3164; Uchumi wa biashara.

Rafiki yangu mpendwa,
Biashara nyingi sana zinazoanzishwa huwa zinaishia kufa ndani ya muda mfupi tangu kuanzishwa kwake.
Na hata zile ambazo hazifi, nyingi zimekuwa hazipati ukuaji mkubwa, badala yake zinabaki kuwa ndogo.

Sababu nyingi zimekuwa zinatolewa juu ya biashara kufa.
Na ya kwanza kabisa ambayo imekuwa inasemwa sana ni ushindani mkali.
Karibu wote ambao biashara zao zimeshindwa wamekuwa wakitaja ushindani mkali kuwa chanzo kikuu cha biashara zao kufa.

Hali mbaya ya uchumi pia imekuwa inatumiwa kama sababu ya biashara nyingi kufa.

Lakini sababu zote hizo ambazo zimekuwa zinatolewa, zimekuwa siyo kiini hasa cha biashara kufa.
Zinaweza kuwepo, lakini zinakuwa zimemalizia tu, chanzo halisi kinakuwa kingine.

Chanzo halisi kinachopelekea biashara kufa ni kuwa na uchumi mbaya.
Hapa haimaanishi uchumi kwa ujumla, bali uchumi wa biashara moja moja.
Maana halisi ya uchumi ni udhibiti wa rasilimali haba.
Inapokuja kwenye biashara, jinsi rasilimali haba kwenye biashara zinavyodhibitiwa, ndiyo inapelekea biashara kufa au kupona.

Kuna rasilimali haba nyingi kwenye biashara. Kuanzia fedha, watu, muda na hata vitendea kazi mbalimbali.
Katika rasilimali hizo nyingi, ya kwanza na yenye athari kubwa zaidi kwenye biashara ni mzunguko wa fedha.
Mzunguko wa fedha ndiyo rasilimali yenye madhara makubwa kwenye biashara kama haitadhibitiwa vizuri.

Kifo cha biashara karibu zote huwa kinaanzia kwenye udhibiti mbaya wa mzunguko wa fedha.
Uchumi sahihi wa biashara kwenye mzunguko wa fedha ni fedha zinazoingia zinapaswa kuwa nyingi kuliko zinazotoka kwenye biashara.
Kuingia ni kupitia mauzo na kutoka ni kupitia matumizi.

Biashara yoyote ile yenye mapato makubwa kuliko matumizi, ina nguvu ya kuendelea kuwepo sokoni na kukabiliana na changamoto nyingine za soko.
Lakini biashara ambayo matumizi ni makubwa kuliko mapato, hiyo tayari ipo kwenye shimo la kifo, ni swala la muda tu kabla haijazikwa.

Huwezi kulaumu ushindani pale mzunguko wa fedha kwenye biashara unapokuwa hasi, yaani matumizi kuzidi mapato.
Hapo ni kwamba tu biashara imeshindwa kufanya kazi.
Ushindani utamalizia tu kile ambacho tayari kimeshaanza.

Kwa maana hiyo basi, ushindani wa kwanza kwenye biashara ya aina yoyote ile ni mauzo madogo na matumizi makubwa.
Pale mauzo yanapokuwa madogo na matumizi yakawa makubwa, ni uhakika biashara imeshindwa na haitaweza kudumu kwa muda mrefu, hata kama ipo yenyewe kwenye eneo ambapo ipo.

Lakini biashara inapokuwa na mauzo makubwa huku matumizi yakiwa madogo, inakuwa na nguvu ya kuweza kupambana sokoni.

Kabla hujahangaika na mambo mengi ya nje ya biashara yako, hebu anzia ndani.
Hebu anzia kwenye uchumi wa biashara yako.
Je kwa mauzo yanayofanyika, biashara inaweza kuendelea kujiendesha yenyewe?
Na je kwa matumizi yaliyopo, biashara itaweza kwenda kwa muda mrefu kiasi gani?

Unaweza kuwa na mauzo makubwa sana, lakini kama gharama za uendeshaji ni kubwa, bado biashara itashindwa.
Hili ndilo wafanyabiashara wengi wadogo wamekuwa hawalielewi na hivyo kusema kuna chuma ulete.

Kadhalika kama gharama za kuendesha biashara zipo chini, hata kwa mauzo ambayo siyo makubwa, bado biashara inaweza kuwa na nguvu kubwa ya kushindana sokoni.

Unaweza kuhangaika na mengi sana kwenye biashara yako, lakini kama hutapatia kwenye uchumi wa msingi wa biashara, bado tu itashindwa.

Weka umakini wako mkubwa kwenye kujenga uchumi sahihi wa biashara yako, kwa kuhakikisha kila wakati mapato ni makubwa kuliko matumizi.
Kwa kusimamia vizuri mzunguko wa fedha, changamoto nyingine nyingi zinazoua biashara nyingi zinakosa nguvu kwenye biashara yako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe