3186; Mrejesho wa watu.

Rafiki yangu mpendwa,
Sisi binadamu kama viumbe wa kijamii, huwa tunapenda sana kuwa ndani ya kundi la watu.
Ili kujihakikishia nafasi yetu kwenye kundi lolote tulilopo, huwa tunajali sana kuhusu mrejesho wa watu wengine kuhusu sisi.

Huwa tunataka sana kukubalika na kila mtu, tukiamini ndiyo njia salama ya kuwa ndani ya kundi lolote lipo.
Lakini kile tunachotaka sana kutoka kwenye makundi tuliyopo, siyo tunachohitaji kwa ajili ya mafanikio makubwa tunayoyataka.

Kama kila mtu anaamini kwenye ndoto kubwa ulizonazo kwenye maisha yako, basi ndoto hizo siyo kubwa vya kutosha.
Ni ndoto za kawaida kabisa ambazo zipo kwenye fikra za kawaida za kila mtu.
Ndoto kubwa sahihi kwako ni zile ambazo wengine wakisikia unazo wanakucheka na kukuambia unajidanganya, kwani haiwezekani kabisa.
Ndoto kubwa sahihi kwako ni zile ambazo wengi hawawezi kabisa kuzielewa. Hizo ndiyo ukizifanyia kazi zinazalisha matokeo makubwa na ya tofauti.

Kama kila mtu anakupenda na kukukubali, kuna mahali unakosea.
Na kwa sehemu kubwa unakuwa huna viwango ulivyojiwekea ambavyo unavisimamia.
Hivyo watu wanakuona wewe ni mtu poa, lakini mwisho wa siku hakuna hatua kubwa unazopiga kwenye maisha yako.
Kukubaliana au kutaka kukubalika na kila mtu ni njia ya uhakika ya kushindwa kwenye maisha.
Ili ufanikiwe ni lazima uwe na viwango vya juu ambavyo unavisimamia.
Katika kusimamia viwango hivyo kuna watu utakaowaudhi, kwa kuwakatalia vitu walivyotaka.
Na hapo watu hao watakuchukia sana.
Lakini pia watakuwepo ambao watakupenda kwa viwango hivyo ulivyojiwekea.

Kama kwenye kufanya kwako masoko na mauzo hakuna watu wanaokulalamikia kwamba unawafuatilia sana au unawapigia sana kelele, basi jua hujapiga kelele za kutosha.
Unatakiwa uendelee kuwafikia wengi zaidi na kwa ukubwa na wingi zaidi. Unapaswa kuwafikia watu mara kwa mara kiasi cha baadhi yao kuona hilo ni kero kwao.
Ni kupitia malalamiko hayo ya wengine ndiyo utaboresha zaidi hatua hizo unazochukua.

Kama hakuna watu wanaokuona una roho mbaya na hujali, unahangaika sana na mambo ya wengine kuliko mambo yako binafsi.
Utawafurahisha wengi kwa kuhangaika na mambo yao, lakini hilo litakuwa kikwazo kwako kukamilisha yako kwa sababu huyapi muda wa kutosha.
Unapaswa kuweka kipaumbele cha kwanza na pekee kwenye mambo yako na kupuuza mengi ya wengine.
Umakini wako una ukomo, upeleke kwenye mambo yako na siyo mambo ya wengine.

Kama hakuna watu wanaoamini unatumia nguvu fulani zisizo sahihi kwenye mambo yako, basi hakuna makubwa unayofanya.
Kwenye biashara uliyopo, utajua kama kweli unaufanyia kazi mchakato sahihi kama washindani wako watakuwa wanakusema vibaya kwamba unatumia nguvu za ushirikina kuteka wateja.
Kwenye maisha ya kawaida, utajua kama kweli unauishi mchakato kama kuna watu wanasema wewe ni ‘freemason’. Waseme umepewa masharti makali ambayo huwa unayafuata bila kuvunja.

Hii ni baadhi ya mirejesho kutoka kwa wengine ambayo ndani yake inakuwa na somo la tofauti na tunavyodhani.
Tuendelee kukusanya hii mirejesho kutoka kwa wengine na kufanya maboresho sahihi ili kuhakikisha tunapata matokeo makubwa tunayoyataka.

Kanuni ya uhakika ya kuweza kufanya makubwa kwenye maisha yako ni kwenda kinyume na kundi kubwa la watu.
Hiyo ni kwa sababu mara nyingi kundi kubwa la watu huwa lipo kwenye njia ya kupotea.
Ukiweza kusimama imara dhidi ya kundi hilo kubwa, hakuna namna utashindwa kupata matokeo makubwa unayoyataka.

Kuwa na ndoto kubwa, ambazo ndiyo zinakuwa kipaumbele pekee kwako na kuwa na mchakato wa uhakika unaoufuata kwenye kuzipambania.
Simama kwenye kile kilicho sahihi bila kujali kundi kubwa la watu linakuchukuliaje.
Hiyo ndiyo namna pekee ya kupata mafanikio makubwa unayoyataka kwenye maisha yako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe