Habari njema mstoa mwenzangu,

Huwa tunahofia sana vitu vya mbele yetu. Kabla hata hatujalifikia jambo, tayari tumeshajipa presha juu ya kitu hicho kitakuwaje.

Kufikiria mambo yajayo kabla hata hatujalifikia huwa linatukosesha kuishi katika hali yetu ya uwepo wa hali ya sasa.

Tunafikiria yajayo na tunaacha kuishi leo na matokeo yake tunapoteza yote.

Ili kesho iwe nzuri, unapaswa kuwa na leo nzuri. Mtu ambaye anaishi vizuri leo, huwa hahofii sijui kesho itakuwaje.

Kama vile mtu anayehofikia kifo, ni mtu ambaye haishi vizuri kila siku kwenye mchakato wa kufurahia maisha yake. Kumbe basi, badala ya kufikiria kifo, unapaswa kuishi vizuri leo.

Siyo vibaya kufikiria yajayo lakini yanawafanya watu kushindwa kuishi sasa na kupoteza tumaini la kufika mbali.

Wengi wanachoka mapema kwa sababu wanafikiria matokeo kwanza kabla ya mchakato. Watu wanafikiria kulivuka daraja badala ya kuendelea na safari na pale atakapolivuka daraja basi daraja atalivuka.

Jambo la wakati ujao huna udhibiti nao. Udhibiti wako mkuu ni kuishi mchakato wa kufikia wakati ujao vizuri leo. Kwa mfano, mtu anaweza kufikiria lengo la UBILIONEA ni kubwa sana, badala ya kufanya kazi na kuligawa lengo hilo katika hatua ndogo ndogo, yeye anafikiria kuwa Bilionea kwa wakati mmoja.

Badala ya kufikiria safari, anza kusafiri kule unakoenda. Kwa mfano, unapotaka kwenda kazini kwako hufikiri sijui utafikaje, bali unaanza kutoka chumbani na unaanza hatua moja na mwisho wake unafika kazini.

Ukifikiria utafikaje kazini, huwezi kufika lakini ukianza kutoka utafika kazi kwako vizuri.

Utalivuka daraja pale utakapolikuta lifikia ni dhana ya kifalsafa ambayo mwanafalsa Marcus Aurelius anatushirikisha katika makala yetu ya leo.

Marcus Aurelius anasema, usiruhusu wakati ujao kukusumbua. Utakutana nao pale itakapobidi, ukiwa na silaha zilezile za akili ambazo leo zinakuwekea silaha dhidi ya leo.

 “Never let the future disturb you. You will meet it, if you have to, with the same weapons of reason which today arm you against the present.” Marcus Aurelius

Usisumbuke utalivukaje daraja, utalifikia pale utakapolikuta.

Tunaposema daraja inaweza kuwa jambo lolote wakati ujao ambalo kwa sasa linakusumbua utalifikiaje.

Kwa mfano, una mtoto wako amemaliza darasa la saba, sasa unafikiria akiwa kidato cha nne atakuwaje.

Mambo yajayo hata yasikusumbue. Wewe pambana na kile ambacho kinawezekana sasa na hayo mengine utayakuta mbele ya safari.

Usifikirie kumla ng’ombe mzima kwa wakati mmoja. Bali anza kumla vipande kidogo kidogo. Ukifikiria utamlaje ng’ombe mzima huenda ukashindwa hata kumla lakini ukienda kwa hatua unafika.

Mkuyu nao ulianza kama mchicha na pale unapoanza kuota wala haukufikiria utakuwaje mkubwa bali ulianza kawaida.

Badala ya kuwaza utalifikia kweli lengo la UBILIONEA, wewe weka juhudi katika mchakato wa kila siku kufikia malengo yako ya UBILIONEA.

Kesho au wakati ujao utakuja kwa namna utakavyokuja au kwa namna ulivyopangwa. Kama vile hujui kifo chako kitakuwaje, ndivyo ilivyo katika mambo yajayo. Ni mambo ambayo yako nje ya uwezo wako kabisa hivyo usikubali yakutoe kwenye njia kuu.

Usifikirie mwaka 2030 utakuwaje? Bali fikiria utawezaje kuishi siku yako ya leo kwa ukamilifu mkubwa.

Kwa mfano, Seneca aliendelea kufurahia maisha yake kama kawaida hata baada ya kuambiwa siku hiyo atauliwa. Wenzake walimshangaa kwamba iweje umeambiwa utauwawa leo halafu unaendelea na maisha yako kama kawaida?

Kufikiria yajayo yanaweza kukukosesha usingizi wa kuishi maisha yako kwa utulivu wakati wa sasa. Badala ya kufurahia ushindi unaopata leo hata kama ni kidogo, wewe unaupuuzia na kufikiria yajayo.

Hatua ya kuchukua leo; usisumbuke na mambo yajayo. Utakutana nayo mbele ya safari.

Usifikirie utalivukaje daraja, bali jiambie utalivuka daraja pale utakapolikuta. Kwa mfano, usifikirie biashara yako itakuwaje, bali anza kufanya biashara.

Usifikirie lini utafikisha milo 250 kwenye uwekezaji wa UTT, bali anza kuchukua hatua kila siku za kuweka ili ufikie lengo lako.
Kumbuka, namba huwa inaanza na sifuri , ili ufikie 10 lazima uanzie chini.

Kinga yako yakutozinguliwa na mambo yajayo ni kuyaachia wakati ukifika utaamua tu. Wakati utasema kila kitu, wewe kaa kwenye mchakato na mchakato wako utaamua yajayo badala ya kusumbuka nayo.

Mstoa mwenzako,
Mwl Deogratius Kessy