3199; Mauzo ya Kibabe.

Rafiki yangu mpendwa,
Niwe mkweli kwamba huwa napenda sana mambo ya kibabe.
Hasa pale ubabe huo unapomwezesha mtu kuvuka hofu na kuchukua hatua.
Naamini bila ya shaka yoyote kwamba kwenye hii dunia bila ubabe wa aina fulani, huwezi kupata makubwa unayotaka.
Maana kila kitu ni cha kupambania na hakuna nafasi ya walio wanyonge.
Maana hata vitabu vya dini vimeeleza wanyonge hawana nafasi.

Nilikuwa nasoma habari ya mtu mmoja aliyekuwa mwandishi na mhariri kwenye jarida fulani na hakuwa anaingiza kipato kikubwa.
Mtu huyo alienda kwa mmiliki wa jarida hilo akitaka amwongeze mshahara kwa sababu kazi anayofanya ni kubwa na malipo anayopata ni kidogo.
Mmiliki huyo alimsikiliza kwa makini mpaka alipomaliza kujieleza, kisha akamwambia hataweza kumwongezea kipato kwa sababu kazi yake siyo bora kama anavyodhani.

Mtu huyo aliposikia maneno hayo alikasirishwa sana, iweje mmiliki huyo wa jarida amdharau kiasi hicho wakati yeye ni mwandishi na mhariri mzoefu.
Mmiliki huyo wa jarida alimwambia kwa upole; “Sikiliza, sijifanyi najua chochote kuhusu uandishi au uhariri, lakini najua sana kuhusu biashara. Kitu cha kwanza na muhimu kabisa kwenye biashara ni mauzo. Na kila mtu kwenye biashara anatakiwa kutimiza majukumu yake kwa namna ambavyo yatakuza mauzo.”

Mwandishi akamuuliza; “Unamaanisha nini?”
Mmiliki akamjibu; “Wacha nikupe maana rahisi ya uandishi na uhariri bora; ni ule unaoleta mauzo makubwa zaidi. Huwezi kulipwa kiasi kikubwa kama uandishi wako hauchangii mauzo makubwa.”

Mwandishi alitafakari hilo kwa kina na akaona ni sahihi.
Na hapo alifanya maamuzi kwamba ataacha ukiritimba wa kiuandishi na kuangalia jinsi gani kila andiko analoandaa linachangia kwenye kuongeza mauzo.
Mmiliki wa jarida lile alipoona mhariri wake anataka kuongeza kipato zaidi, akawa anazidi kumjenga kimauzo.
Mara kwa mara alikuwa anampa kauli zinazomwongoza kwenye kutekeleza majukumu yake.
Kwa mfano;
“Acha wasomaji wako wakuongoze nini cha kuandika.”
“Usijifanye una akili kushinda soko.”
“Kama hujui cha kufanya kwenye biashara, jiulize swali hili; nini kitakachoingiza fedha zaidi?”

Mmiliki huyo wa jarida alikuwa pia akiongozana na mhariri huyo kwenye mikutano mbalimbali aliyohudhuria na kumtaka abebe majarida ya kutosha.
Kwenye mkutano, mmiliki wa jarida alitumia kila fursa kusalimiana na watu wote mahimu, kwa kujitambulisha yeye mwenyewe na mhariri wake, kisha alimwambia mhariri ampe mtu huyo jarida. Baada ya kumpa jarida, mmiliki alimwambia mtu waliyesalimiana naye; “Ofisi yako inapaswa kujiandikisha kwenye jarida hili.”
Na aliendelea kusisitiza hivyo mpaka alipopata jibu alilotaka.
Alikuwa king’ang’anizi hasa na ndivyo alivyopata mafanikio aliyokuwa nayo.

Kuna kipindi mhariri huyo aliharibu injini ya gari kwa kuendesha bila oil, mmiliki alimtaka apigie wazalishaji wa gari hiyo wawape injini nyingine, japo hawakuwa na waranti.
Alipiga simu zaidi ya mara 500 na majibu yalikuwa ni hawawezi kupewa injini nyingine.
Lakini mmiliki alimtaka aendelee kupiga simu bila kuacha.
Alipigiwa simu mpaka na makamu wa raisi wa kampuni ya magari kuambiwa kwamba hawawezi kupewa injini nyingine bure.
Lakini mmiliki alimtaka aendelee kupiga simu bila kuchoka.
Na mwisho walipewa injini ya bure.

Mhariri alijifunza mengi kupitia mmiliki wa jarida na kugundua kwa nini alikuwa na mafanikio aliyokuwa nayo.
Na tangu hapo alianza kuangalia kila anachofanya kwa mtazamo wa mauzo.
Haikuchukua muda alibadili mwelekeo wa mauzo wa jarida na akaanza kulipwa vizuri.

Tukiwa hapo hapo kwenye kauli za kibabe kuhusu uandishi na mauzo, ipo habari ya Warren Buffett ambaye alinunua gazeti lililokuwa la miaka mingi.
Katika kuchukua hatua za kutaka gazeti hilo lifanye mauzo zaidi, alibadili mpango wa kulichapa gazeti na kuwa gazeti la kila siku ya wiki tofauti na awali.
Waandishi hawakufurahishwa na hilo, hivyo wakaakua kuanzisha mgomo kumshinikiza Warren kurudisha utararibu ambao walishauzoea.

Warren aliwapa siku saba za kurudi kazini na kama hawatafanya hivyo basi atawafukuza wote. Alimalizia kwa msisitizo akisema; “Hakuna chochote kinachofanyika ndani ya chumba cha habari kinachoathiri mauzo ya gazeti hilo.”
Baada ya kuona msimamo wa Warren, waandishi hao waliacha mgomo wao na kurudi kazini.

Kwenye mifano tuliyojifunza hapa, tumeona jinsi ambavyo mauzo yametumika kama kigezo cha kufanya maanuzi yote muhimu kwenye biashara.
Hivyo ndivyo tunavyopaswa kwenda na maamuzi yote ya biashara zetu, tuangalie kile kinachoathiri mauzo kisha kufanya hicho.

Mauzo ndiyo kipaumbele cha kwanza kwenye biashara yoyote ile.
Tuhakikishe maamuzi yoyote tunayoyafanya yana mchango mkubwa kwenye mauzo.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe