3139; Dola.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwa zama tunazoishi sasa, sifa za utajiri huwa zinapimwa kwa thamani ya dola za Kimarekani.
Huenda hilo likaja kubadilika kwa zama zijazo, ila kwa sasa hicho ndiyo kipimo.

Hivyo basi, inapokuja kwenye kiwango cha utajiri ambacho mtu amefikia, thamani inayotumika ni ya dola.
Na kinachopimwa ni thamani ya fedha na mali zote ambazo mtu anamiliki baada ya kuondoa madeni yote anayodaiwa.

Lengo kubwa tulilonalo hapa ni kila mmoja kufika thamani ya utajiri wa ngazi ya ubilionea.
Hiyo ikiwa na maana kwamba thamani ya utajiri wa dola bilioni moja na kuendelea.

Hili ni lengo kubwa sana na gumu kufikia, lakini linawezekana, kwa sababu wapo watu wengine ambao wameweza kulifikia.

Hatua ambayo ni muhimu sana kwenye hili lengo ni kuelewa ukubwa wake.
Wengi wanapotaja ubilionea, wanaona ni rahisi kwa kufikiria kwa thamani ya shilingi.
Lakini unapofikiria kwa thamani ya dola na kuigeuza kwa shilingi, ndiyo unaona ukubwa wake halisi.

Hapo chini ni ngazi za utajiri kwa thamani ya dola ukilinganisha na shilingi, kwa wastani wa manadilishano ya dola kwa shilingi kwa mwaka 2023;

1. BiliONEA (USD bilioni 1+, TSH trilioni 2.5+)
2. MiliONEA (USD milioni 1+, TSH bilioni 2.5+)
3. LakiONEA (USD laki 1+, TSH milioni 250+)
4. ElfuONEA (USD eflu 1+, TSH milioni 2.5+)
5. MiaONEA (USD 100+, TSH 250,000+)
6. KumiONEA (USD 10+, TSH 25,000+)
7. UnaniONEA (USD chini ya dola 10, Tsh chini ya 25,000)

Hiyo ngazi ya saba nimeiongeza tu, lakini ni kiashiria cha mtu ambaye amefulia kabisa, yaani ambaye hana kitu.

Sasa unaweza kujionea wewe mwenyewe ukubwa wa lengo tunalopambania, ambalo ni kubwa kiasi cha kutosha bajeti ya baadhi ya wizara za serikali.

Lakini hilo lisikushtue, kwa sababu sisi tunayo kanuni rahisi sana ya kumla ng’ombe.
Tunamchinja na kumkata vipande vidogo vidogo kisha kula kipande kimoja kwa wakati mpaka ng’ombe huyo anaisha.

Lengo letu kuu la ubilionea lipo pale pale, lakini tunaligawa kwenye vipande na kipande chetu cha kwanza kabisa kupigania kwa juhudi za kila aina ni ngazi ya ULAKIONEA yaani utajiri wa dola laki moja na kuendelea au shilingi za Kitanzania milioni 250 na kuendelea.

Ngazi ya ulakionea, licha ya kuwa ndogo ukilinganisha na lengo la ubilionea, huwa ndiyo ngazi ngumu sana kuweza kuifikia.
Mtu anapoweza kutoboa ngazi hiyo, huwa ni rahisi sana kwake kufika umilionea, kwa kipindi kifupi kuliko alichotumia kufika ulakionea.

Na hatua nyingine ngumu huwa ni kutoka utajiri wa milioni moja mpaka milioni 100, lakini baada ya hapo kufika ubilionea ni rahisi zaidi.

Sasa turudi tunapoanzia kwa sasa, ngazi ya ulakionea.
Charlie Munger, bilionea na mmoja wa wawekezaji bora kabisa kuwahi kutokea amewahi kunukuliwa akisema;
“Kupata dola 100,000 za kwanza ni kitu kigumu sana, lakini huna budi kukifanya. Sijali inabidi ufanye nini ili kupata kiasi hicho – kama itakubidi kutembea kwa mguu kila unakoenda na kutokula chochote ambacho hujakinunua kwa bei ya punguzo, tafuta njia ya kupata kiasi hicho cha dola 100,000. Baada ya hapo unaweza kupunguza kidogo makali ya zoezi hilo.

Ujumbe mkuu wa Charlie Munger hapo ni kupambana kuongeza kipato, huku ukidhibiti sana matumizi yako, hasa kwenye hatua za awali.
Ni kweli huwezi kufikia ubilionea kwa kubana matumizi, lakini kwenye hatua za awali, hiyo ni tabia muhimu sana kujijengea.
Kwa sababu siyo tu itapunguza matumizi yako ya fedha, bali pia itakupa fokasi kubwa kwenye safari yako.
Kwa sababu matumizi mengi huwa ni usumbufu.

Naye bilionea anayejitafuta, Alex Hormozi anasisitiza sana kwenye ngazi hiyo ya kwanza ya ulakionea, akishauri hatua za mtu kuchukua ili kufika hapo.
Hormozi anasema;
“Kama huna angalau dola 100,000 kama akiba yako na ungependa kufikia ngazi hiyo kwa haraka;
1) Acha kula chakula cha kununua. Nunua vitu kwa bei ya punguzo pekee.
2) Acha kununua nguo mpya. Tumia hisani au msaada pekee.
3) Hudhuria matukio ya marafiki ya bure pekee. Kama hawaungi mkono malengo yako (ya ubilionea), hao siyo marafiki zako.
4) Tumia muda wako wote kuomba kazi na kujifunza ujuzi mpya utakaokuwezesha kuingiza kipato zaidi.
5) Mwangalie mtu anayefanya kazi kwa juhudi kuliko wote, kisha wewe fanya kazi mara mbili zaidi yake.
Kisha subiri kwa miezi 36.”

Anachosema Hormozi ni kile kile alichosema Munger, ila tu hormozi ameongeza mambo ya kufanya.

Tunachokwenda kufanya sisi kwenye programu ya bilionea mafunzoni ni;
1. Kuchagua mfumo wa uwekezaji wa UTT kama mahali pa kuweka hiyo dola 100,000 ndani ya miaka mitatu ijayo. Najua kwa wengi ukikusanya thamani ya vitu vingi ambavyo tayari unavyo, unavuka hiyo dola laki moja. Tutakachokwenda kupima ni kwenye uwekezaji wa UTT pekee.
2. Kupunguza sana matumizi yetu, kununua vile tu ambavyo tusiponunua tutakufa. Chochote kinachoweza kusubiri, kinapaswa kusubiri kwa muda mrefu iwezekanavyo.
3. Kuchagua biashara moja ambayo tutaweka mtu utaweka juhudi zako zote kwenye kuifanya na nusu ya faida unayopata kila mwezi unaipeleka kwenye mfuko wa UTT. Muda wako wote wa siku nzima unakuwa kwenye biashara yako. Siku yako ya kibiashara inaanza saa 10 alfajiri na kuisha saa 2 usiku, siku 6 za wiki. Muda mdogo unaopata wa kupumzika ni kwa ajili ya mapumziko tu na siyo kwa anasa zozote.

Tunakwenda kuzingatia hayo matatu siyo tu kwenye ngazi ya ulakionea tunayoanza nayo, bali kwa kipindi chote cha maisha yetu yaliyobakia.
Hivyo biashara tunazochagua kufanya zinapaswa kuwa kitu ambacho tunapenda sana kufanya ili tuwe tayari kufanya muda wote na siyo kukimbilia mapumziko na starehe.
Pia ziwe biashara ambazo zina fursa kubwa ya ukuaji kadiri muda unavyokwenda ili juhudi kubwa tunazoendelea kuweka zitufikishe kwenye lengo.

Kanuni kuu ya kujenga utajiri ni ile ile, ambayo haitakuja kubadilika. Ongeza sana kipato chako huku ukidhibiti sana matumizi yako.
Na nyongeza, chagua kitu ambacho unapenda sana kufanya na unaweza kulipwa kwa kukifanya kisha tumia muda wako wote kufanya kitu hicho kwa ubora na upekee sana.
Zingatia hayo na hakuna kitakachoweza kukuzuia kupata utajiri unaoutaka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe