3165; Huruma

Rafiki yangu mpendwa,
Huwa kuna taratibu mbalimbali ambazo huwa tumejiwekea kwenye kushirikiana na watu wengine.
Kwa taratibu hizo, huwa tuna hatua za kuchukua pale mtu anapokwenda tofauti na anavyopaswa kwenda.

Kuna watu ambao wanakuwa wameenda tofauti kabisa na taratibu ambazo tumeweka.
Lakini inapokuja kwenye kuchukua hatua zinazopaswa kuchukuliwa, huruma inatuingia.
Tunawaonea watu hao huruma, na kuona tunalazimika kuwapa nafasi nyingine kwa sababu wataweza kufanya vizuri zaidi.

Kama utakuwa ni mdadisi, utakuwa umejionea wazi ya kwamba wale ambao hukufanya maamuzi juu yao kwa sababu ya huruma, ndiyo pia wamekuwa chanzo kikubwa cha changamoto kwako.
Watu hao ndiyo huwa wanayafanya maisha yako kuwa magumu na usiyoyafurahia.
Kwa kifupi watu ambao uliacha kufanya maamuzi kwa sababu ya kuwaonea huruma, ndiyo huwa wanakosa kabisa huruma kwako.

Kumbuka wateja ambao ulivunja utaratibu uliojiwekea kwenye biashara kwa sababu unawaonea huruma, ndiyo hao hao wanaishia kukutesa sana kwenye yale wanayofanya.
Huenda uliwapunguzia bei au hata kuwapa bure kwa huruma uliyokuwa nayo kwao.
Lakini baada ya wao kupata ulichowapa, wanaona wanastahili zaidi hivyo kuanza kukusumbua.
Hapo ndipo wanapokupa mateso makubwa sana ambayo hukuyategemea.

Kadhalika kwa wafanyakazi unaokuwa umewaajiri au watu wengine unaoshirikiana nao, wale ambao hawakidhi vigezo ila ukawaacha kwa sababu ya huruma ndiyo huja kukupa mateso makubwa.
Watu hao ambao wewe uliwaonea huruma, wao wanakosa huruma kabisa.

Unakuwa umewaonea huruma kwamba ukiwaacha hawana pa kwenda.
Lakini wao wanapopata upenyo kidogo tu, huwa wanautumia kikamilifu kuchukua hatua ambazo wewe ulipaswa kuchukua ila ukaingiwa na huruma.

Kwa kifupi, wale unaowaonea huruma ndiyo huwa wanakuwa katili sana kwako.
Ulitegemea wangekuwa wa kwanza kurudisha huruma uliyoonyesha kwao, lakini wanaishia kufanya ukatili ambao unakuumiza sana.
Japo wapo wanaokuwa wanafanya bila kujua, wengi wanakuwa wanajua kabisa kile wanachofanya.
Wanakuwa wanalipa chuki iliyojengeka kwako kwa sababu ya ile huruma unayokuwa umewapa.
Watu huwa hawapendi kujiona hawana nguvu dhidi ya wengine.
Watatumia hata kuwapa wengine hali ya hatia ili tu nao wajione wapo juu.
Na ndiyo maana wale unaokuwa umefanya maamuzi kwa huruma, ndiyo huja kufanya maamuzi yanayokuumiza sana.

Kitu kikubwa cha kuondoka nacho hapa ni kuhakikisha unafuata utaratibu uliojiwekea kwenye kila eneo la maisha yako.
Pale anapopatikana mtu ambaye hajafikia taratibu zilizopo, kamwe usimchague kwa sababu ya huruma.
Badala yake endelea kuwafikia wale watakaokuwa wanakidhi vigezo ulivyoviweka.

Watu sahihi wapo wengi sana.
Kama hujawapata siyo kwa sababu hawapo.
Bali ni kwa sababu hujatafuta vya kutosha.
Unapojaza nafasi na watu ambao hawakidhi vigezo, unajisahau kwenye kutafuta walio sahihi.
Na hao wasio sahihi siyo kwamba watatumia fursa uliyowapa kuhakikisha wanakidhi vigezo.
Badala yake wanakuwa wanatafuta fursa ya wao kukuumiza pia.

Unaweza kuona hayo yote hayajakaa sawa, lakini ndivyo dunia ilivyo, haipo ndani ya uwezo wako kupanga dunia iendeje.
Wewe jiwekee mchakato wako na ufuate mchakato huo mara zote bila kuacha kwa sababu za kihisia.
Maana mara zote pale hisia zinapokuwa juu, fikra huwa zinakuwa chini kabisa na maamuzi yanayofanyika yanakuwa siyo sahihi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe