Pale mtu anapoanza kujifunza falsafa ya Ustoa na kupata uelewa kidogo, kila mtu anayemuona haishi falsafa ya Ustoa anakuwa anaona kama kuna kitu anakosa. Anataka alazimishe hata watu ambao wanahusiana nao, waishi pia falsafa ya Ustoa kwa nguvu.

Ni kama vile mtu ambaye anasoma kitabu kimoja kuhusu mafanikio, anatoka hapo na hamasa kubwa na kutaka pia wengine wapate kile ambacho yeye amepata.

Wakati tunajifunza haya masomo hapa kwenye kisima cha maarifa, tunatamani sana na wale wanaotuzunguka wawe kama sisi. Siyo kitu kibaya, ni kitu kizuri sana.

Tunatamani hata watu wetu wa karibu kama vile wenza, watoto waweze kujifunza hii misingi tunayojifunza hapa. Wakati mwingine unakasirika kuona wale ambao unataka wawe kama wewe hata hawaoneshi hali ya kujali.

Muda ambao wewe unaamka unataka watu wako wa karibu pia nao waamke, jinsi unavyopambana wewe kuanzia kwenye kujifunza, kufanya kazi basi unapata msukumo mkubwa ndani yako wa kutamani kuona yale mazuri ambayo unayapata wewe uyaone na kwa wengine pia.

Hali hii ya kuona wengine wanaenda kinyume na wewe, inaweza kukuletea hasira ndani yako na hata kupelekea kugombana nao kama usipoweza kudhibiti hasira zako.

Tunapaswa kukubaliana na asili, hatuwezi kuwa kama wengine na wengine nao hawawezi kuwa kama sisi. Kama sisi tunafanya kazi kuliko watu wote hatuwezi kuwasukuma na wengine wafanye kazi zaidi yetu yaani waende hatu ya ziada kuliko sisi.

Falsafa ya Ustoa imetuandalia mazingira mazuri kati yetu sisi na wale ambao tunahusiana nao. Je, tufanye nini pale watu wetu wa karibu wanaposhindwa kwenda na sisi?

Aliyekuwa mtawala wa Roma na Mwanafalsafa wa falsafa ya Ustoa, Mwanafalsafa Marcus Aurelius aliwahi kunukuliwa akisema,

Wavumilie wengine na kuwa mkali kwako mwenyewe.

Be tolerant with others and strict with yourself.” – Marcus Aurelius

Kama watu wengine hawawezi kwenda kama wewe wala usiwalazimishe, bali wavumilie na wewe usijionee huruma. Kwa mfano, kama wewe unaweza kula mara moja kwa siku, na wale wanaokuzunguka hawawezi, basi wavumilie lakini wewe endelea na kile ulichochagua kufanya bila kujionea huruma.

Kama wewe unaweza kufanya kazi zaidi ya watu wengine kwenye biashara yako vizuri, endelea kufanya bila kujivumilia na kwa upande wa wengine, wavumilie.

Usipowavumilia wale ambao unahusiana nao, utaishia kuumia tu, hivyo tumia nafasi hiyo kujisukuma wewe zaidi kuliko wengine.

Kwa mfano, wako ambao wanaweza kusoma kitabu kimoja kwa mwezi badala ya kuwasema kwa nini wanajinyima fursa nzuri ya kujifunza, wewe kuwa mkali zaidi kwako kwa kusoma kitabu kimoja kwa siku au kwa wiki.

Kama kuna watu wengine hawajitumi kwenye lengo la UBILIONEA, MAUZO, jitume sana wewe mwenyewe kuwa wa kwanza kuwaonesha inawezekana na wao wavumilie.

Kwa mfano, wewe kama mmiliki wa biashara, unapaswa kuwa mtu namba moja kwenye kila eneo la biashara yako. Kwa mfano, ukija kwenye mauzo, wewe ndiyo unauza zaidi kuliko wengine, kwenye kupiga simu, wewe ndiyo unapaswa kupiga simu nyingi zaidi kuliko wengine hata wengine wasipokufikia wavumilie lakini wewe usijivumilie bali unapaswa kwenda hatua ya ziada.

Kama kuna watu ambao wakitajwa wanafanya kuliko watu wengine basi uwe wewe lakini hata kama wengine hawafikii viwango vyako unapaswa tu kuwavumilia lakini wewe usijivumilie nenda hatua ya juu zaidi.

Kwa mfano, kama wewe ni mwandishi, na watu wengi hawaandiki kila siku, wewe andika kila siku bila kujihurumia na wale ambao hawaandiki kila siku wavumilie tu.

Waache watu wengine watoe sababu,
Waache watu wengine walalamike,
Waache watu wengine wawe waongeaji ,
Lakini wewe, usiwe kama wao bali wewe kuwa mtu wa kuonesha matokeo na siyo sababu.

Ukishakuwa mtu ambaye unafanya zaidi ya wengine kwanza utajenga ushawishi mkubwa hata kwa wale ambao wanakuzunguka. Wale ambao wanakuzunguka au unaohusiana nao, unakuwa unateka mioyo yao kupitia ufanyaji wako. Watakuogopa na kukuona huyu si mtu wa kawaida na itakua rahisi wewe mambo yako kwenda mbele kwa sababu wewe unafanya zaidi yao.

Lakini, biashara ya wewe kujivumilia halafu unakuwa mkali kwa wasaidizi wako hiyo haitakiwi katika falsafa ya Ustoa.

Hatua ya kuchukua leo;
Wavumilie wengine kwenye mambo yote lakini kwako wewe mwenyewe usijivumilie bali kuwa mkali zaidi kwenye maeneo haya manne;

Moja, fanya kazi kuliko mtu mwingine yeyote yule (outwork)

Mbili, jifunze kuliko mtu mwingine yeyote yule (outlearn)

Tatu, tawala kwenye kile unachofanya kuliko mtu mwingine yeyote yule yaani hodhi (outmanage)

Nne, uza zaidi kuliko mtu mwingine yeyote yule ( outsale)

Kitu kimoja zaidi, fanya zaidi ya wengine, usiruhusu sababu yoyote ile, bali chukua hatua kubwa, bila hofu wala kutoruhusu sababu yoyote ile.
Yaani wewe ndiyo uwe bora zaidi kwenye kile unachofanya kiasi kwamba hakuna atakayeweza kukupuuza. Teka mioyo ya watu kwa kufanya zaidi yao. Waache wao wafanye kimazoea, wewe fanya kwa ukubwa.
Kwa mfano, kama watu wengine wanafanya biashara moja na wewe, wewe jitofautishe kwa kutumia maarifa unayopata hapa kwenye CHUO CHA MAUZO na BILIONEA MAFUNZONI kuhakikisha unakuwa bora zaidi kuliko kuwa na maarifa halafu mtu ambaye hana maarifa anakuzidi tena kwa ubora, hiyo itakua haina maana ya wewe kuendelea kukaa hapa.

Ni mimi mstoa mwenzako,
Mstoa Mwl Deogratius Kessy