3195; Kuwa mchezaji hatari kwenye mashindano.

Rafiki yangu mpendwa,
Kama tukiyachukulia maisha kama mchezo na wewe kama mchezaji, unaweza kuwa mchezaji hatari sana kwenye hayo mashindano.
Utakuwa na hatari pale unapokuwa unaanzia chini kabisa na huna chochote cha kupoteza.

Kwenye mashindano ya aina yoyote ile ni wachezaji wanaoanzia chini kabisa na hawana cha kupoteza ndiyo huwa wanaleta matokeo ya kushangaza.

Mtu ambaye tayari yupo chini, hana hofu ya kuanguka, kwa sababu hana pangine pa kwenda isipokuwa juu.
Kwa kuwa anaanzia chini kabisa, uelekeo pekee anaokuwa nao ni wa kwenda juu.

Mtu huyo anakuwa hana chochote cha kulinda na hivyo umakini wake wote unakuwa kwenye kitu kimoja tu, kwenda juu.
Hiyo ndiyo inawafanya wawe washindani hatari na wenye nyenzo kubwa ya kupata ushindi.

Hofu ya kushindwa au kuanguka ni kikwazo kikubwa sana kwa walio wengi kupiga hatua kwenye maisha yao.
Kugawa umakini wako kati ya kushinda na kuepuka kushindwa kunafanya umakini huo kupungua.
Ni pale umakini wako wote unapokuwa kwenye kitu kimoja ndiyo unakuwa na nguvu ya kuleta matokeo makubwa.
Kama ambavyo jua likitawanyika linamulika, lakini likikusanywa mahali pamoja linachoma moto.

Steve Jobs alikuwa na kauli yake; baki na njaa, bali mjinga (stay hungry, stay foolish). Nadhani unajua jinsi ukiwa na njaa unavyohangaika ili kupata chakula, mbele ya njaa hakuna hofu wala aibu yoyote, utafanya kila uwezalo ili tu uweze kupata chakula.
Lakini ukishashiba, unapunguza makali, unaanza kuwa na ustaarabu mwingi ambao unapelekea ukose yale unayotaka.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye safari yoyote ya mafanikio makubwa.
Mtu anapoanzia chini kabisa anakuwa ni mwenye njaa kali hivyo anapambana hasa kupata shibe, hasikilizi wala kuhofia kingine chochote. Na hilo ndilo linamfanya awe mshindani hatari na anayepata matokeo makubwa na ya tofauti.

Ni pale mtu anapoanza kupanda ngazi za mafanikio ndiyo njaa yake ya mafanikio inapungua na hivyo kasi yake ya ukuaji kupungua kitu kinachopunguza hatari yake.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye kujifunza, wengi wanaoanzia chini kabisa wanakuwa tayari kujifunza mengi ili kutoka kwenye hali hizo.
Ni pale wanapoanza kupiga hatua ndiyo wanaona hawahitaji tena kujifunza kwani wameshajua kila kitu.
Na hilo linapunguza makali ya ukuaji wao, kitu kinachofanya wapate matokeo ya kawaida.

Unapokuwa unaanzia sifuri kabisa, huo msukumo mkubwa tayari unakuwa ndani yako, ni wewe tu uufanyie kazi kwa ukubwa bila kujizuia.
Lakini unapoanza kupiga hatua ndiyo unahitaji kujilazimisha kubaki chini kifikra ili ule msukumo mkubwa unaokuwa nao usiondoke.
Uendelee kupata msukumo ambao unakupeleka kwenye matokeo makubwa kuliko ambavyo umewahi kupata.

Hata kama umeshiba, jione bado una njaa na tafuta chakula zaidi bila ya kujali wengine wanasema nini juu yako.
Hata kama tayari vitu unavijua, jichukulie hujui kitu na jifunze tena. Kama kuna kitabu umeshasoma chukulia hujakisoma na kisome tena. Kwa kufanya hivyo kuna mengi utakayojifunza ambayo hukuyapata ukiposoma kitabu hicho kwa mara ya kwanza.

Ukiweza kubaki na mtazamo huo wa chini na wa kupambana mara zote bila kuwa na hali ya kuridhika na kulinda ambayo umeshayapata, hakuna kinachoweza kukuzuia kupanda ngazi za juu zaidi ya pale ulipo sasa.

Acha kulinda hapo ulipo sasa, hilo linakushikilia usipige hatua.
Acha kuhalalisha hapo ulipo sasa, bado ni chini sana ukilinganisha na unakopaswa kuwa.
Mara zote kuwa na njaa kali ya kutaka mafanikio makubwa zaidi na kuwa mjinga wa kujifunza na kuchukua hatua.

Nguvu kubwa ya kupata mafanikio yoyote makubwa unayoyataka tayari ipo ndani yako.
Unachohitaji ni kuiamsha na kuitumia.
Hali unazokuwa nazo zinaweza kuamsha uwezo huo kwa kiasi.
Lakini unapouamsha makusudi, utaweza kuutumia kufanya makubwa zaidi.

Baki na njaa na baki mjinga maisha yako yote, utakuwa mchezaji hatari sana kwenye haya mashindano ya maisha.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe