Mpendwa mstoa mwenzangu,
Maandiko ya kiimani yanasema kwamba, huwezi kumpenda Mungu usiyemwona kama huwezi kumpenda jirani yako.
Mafundisho mengi yanatufundisha sisi kuwapenda wengine. Ndiyo maana hata mtu akipata fedha, anaanza kuwalipa watu wengine kwanza na kujisahau yeye mwenyewe.
Watu wengi hatujafundishwa kujipenda sisi wenyewe kwanza. Na matatizo mengi kwenye maisha yetu yanaanzia pale tunaposhindwa kujipenda sisi wenyewe.
Kwa mfano, enzi wewe unakua ulikuwa unakatazwa kutumia baadhi ya vyombo. Nyumbani kulikuwa na vyombo vingi kabatini lakini ulikuwa unaambiwa hivyo viache ni vya wageni.
Mpako hapo unapata picha kwamba, tumelelewa katika tamaduni za kuwaangalia wengine zaidi kuliko kujiangalia sisi wenyewe.
Mpaka tunakua tunaamini kwamba vyombo vizuri ni kwa ajili ya wageni na sisi tunatumia vile vya kawaida.
Tumekuwa hatujithamini sisi wenyewe kwanza, bali tunawathanini wengine na sisi kuwa chaguo la pili.
Mwanafalsa na aliyekuwa mtawala wa Roma mwanafalsa Marcus Aurelius aliwahi kunukuliwa akisema,
Jipende wewe mwenyewe kwanza. Ndiyo kitu pekee ambacho unaweza ukajipa kwenye maisha yako.
Nukuu;
Commit to loving yourself completely. It’s the most radical thing you will do in your lifetime.
Zawadi pekee ambayo unaweza ukajipa kwenye maisha yako, ni kujipenda wewe mwenyewe. Hakuna zawadi nyingine. Hakuna mtu atakayeweza kukupenda zaidi ya wewe mwenyewe.
Kutokujipenda ni sawa na mfanyabiashara au muuzaji ambaye haijui biashara yake. Kuna raha pale ambapo muuzaji anapoijua biashara yake na biashara yako ni pale wewe utakavyojipenda.
Unavyojipenda wewe mwenyewe, hata wewe mwenyewe unafurahia. Na ukifurahia ndiyo unakuwa unafanya majukumu yako vizuri.
Kazi unayoifanya ikusaidie kupata mahitaji ya msingi yatakayokuwezesha wewe kujipenda na kupata mahitaji yako ya msingi.
Kocha Dr Makirita Amani, huwa anasema kwamba, upendo unaanza na kujipenda wewe mwenyewe.
Kisha kuwapenda wengine.
Na tatu, kupenda kile unachofanya.
Mapinduzi makubwa kwenye maisha yanaanza na watu kwanza kujipenda wao wenyewe. Mtu akishajipenda yeye mwenyewe, lazima atawaambukiza watu wengine moto wa upendo.
Mtu ambaye anajipenda anasimamia kile alichoahidi. Anafanya kile anachopaswa kufanya.
Anakuwa mtu wa kuaminika.
Anakuwa mtu ambaye hana chuki wala wivu na mtu.
Kama mtu unajipenda, lazima utapambana ili uwe na maisha mazuri, utawapenda wengine na utapenda kile unachofanya.
Kuishi maisha mazuri ni kujipenda wewe mwenyewe kwanza. Kuwa na maisha mazuri halafu hujipendi inakuwa haina maana. Thamani yako inaanza na kujipenda wewe mwenyewe. Usipojipenda wewe mwenyewe watu watakupuuza kama vile muuzaji ambaye haijui biashara yake wateja wanavyompuuza.
Faida ya kujipenda wewe mwenyewe ni nyingi kuliko maelezo. Jipende wewe mwenyewe ndiyo zawadi ambayo unaweza kujipatia.
Rafiki na mstoa mwenzako,
Mwl.Deogratius Kessy
Asante sana Mwalimu Kessy upendo wa kweli unaanzia kwakujipenda wewe binafsi kisha kuwapenda wengine
LikeLike
Asante Mwl Deo,
Ukijipenda wewe kwanza, jamii itakupenda na kukuheshimu.
LikeLike