3162; Kufanya na kutokufanya.

Rafiki yangu mpendwa,
Kila mtu huwa anakosea kwenye maisha.
Hayupo hata mmoja ambaye anapatia mara zote.
Tunachotofautiana ni aina ya makosa, ukubwa na madhara.

Hapa tutaangalia aina ya makosa na jinsi yanavyowatofautisha watu kwenye matokeo wanayopata.

Kuna aina mbili za makosa.
Aina ya kwanza ni makosa ya kufanya. Hapa ni pale unapofanya kitu halafu ukakosea.
Aina ya pili ni makosa ya kutokufanya.
Hapa ni pale unapokuwa umekosea kwa kutokufanya kitu ambacho kilipaswa kufanyika.

Kwenye aina hizo mbili za makosa, makosa mazuri ni yale ya kufanya kuliko ya kutokufanya.
Hiyo ni kwa sababu unapofanya na ukakosea, kuna vitu unavyojifunza ambavyo utakapokuja kufanya tena utaboresha zaidi.
Unapofanya na ukakosea, wakati mwingine hautarudia makosa hayo hayo na hivyo kuzidi kufanya kwa usahihi.

Lakini pale unapokuwa haufanyi kabisa, hakuna chochote unachokuwa unajifunza.
Sana sana unakuwa umezidi kujijengea hofu ya kufanya.
Kadiri unavyokuwa hufanyi, ndivyo pia unavyozidi kuhofia kufanya.
Utajiona kama unaepuka makosa, lakini kumbe unafanya makosa makubwa zaidi.

Tuangalie kwenye eneo la mauzo jinsi linavyoweza kuathiriwa na kufanya au kutokufanya.
Wauzaji wote wanajua mambo yanayopaswa kufanyika ili kuuza zaidi.
Ni kutengeneza wateja wapya tarajiwa wengi zaidi (kwa kupiga kelele), kuwageuza wateja tarajiwa kuwa kamili (kwa kuwaambia wanunue), kuwahudumia vizuri (kwa kuwapa ahadi kubwa na kutimiza) na kuwa na ufuatiliaji endelevu (angalau kila wiki kumfikia mteja).

Lakini wengi wamekuwa hawafanyi hayo, kwa kuhofia kukosea.
Hawapigi kelele zaidi kwa kudhani wataonekana wanachouza siyo sahihi.
Hawawaambii watu wanunue kwa sababu wataonekana wana tamaa.
Hawaahidi makubwa kwa sababu wanahofia watashindwa kutimiza.
Na hawafuatilii kwa uendelevu kwa kuona watakuwa wanawasumbua wateja.
Kwa kutokufanya yote hayo, matokeo wanayopata yanajulikana, ni mauzo kuwa madogo zaidi.
Hapo mtu anakuwa amekosea zaidi kwa kuepuka kukosea.

Tukiangalia upande wa pili, ambapo mtu amefanya na akakosea kweli, tunaona picha ya tofauti.
Muuzaji anayepiga kelele zaidi, hata kama ataonekana anachouza siyo sahihi, lakini wengi zaidi watajua nini anachouza.
Anayewasisitiza watu wanunue, hata kama ataonekana ana tamaa, kuna wateja watasukumwa kununua kwa huo msisitizo wao.
Anayeahidi makubwa sana, hata kama atashindwa kuyatimiza, atajua nini anapaswa kufanya ili kutekeleza.
Na anayefanya ufuatiliaji endelevu kwa wateja mpaka anaonekana ni msumbufu, wateja hawawezi kumsahau.

Kwa vyovyote vile utakosea.
Kwa kufanya utakosea.
Na kwa kutokufanya pia utakosea.
Ni bora ukosee kwa kufanya, kwa sababu kuna wengi watajua unachofanya kupitia hayo makosa yako na wewe utajifunza kufanya kwa ubora zaidi.

Na muhimu zaidi kwenye maisha ni bora kuchukiwa kuliko kupuuzwa.
Kwa sababu anayekuchukia anakuwa anakujua, hivyo pamoja na chuki zake, anajua unafanya nini.
Anayekuchukia ataenda mbele zaidi na kukusema vibaya kwa wengine, ambao nao pia watakujua hata kama walikuwa hawakujui.
Lakini kupuuzwa ni kupotezwa.
Anayekupuuza hakujui, hakuongelei kwa wengine kwa vyovyote vile na hivyo hakuna anayejua uwepo wako na unafanya nini.

Usijione mstaarabu sana kwa kuepuka kufanya ili usikosee, huko kwenyewe tayari ni kukosea, ambako hata hakuna manufaa.
Ni bora ukose ustaarabu kwa kufanya na ukakosea, kwa sababu utajifunza kufanya kwa ubora zaidi na wengine watajua unachofanya.

Thomas Edison alikosea zaidi ya mara elfu kumi kwenye kugundua taa ya umeme.
Mwandishi wa habari alipomuuliza aliwezaje kuendelea kufanya licha ya kukosea zaidi ya mara elfu 10?
Edison alimjibu; sijakosea mara elfu 10, bali nimejifunza njia elfu 10 ambazo hazifanyi kazi na hivyo kutokuzirudia tena.

Kumbe kufanya na ukakosea unakuwa hujakosea, bali unakuwa umejifunza kile ambacho hakifanyi kazi.
Wakati mwingine hutarudia tena kufanya kwa namna hiyo hiyo.
Badala yake utaboresha zaidi.
Na hapo unakuwa hujakosea, bali umejifunza na kuwa bora zaidi.

Makosa makubwa mawili ambayo watu wengi wanayarudia rudia kwenye maisha ni kutokufanya kabisa au kukata tamaa baada ya kufanya na kukosea.
Njia ya kuvuka makosa hayo ni kufanya kwa mwendelezo bila kuacha.
Kila unapofanya unajitathmini na kuangalia wapi pa kuboresha zaidi unapofanya tena.
Ukienda hivyo kwa muda mrefu, utayafuta makosa mengi na kuishia kuwa bora zaidi.

Kosea kwa kufanya, utajifunza mengi zaidi kuliko kukosea kwa kutokufanya.
Kwenye mauzo, kosea kwa mambo utakayowafanyia wateja kuliko kutokufanya kabisa.
Usipofanya utajiona uko sahihi, lakini wateja ambao wangejua uwepo wako hata kwa makosa hawatajua.
Lakini unapofanya na ukakosea, wengi zaidi watajua uwepo wako hata kwa hayo makosa yako.
Halafu uzuri ni utapata nafasi nyingine ya kusahihisha makosa ambayo umefanya.
Utaweza hata kuomba msamaha na kufanya kitu cha kufidia, ukiwa tayari umeshajulikana.
Kitu ambacho hakiwezekani kama hata hujulikani kama upo.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe