Mpendwa mstoa mwenzangu,
Tunaishi katika zama za kelele. Na ni ngumu katika zama hizi mtu kuonekana kuwa mpweke, kukaa bila kuwa na kitu cha kufanya.
Zama hizi mtu anayekaa kimya bila kupiga kelele kwenye mitandao ya kijamii au kuchangia kwenye hoja mbalimbali anaonekana kama vile amepitwa na wakati.
Kwa lugha rahisi, hizi ni zama ambazo watu wanaogopa sana upweke. Ndiyo maana mtu hawezi kukaa bila kuwa na kitu cha kufanya. Pata picha ukikutana na mtu haiwezi kupita dakika 15 hajashika simu yake.
Watu wanaogopa sana kuwa katika hali ya upweke.
Aliyekuwa mwanahisabati, mwanafalsa na mwandishi Blaise Pascal mwaka 1654 aliwahi kunukuliwa akisema,
Matatizo yote ya binadamu chanzo chake ni mtu kushindwa kukaa peke yake kwenye chumba bila ya kuwa na kitu cha kufanya.
Mwaka 2019 novemba 22, Kocha Dr Makirita Amani aliandika kwenye Amka Mtanzania “Mwaka 2014 kulifanyika utafiti ambapo watu walipewa jukumu moja tu, kukaa kwenye chumba peke yao na kufikiri. Chumba hicho hakikuwa na kitu chochote kile, bali nyaya za umeme ambazo mtu akizishika anapigwa shoti na kuumia.
Kabla ya kuingia kwenye chumba hicho, watu waliulizwa kama wapo tayari kushika nyaya hizo za umeme na kupigwa shoti, wote walisema hawapo tayari kuzishika. Hivyo waliwekwa kwenye chumba hicho na kuachwa, kwa dakika 15 mpaka 25 bila ya kitu cha kufanya, bali kufikiri tu.
Baada ya kuachwa kwenye chumba hicho kwa muda, asilimia 67 ya wanaume na asilimia 25 ya wanawake walizishika nyaya za umeme na kupigwa shoti. Tena wengine walifanya hivyo zaidi ya mara moja. Waendeshaji wa utafiti huu walijumuisha kwamba, watu huwa hawapo tayari kukaa bila ya kuwa na kitu cha kufanya, watafanya hata kitu kinachowadhuru lakini siyo kukaa kwa upweke.”
Watu wengi waliofanya makubwa duniani na hata ambao wanaoendelea kufanya makubwa ni wale ambao wanapata muda wa utulivu na kuwa peke yao kwenye upweke.
Sina uhakika kama itakufaa lakini yako matatizo mengine ya watu siku hizi ni kutaka kuongea na kuchangia kwenye kila kitu na hili tunaliona zama hizi baada ya uwepo wa simu janja na intaneti.
Mtu asipochangia kwenye kitu, ataonekana kama ameshindwa hiki kinawafanya watu wachangie kwenye kila jambo. Kwenye falsafa, siyo dhambi kukaa kimywa na unapaswa kuongea pale ambapo ni muhimu tu kuongea.
Mwanafalsa Epictetus anatuambia, kwa sehemu kubwa kuwa mkimya, na sema kile ambacho ni muhimu na kinachotakiwa kwa maneno machache.
Siyo ujinga kukaa kimya na ukimya wa mtu muda mwingine huonekana ni hekima hata kama mtu huyo ni mpumbavu.
Unapokuwa mahali kwenye kikao au mazungumzo yoyote yale, usiwe mwongeaji sana wa kutaka kuchangia kwenye kila kitu. Badala yake kuwa msikilizaji na pale inapobidi kuchangia changia kwa ufupi na usiwe na maneno mengi bali nenda moja kwa moja kwenye hoja husika.
Ni mara ngapi tunaenda sehemu tunataka tutawale mazungumzo? Badala ya kutaka kuwa wasikilizaji ?
Matatizo mengi yanayotokea chanzo chake ni kuongea sana. Pata picha ulishawahi kumuona bubu anagombana na mtu kwa sababu ya kuongea?
Unaibua matatizo mengi kwa sababu ya kuongea sana. Hata katika mahusiano, changamoto nyingi zinaanzia pale mmoja anapokuwa anaongea sana.
Ukiwa mkinya utapunguza matatizo mengi kwa wale ambao mnahusiana kwenye mahusiano yako kuliko kuwa mwongeaji sana.
Na kuongea siyo tu ana kwa ana bali pia hata kwa njia ya mitandao ya kijamii.
Sehemu kubwa ya mazungumzo yetu Epictetus anasema tuwe kimya. Kuwa kimya ni kitu ambacho watu wengi hawawezi kwenye zama hizi. Kukaa kimya bila kuongea.
Kwenye zama hizi, ukimya una faida nyingi. Unaweza kutumia ukimya na kuokoa nguvu nyingi na kuzitumia nguvu hizo katika uzalishaji, kujitathimini na kufanya tahajudi.
Usione aibu kukaa kimya na kutokuchangia kwenye kitu. Na hata kama huna maoni usiogope kusema huna maoni kuliko kutaka kuchangia tu.
Ukilazimisha kuongea, utakuja kuongea ambavyo havitakiwi na kusababisha matatizo kwa watu wengine.
Punguza matatizo kwa kuwa mkimya na ongeza matatizo kwa kuwa muongeaji sana.
Hatua ya kuchukua; kama huna cha kuchangia kaa kimya na ikitokea unataka kuongea, sema kile kinachohitajika kwa maneno machache tu.
Ukimya ni nyumba nzuri kuishi katika zama hizi za kelele. Kila mmoja wetu aishi kwenye kwenye nyumba ya ukimya na kuepukana na kelele za dunia.
Acha ukimya kuwa kanuni yako kuu na ongea kile ambacho ni muhimu tu na kwa maneno machache.
Let silence be your general rule; or say only what is necessary and in few words. Epictetus
Zeno anasema, ni bora kutembea na miguu kuliko ulimi.
Akiwa na maana kwamba ni bora mtu anayetembea kuliko anayeongea.
Better to trip with the feet than the tongue.”
—Zeno
Seneca anasema ukimya ni somo ambalo mtu hujifunza kutoka kwenye magumu ya maisha aliyopitia.
Nukuu;
“Silence is a lesson learned through life’s many sufferings”
—Seneca
Marcus Aurelius anatuambia kuwa, jikumbushe kwamba kazi yako ni kuwa binadamu mwema; jikumbushe wewe mwenyewe kwamba asili inahitaji watu. Kisha fanya hivyo, bila kusita na ongea ukweli kama ulivyo. Lakini kwa ukarimu. Unyenyekevu. Bila unafiki.
Nukuu;
Remind yourself that your task is to be a good human being; remind yourself what nature demands of people. Then do it, without hesitation, and speak the truth as you see it. But with kindness. With humility. Without hypocrisy.”
—Marcus Aurelius
Kitu kikubwa cha kuondoka nacho hapa ni pata utulivu kwenye maisha yako na usiwe mwongeaji sana bali kuwa msikilizaji.
Kumbuka, matatizo mengi yanaanzia kwa kuongea hivyo jifunze kunyamaza na utakua salama.
Rafiki na mstoa mwenzako,
Mwl Deogratius Kessy
Matatizo makubwa kwenye zama hizi yanatokana na watu kuongea sana kuliko kukaa kimya. Ni vyema kupata utulivu kwenye maisha na kuepuka kuongea sana na badala yake kuwa msikilizaji.
LikeLike
Asante sana Mwl Deo,
Nimejifunza asili inahitaji watu. Bila kusita ninapaswa kuwa binadamu mwema, kuongea ukweli kama ulivyo, kwa ukarimu, kwa unyenyekevu na bila unafiki.
LikeLike
Ni kweli matatizo mengi yanatokana Na kuongea sana nitakuwa mkimya
LikeLike
Tutaepuka kuingia kwenye matatizo na makwaluzano na wengine ikiwa tutaacha ukimya kuwa kanuni yetu kuu na kuongea kile ambacho ni muhimu tu na kwa maneno machache.
Asante sana Mwl.Deo
LikeLike