3197; Shujaa.

Rafiki yangu mpendwa,
Pata picha una mtu wako wa karibu (anaweza kuwa mzazi, mtoto au mwenza) ambaye yupo kwenye mji tofauti na ulipo wewe.
Unapata taarifa za watabiri wa hali ya hewa kwamba ule mji ambapo mtu wako wa karibu yupo, utakumbwa na mafuriko makubwa siku inayofuata.
Je utachukua hatua gani?

Kwa haraka sana utamtafuta mtu huyo wa karibu kwako na kumpa taarifa hizo ili achukue tahadhari.
Sasa pata tena picha unapiga simu ya mtu wako wa karibu na inaita tu bila kupokelewa, au hata haipatikani kabisa!
Kwa hakika utaanza kupatwa na wasiwasi, kwa kuwa hujui nini kinaendelea upande walipo.
Utaendelea kumtafuta kwa njia nyingine mbalimbali.
Kama simu haijapokelewa, utamtumia ujumbe kwa njia mbalimbali. Utaendelea kumtafuta bila kuchoka mpaka umpate.
Lengo lako likiwa ni kuwapa taarifa ili wachukue tahadhari, kwa sababu maisha yao yapo hatarini.
Hutatulia mpaka pale unapojihakikishia kwamba watu hao wa karibu kwako wapo salama.

Sasa turudi kwenye mauzo, je huwa unamtafuta mteja mara ngapi na kwa njia zipi mbalimbali pale unapomtafuta mara moja na akawa hapatikani?
Kwa wauzaji wengi, wanapomtafuta mteja mara moja na asipatikane au akawajibu vibaya basi wanaachana naye kabisa na kwenda kwa mwingine.
Hilo siyo sahihi.
Kwanza wateja wako ni watu muhimu sana kwako, kwa sababu ndiyo wanayawezesha maisha yako kwenda.
Na pili, wateja wako wapo hatarini kama hawajapata kile unachouza, kwa sababu wataenda kupata kwa wauzaji wengine, kitu kisichokuwa na ubora kama chako na atatozwa gharama kubwa kulilo unavyotoza wewe.

Wewe ni shujaa ambaye wajibu wako namba moja ni kumwokoa mteja wako kutoka kwenye hayari aliyopo.
Na hivyo unapaswa kufanya kila kinachopaswa kufanyika mpaka uweze kumpata na kumpa habari njema na za ukombozi kwake.
Kama umempigia simu na hajapokea, utarudia tena kumpigia simu baada ya muda, pamoja na kumtumia ujumbe mfupi unaomtaka muwasiliane kwa sababu una jambo muhimu.
Kama amekukatia simu mpelekee ujumbe kwamba amefanya makosa makubwa kwani kuna jambo muhimu ulilonalo ambalo anapaswa kulijua.

Kadiri unavyomtafuta mtu kwa wingi na kwa njia mbalimbali, ndivyo unavyojiweka kwenye nafasi nzuri ya kumpata na kukamilisha yale uliyopanga.
Na ni kweli kabisa kwamba unazo taarifa muhimu kwa mteja ambazo unalazimika kuzifikisha kwake kwa sababu yupo hatarini kama hatachukua hatua sahihi.
Kadiri unavyokuwa na imani kwenye hili na kutoa thamani kubwa kwa wateja wako, ndivyo utakavyozidi kuaminika na wateja wako na kufanya mauzo makubwa zaidi.

Maisha ya wateja wako yapo hatarini.
Wewe una taarifa muhimu za kuwafikishia ili wajitahadhari na hatari iliyo mbele yao.
Unajaribu kuwafikia ila inashindikana.
Huo ndiyo wakati wa kuwa shujaa na kufanya kila namna ili kuwafikia wateja wako na kuwafikishia taarifa muhimu ulizonazo.
Usiwaangushe wateja wako hata kama wanaonekana kukuletea ubishi.
Una wajibu mkubwa wa kuhakikisha wapo salama.
Hivyo pambana kwa kila namna ili kutekeleza hilo.

Watu wanakupa uzito na umakini pale unapokuwa king’ang’anizi, wanaona lazima jambo utajalokuwa nalo ni muhimu sana kwao.
Tumia nguvu hiyo ya ung’ang’anizi kuhakikisha unawafikia wateja wako wote kwa uhakika na kuwashawishi kuchukua hatua sahihi kwao.

Kama utashindwa kuwafikia wateja kwa sababu wanakukwepa kwa namna mbalimbali, tatizo siyo hao wateja, bali tatizo ni wewe.
Unakuwa umeshindwa kuonyesha ushujaa ambao tayari upo ndani yako.
Mwishowe unawaangusha wateja wako kwa kuwaacha kwenye hatari ambayo inawagharimu sana.

Hilo halipaswi kuendelea tena tangu sasa,
Chukua hatua kama shujaa mwenye uwezo wa kuyaokoa maisha ya wateja wako.
Timiza wajibu wako wa kishujaa kwa kuhakikisha hakuna chochote kitakachosimama kati yako na mteja wako.

Ukiwa na mtazamo huu kwenye kuwafuatilia wateja wako na kuutekeleza, utaweza kuimarisha sana mahusiano yako na wateja na hata kukuza mauzo.
Yale yote unayoyajua kuhusu biashara yako yana manufaa sana kwa wateja wako.
Ukiweza kuyawasilisha vyema kwao, utatimiza wajibu wako wa kishujaa wa kuhakikisha maisha ya wateja wako yapo salama.

Usiwaangushe wateja wako,
Maisha yao yanakutegemea sana wewe,
Kama shujaa.
Timiza wajibu wako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe