3200; Kushindwa ni kuacha.

Rafiki yangu mpendwa,
Karibu kila mtu kwenye maisha anataka kupata mafanikio makubwa.
Lakini kwenye uhalisia ni wachache sana ambao wamefanikiwa.
Wengi sana wameshindwa.

Na unapoangalia kwa karibu wale walioshindwa,
Unagundua siyo kwa sababu ya kukosea au kukutana na ugumu.
Bali ni kwa sababu waliacha kufanya.

Iko hivi, wanaofanikiwa na wanaoshindwa wote huanza na malengo ya aina moja.
Na kuanza kuchukua hatua ili kufikia malengo hayo.
Halafu wanakutana na ugumu.
Hapo ndipo wanapoachana.
Wanaoshindwa huwa wanaacha kufanya pale wanapokutana na ugumu.
Wanaenda kwenye vitu vingine wanavyoona ni rahisi zaidi.
Lakini huko pia wanakutana na ugumu.
Na hilo ndiyo linapelekea wawe wanaanza mambo mengi na kuishia njiani.

Wanaofanikiwa wanaendelea kufanya licha ya kukutana na magumu.
Wanajua magumu yapo kila mahali na hivyo hawajaribu kuyakimbia.
Badala yake wanayakabili na kuyavuka.
Wakikosea wanarekebisha makosa yao na kuendelea.
Hakuna hata wakati mmoja wanakuwa na fikra za kuacha kufanya kile walichopanga kufanya.

Safari nzima ya mafanikio ni mwendelezo wa fursa na mrejesho.
Pale mtu anapopata matokeo aliyokuwa anayataka yanafungua fursa kwake kufanya kwa ukubwa zaidi.
Na pale mtu anapopata matokeo ya tofauti na aliyokuwa anayataka unakuwa ni mrejesho kwake kwamba kuna kitu hafanyi kwa usahihi.
Hivyo anarudi kujitathmini kwenye kila anachofanya na kuona wapi anahitaji kufanya kwa ukubwa zaidi, ubora zaidi au hata kufanya kwa upya kabisa.

Wanaofanikiwa wanaujua vizuri mwendelezo huo wa fursa na mrejesho na wanaenda na kila wanachopata.
Wanajua chochote wanachopata siyo mwisho, bali ni sehemu ya safari.
Na hilo linawawezesha kupiga hatua kubwa zaidi.

Wanaoshindwa kila kitu kwao ni mwisho.
Wakipata wanachotaka wanajiona tayari wamemaliza.
Hawajisumbui tena kama awali na hilo huwa linapelekea wapate anguko hata baada ya kuwa wamepiga hatua fulani.
Na wakikosa wanachotaka wanajiona hawawezi kukipata kamwe, hivyo wanakata tamaa na kuacha.

Kama unataka kujihakikishia mafanikio kwenye jambo lolote lile, chagua kufanya kwa mwendelezo na msimamo bila kuacha.
Unachopaswa ni kupokea kila matokeo kama fursa na mrejesho.
Matokeo mazuri ni fursa ya kufanya kwa ukubwa zaidi
Na matokeo mabaya ni mrejesho wa wapi unahitaji kurekebisha kwenye ufanyaji wako.

Marekebisho huwa ni ya aina tatu.
Kwanza ni kufanya kwa wingi na ukubwa. Hapa unaongeza kiwango cha ufanyaji. Na hilo pekee linatatua mengi yanayokuwa yanamkwamisha mtu.
Mkwamo mkubwa ambao watu wanakutana nao ni kwa sababu wanafanya kwa kiwango kidogo kuliko inavyohitajika.

Baada ya kufanya kwa ukubwa wote unaowezekana na bado matokeo yasiwe mazuri, unaenda kwenye hatua ya pili ambayo ni ubora.
Hapa unaboresha zaidi kila unachofanya.
Unafanya kwa namna ambayo ni bora ukilinganisha na ulivyokuwa unafanya awali.
Hilo linakuwa na nguvu ya kuleta matokeo ya tofauti.

Na kama maboresho wamefanyika mpaka mwisho ila matokeo bado siyo mazuri, ndiyo hatua ya tatu inaweza kufanyiwa kazi.
Hatua hiyo ni kufanya kitu kipya.
Hapa unaanza kitu kingine kipya kwenye safari hiyo hiyo uliyochagua.

Kwa bahati mbaya sana, watu huwa wanakimbilia kufanya vitu vipya kabla hata hawajafanya kwa ukubwa na ubora.
Na hilo linawapelekea kuanza vitu vingi vipya lakini hawafiki navyo mbali.

Wewe umeshajifunza haya na hivyo unakuwa tofauti kabisa na walio wengi.
Hutashindwa kamwe kwa sababu hutaacha kufanya kwa namna yoyote ile.
Utatumia kila fursa na kila mrejesho kufanya kwa ukubwa, ubora na upya kwa maisha yako yote.
Hayo ndiyo maisha ya ushindi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe