3176; Kuza mauzo kwa macho na masikio.

Rafiki yangu mpendwa,
Mauzo ndiyo moyo wa biashara.
Matatizo mengi ya biashara huwa yanaanzia kwenye mauzo.
Pale mauzo yanapokuwa chini, changamoto nyingi hujitokeza kwenye biashara.

Kwa maana hiyo basi, mahali pa kuanzia kutatua changamoto nyingi za kibiashara ni kukuza mauzo.
Zipo njia nyingi za kukuza mauzo kama ambavyo tumekuwa tunajifunza kwenye programu ya CHUO CHA MAUZO.
Lakini msingi mkuu wa njia hizo zote ni matumizi sahihi ya viungo viwili vya mwili wako; macho na masikio.

Ukitumia kwa usahihi macho na masikio yako, utaweza kufanya mauzo makubwa kwenye biashara yako.
Unafanya hivyo kupitia majukumu makubwa mawili;
1. Kuziangalia namba zako.
2. Kuwasikiliza wateja wako.
Hakuna tatizo la mauzo ambalo haliwezi kutatuliwa kwa njia hizo mbili.

Angalia namba zako.
Ukweli mkubwa unaoweza kupata kuhusu mwenendo wako wa mauzo ni kwa kuziangalia namba zako za mauzo.
Namba hizo ndiyo kile kinachofanyika kwa mauzo.
Matokeo unayokuwa unayapata kwenye mauzo, yanatokana na jinsi unavyofanyia kazi namba zako.
Namba za mauzo zipo nyingi, lakini za msingi kuangalia kila wakati ni hizi sita;
1. Wateja tarajiwa wangapi unaowatengeneza.
2. Wateja tarajiwa wangapi unaowageuza kuwa kamili.
3. Wateja kamili wangapi wanaorudi tena kununua.
4. Mauzo kiasi gani wateja wanafanya kila wanapokuja kwenye biashara.
5. Faida kiasi gani inayopatikana.
6. Juhudi zinazofanyika kuwafikia wateja, kwa kuwapigia simu na/au kuwatembelea.

Ukiziangalia hizo namba kwa umakini mkubwa, utaweza kupima mwenendo wa mauzo na kuona wapi pa kuboresha ili kuuza zaidi.
Kwa kukuza hizo namba, mauzo yataweza kuwa makubwa zaidi na faida nzuri kutengenezwa.

Sikiliza wateja wako.
Ni rahisi kudhani unajua kile wateja wanataka na hivyo kutumia nguvu kubwa kuwalazimisha wachukue kile unachowauzia.
Lakini kama hawakinunui kwa ukubwa uliodhani watafanya hivyo, hebu wasikilize kwanza.
Huenda kuna namna tofauti wanataka ambayo wewe hujaweza kuwapa.
Huenda kuna vitu wanapata kwingine ila kwako hawapati.
Na huenda kuna namna wanaona thamani wanayopata kwako ni ndogo kuliko bei wanayopaswa kulipa.

Kwa bahati mbaya sana huwezi kuwasikiliza wateja kwa yale wanayokuambia.
Kwa sababu mengi wanayokuambia siyo ukweli. Hasa pale unapowataka wanunue na wakakupa majibu yao pendwa kama nitakutafuta nikiwa tayari.
Hapo wanakuwa wanakukwepa tu.
Ukiondoka na hayo na kudhani umejifunza, hujajifunza chochote.

Unawasikiliza wateja wako kupitia kuwauliza maswali mahususi kuhusu maumivu waliyonayo na kule wanakotaka kufika. Kisha unasikiliza kwa makini nini wanasema na pia nini hawasemi.
Wasikilize wanavyoyaelezea maumivu yao, utajifunza mengi kwa mtazamo wao.
Pia sikiliza wanavyoeleza kule wanakotaka kufika, utaona jinsi ya kuwasaidia kufika.

Unapaswa pia kuwasikiliza wateja kwa kutumia macho yako.
Kuangalia tofauti ya kile wanachosema na wanachofanya.
Maana wanachosema ni kufurahisha, wanachofanya ndiyo ukweli.
Kwa kuangalia jinsi wateja wanavyotumia fedha zao, unapata ukweli mkubwa kuhusu wao.
Wanaweza kukudanganya kwa maneno mengi, lakini kura ya kweli wanapiga kwa matumizi ya fedha zao.
Ukiweza kuona jinsi ambavyo wateja wanatumia fedha zao, utajua ukweli mkubwa kuwahusu wao.

Kuza mauzo yako kwa kutumia macho na masikio yako.
Kwa kuziangalia namba zako za biashara mara zote.
Na kuwasikiliza kwa makini wateja wako mara zote.

Kwa bahati mbaya sana, wauzaji wengi wamekuwa wanahangaika na mambo mengi, ila wanayapuuza haya mawili ambayo yangeweza kuleta mapinduzi makubwa kwao.
Wewe usiwe kama hao wengi ambao wanahangaika sana ila hawakuzi mauzo.
Weka macho kwenye namba na masikio kwa wateja na utaziona fursa za kuweza kuuza zaidi.

Na kwa yote unayojifunza kwa kuangalia na kusikiliza, anza kuchukua hatua mara moja.
Nenda ukiboresha mchakato wako wa mauzo ili kila wakati uwe unafanya mauzo makubwa zaidi kuliko ulivyokuwa unafanya kipindi cha nyuma.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe