3178; Sijali, Naweka Kazi.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye michezo, hasa mpira wa miguu, mashindano ambayo yanafanyika kwa njia ya ligi, timu inaweza kuwa imeshashinda kwa pointi ambazo imejikusanyia kabla hata ya ligi kuisha.
Lakini lazima timu hiyo ikamilishe michezo yote iliyobaki kwenye mzunguko wa ligi.
Ushindi unaweza kuwa umeshapatikana kabisa, lakini lazima muda usubiriwe, wa michezo yote kukamilika.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye ushindi wa maisha ya mafanikio.
Ushindi wa mafanikio siyo wa kusubiri mpaka kufikia kilele.
Bali ni ushindi unaopatikana kwa maamuzi ambayo mtu unafanya kisha kusubiri muda ili ushindi huo ujidhihirishe.

Yaani safari ya mafanikio ni sawa na ligi ambayo unaanza kwa kupewa ushindi, halafu kazi yako kuu inakuwa kulinda ushindi huo usipotee.
Hivyo unalazimika kuweka juhudi kubwa mara zote ili kulinda usipoteze.
Ni sawa na kuogelea, ukisimama unazama.
Hivyo lazima uendelee kupiga mbizi, iwe unataka au hutaki, unajisikia au hujisikii.

Ili usipoteze ushindi ambayo unakuwa umeanza nao, unapaswa kwenda na mtazamo wa; SIJALI, NAWEKA KAZI.
Umeshajua nini unataka na umeshajua unapaswa kufanya nini ili kukipata.
Hivyo kinachobaki ni wewe kuweka kazi ili ukipate.
Ukishaweza kufikia hatua ya hujali bali unaweka kazi, ushindi ni uhakika kwako.

Unajisikia kuchoka sana? Usijali, weka kazi.
Watu hawakuelewi? Usijali, weka kazi.
Unakutana na magumu na changamoto? Usijali, weka kazi.
Matokeo yanachelewa? Usijali, weka kazi.
Ukiweza kufikia ngazi hii ambayo kuweka kwako kazi hakuathiriwi na chochote kile, ushindi ni wa uhakika kwako.
Hata kama unaanzia chini kabisa na huna chochote.

Ndiyo maana nakuambia umeshashinda, unachosubiri ni muda tu upewe kombe.
Lakini pia muda huo hauna mwisho.
Maana zoezi la kutojali na kuweka kazi ni endelevu.
Ukiacha tu, umepoteza kila kitu.

Siku Elon Musk anatangazwa na jarida la Forbes kama mtu tajiri zaidi duniani, hakuwa na mengi ya kusema.
Kupitia mtandao wa twitter (sasa X) aliandika; “How strange. Well, back to work…”
Akimaanisha; “Inashangaza. Sawa, narudi kazini.”

Kwa watu wa kawaida kufikia nafasi hiyo ingekuwa ndiyo ushindi mkubwa kwao na hata kuacha kujitesa.
Lakini kwa Elon, ushindi ulishaanza kabla ya hayo matokeo.
Na ushindi huo unaendelea baada ya hayo matokeo.
Ni ushindi wa SIJALI, NAWEKA KAZI.

Ni watu wachache sana wanaoweza kwenda vizuri na dhana ya SIJALI, NAWEKA KAZI.
Inamtaka mtu kujitoa kweli kweli kupata kile anachotaka.
Ndiyo kinachowatofautisha wanaopata ushindi mkubwa na wanaobaki kawaida.

Dunia haitakuangusha kamwe kama utakuwa tayari kuweka kazi mara zote.
Hakuna kazi inayopotea bure bila kulipwa.
Na kikubwa sana wanachokosa watu kwenye kazi ni msimamo na subira.
Maana kila mtu anaweza kuweka juhudi kubwa.
Ila wanaoshinda ni wale wanaoweza kuweka juhudi hizo kwa muda mrefu bila kuacha, hata wakutane na nini.
Wakipoteza wanaendelea kuweka juhudi.
Na hata wakishinda wanaendelea na juhudi.

Wasiofanikiwa huwa wanayumbishwa sana na matokeo wanayopata.
Wakipata matokeo mabaya wanaona hawawezi tena, hivyo wanakata tamaa na kuacha kuendelea kuweka kazi.
Na hata wakipata matokeo mazuri, wanayasherekea sana na kujiona wameshamaliza, hawahitaji tena kuweka kazi.
Na hivyo ndivyo wanavyoshindwa vibaya sana.

Sisi ushindi wetu ni wa uhakika kwa sababu tumechagua kuendelea kuweka kazi bila kuacha, haijalishi ni matokeo ya aina gani tumepata.
Tukipata matokeo mabaya, tunaendelea kuweka kazi.
Na hata tukipata matokeo mazuri, tunaendelea kuweka kazi.
HATUJALI, TUNAWEKA KAZI na ndiyo maana tunao uhakika wa ushindi.

Kwenye hii safari, kushindwa ni pale unapoacha kufanya.
Hivyo ni mwiko kwetu kuacha kuweka kazi, hata iweje.
Tunajua muda utatupa chochote tunachotaka, kama tutaendelea kuweka kazi.
HATUJALI, TUNAWEKA KAZI huku tukiwa na subira isiyochoka.
Ushindi tunao, hatutakubali kuupoteza kwa namna yoyote ile.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe