke kwa nguvu kubwa. Vitu hivyo ni chuki, wivu na dharau.
Anatuambia hekima pekee ndiyo inayoweza kutuonyesha jinsi ya kuepuka vitu hivyo vitatu.
Wivu huwa unaleta chuki na chuki huwa inaleta dharau.
Hivyo kwa kuanza kwa kuepuka wivu, tunaweza kuepuka hivyo vinyine kwa urahisi.
Seneca anasisitiza kwamba kama hatutaki dharau ya wengine itusumbue, basi pia tusilewe sifa au heshima wanazotupa. Ukiweza kuchukulia kawaida heshima wanayokupa wengine, utaweza pia kuchukulia kawaida dharau wanayoweza kukuonyesha.
Lakini kama utathamini sana heshima yao, dharau pia itakuumiza sana.

Hatua ya kuchukua;
Ishi maisha yako na waache wengine nao waishi maisha yao. Usijilinganishe na wengine, maana hiyo ndiyo njia ambayo inazalisha wivu kwa haraka.
Usiwe na chuki wala dharau kwa wengine. Na ili dharau za wengine zisikuukize, usifurahishwe na sifa au heshima zao kwako.

Nukuu;
“Let us withdraw ourselves in every way; for it is as harmful to be scorned as to be admired.” – Seneca

“Tunapaswa kujiepusha na mengi kadiri iwezekanavyo; kwa sababu ni hatari kudharauliwa kama ilivyo kuheshimiwa.” – Seneca

6. Falsafa ndiyo kimbilio.

Seneca anatuambia kimbilio la yote ambayo tumeyaona ni falsafa. Kwa sababu falsafa inaheshimiwa na wote, wema na wabaya.
Mara nyingi falsafa huwa haiibui uadui kwa watu kama mazungumzo ya aina nyingine.
Kutokana na utulivu wa faslafa na namna ambavyo haimlazimishi yeyote kuwa vile inavyotaka, watu wote huiheshimu.

Lakini Seneca anatutahadharisha kwamba tunapaswa kuishi falsafa kwa utulivu na kiasi. Kwa sababu tukitumia falsafa kama kitu cha kutaka tuonekane sisi ni bora kuliko wengine, tutaishia kuibua uadui usio na maana.
Hivyo falsafa inaweza kuwa kimbilio la uhakika kwetu kama tutaitumia kuyaboresha maisha yetu na siyo kuitumia kuwapangia wengine jinsi ya kuendesha maisha yao.

Hatua ya kuchukua;
Chagua kuishi kwa falsafa ya Ustoa ambayo inayafanya maisha yako kuwa bora. Lakini epuka kutumia falsafa kuwapangia wengine jinsi ya kuendesha maisha yao, utatengeneza maadui wasio na msingi.

Nukuu;
“One must therefore take refuge in philosophy; this pursuit, not only in the eyes of good men, but also in the eyes of those who are even moderately bad, is a sort of protecting emblem.”

“Mtu anapaswa kuifanya falsafa kuwa kimbilio lake; kwa sababu ndiyo alama ya ulinzi kwa watu wema na hata wasio wema.” – Seneca

7. Vipi kuhusu kujihusisha na siasa?

Kwenye barua hii, Seneca pia amegusia swala la kujihusisha na siasa kama mwanafalsafa.
Anatoa mifano ya wanafalsafa kwa pande zote mbili, ambao walijihusisha na siasa na ambao walijitenga na siasa kwa lengo la kuzalisha kazi za kifalsafa ambazo zitakuwa na manufaa kwa wengi.
Hitimisho lake ni kila kitu kinapaswa kuwa kwa kiasi, kama ilivyo kwenye mambo mengine, mwanafalsafa unapaswa kujihusisha na siasa kwa kiasi.
Seneca anasema, mtu mwenye hekima havurugi tamaduni za wengine, lakini pia hajionyeshi kama yeye ni tofauti sana na hao wengine.
Kila kitu kinapaswa kufanyika kwa kiasi ili mtu kutokusumbuliwa na wengine.
Anamalizia kwa kusema mtu mwenye hekima huwa anafanya kila kitu kwa sababu, hivyo tunapaswa kujihusisha na siasa pale tunapokuwa na sababu maalumu. Tukijua kwamba matokeo yanaweza kuwa nje ya uwezo wetu, ila sababu ya kufanya, ipo ndani ya uwezo wetu.

Hatua ya kuchukua;
Fanya kila kitu kwa sababu na fanya kwa kiasi. Usifanye kwa kufuata mkumbo na wala usifanye kwa kutaka kuonekana zaidi ya wengine. Hayo ndiyo huwa yanaleta matatizo kwa wengi.

Nukuu;
“And finally, the wise man regards the reason for all his actions, but not the results. The beginning is in our own power; fortune decides the issue.” – Seneca

“Mtu mwenye hekima huwa na sababu mwenye matendo yake yote, lakini hawezi kudhibiti matokeo ya matendo hayo. Kuanza kupo ndani ya nguvu zetu; lakini asili ndiyo inayoamua.” – Seneca

8. Unachokitamani sana, huwezi kukifurahia.

Seneca anamaliza barua hii kwa kutushirikisha kauli aliyojifunza kutoka kwa mwanafalsafa Epicurus, kwamba anayeufurahia utajiri ni yule ambaye hautaki sana.
Hiyo ina maana kwamba, kadiri mtu anavyokuwa hana tamaa na kitu, ndivyo anavyokifurahia na kuwa na maisha bora.

Hakuna hisia mbaya kwenye maisha kama tamaa. Kwa sababu unapokuwa na tamaa ya kitu, huwa unadhani kwamba kwa kukipata utakifurahia na maisha yako kuwa bora. Lakini matokeo huwa tofauti, pale unapopata kile ulichotamani sana, ndiyo unazidi kutamani vingine zaidi.

Seneca anasema kinachowafanya wale wanaoutaka sana utajiri kutokuufurahia ni kwa sababu wanakuwa na wasiwasi wa kuupoteza. Hivyo kadiri wanavyopata utajiri, ndivyo wanavyozidi kupata hofu na wasiwasi, ambao wanadhani watauondoa kwa kupata utajiri zaidi.
Na hivyo ndivyo maisha yao yote yanavyoenda, wanakuwa na utajiri mkubwa, lakini ambao hawaufurahii kwa sababu mara zote wana hofu na wasiwasi wa kuupoteza.

Hatua ya kuchukua;
Tafuta utajiri lakini usiwe na tamaa nao. Ufurahie wakati unao na kuwa tayari kuupoteza. Jiamini kwamba kama umeweza kuutengeneza, utaweza kuutengeneza tena hata ukiupoteza. Na maisha yako hayabadiliki kwa namna yoyote ile iwe una utajiri au huna, kwa sababu tayari yamejitosheleza.

Nukuu;
“He who needs riches least, enjoys riches most.” – Epicurus
“Yule ambaye hauhitaji sana utajiri, ndiye anayeufurahia zaidi.” – Epicurus

“He who craves riches feels fear on their account. No man, however, enjoys a blessing that brings anxiety; he is always trying to add a little more. While he puzzles over increasing his wealth, he forgets how to use it.” – Seneca

“Yule anayeutamani sana utajiri anaishia kuwa na hofu. Hakuna mtu anayeweza kufurahia kitu kinachompa hofu; kwani kila mara anakuwa anakazana kuongeza. Wakati mtu anahangaika kuongeza utajiri anasahau jinsi ya kuutumia.” – Seneca

Rafiki yangu Mstoa, barua hii imetufungua sana jinsi ya kuishi kwa misingi yetu ya kifalsafa huku tukiendelea kuchangamana na watu wengine.
Maana lengo la falsafa ni kuwa na maisha bora, na hatuwezi kuwa na maisha bora kama hatuna maelewano mazuri na wengine.
Tukizingatia haya tuliyojifunza hapa, tutaweza kuwa na maisha bora sana kupitia falsafa ya Ustoa tuliyochagua kuiishi kwa maisha yetu yote.

Kutoka kwa Mstoa mwenzako,
Kocha Dr Makirita Amani.