3208; Unajua lakini hufanyi.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye ukurasa uliopita wa 3207 tumejifunza umuhimu wa kuchukua hatua ili kuzalisha matokeo tunayotaka badala ya kusubiri matokeo yajizalishe yenyewe.

Hilo ni jambo ambalo kila anayetaka mafanikio makubwa analijua, kwamba matokeo makubwa hayatokei tu, bali yanasababishwa.

Tukiendelea na mfano wa ukurasa huo, kwenye zoezi la upigaji simu, kila mtu anajua kwa kupiga simu unapata matokeo mazuri kuliko kusubiri watu wakupigie simu.

Lakini bado kujua hayo haisaidii, inapofika kwenye upigaji wa simu.
Kwani muda wa kupiga simu unapofika, kuna sababu nyingi ambazo zimekuwa zinazuia usifanye hilo.
Unajikuta umefanya mambo mengine ambayo hayana tija kabisa.

Kwenye jambo lolote unalofanya kwenye maisha yako, huwa linahusisha maeneo manne ambayo unayo.

Eneo la kwanza ni mwili.
Huo ndiyo unaochukua hatua iliyopangwa kuchukuliwa.
Kwenye zoezi la kupiga simu, mikono, masikio na mdomo vinahusika.
Hivyo tayari unavyo, hivyo mwili siyo kikwazo kwako.

Eneo la pili ni akili.
Hii ndiyo inafikiri na kufanya maamuzi kwenye yale unayopanga.
Kwenye zoezi la kupiga simu, tayari unajua umuhimu wa kupiga simu na ukipiga uongee nini.
Hivyo pia akili siyo kikwazo kwako.

Eneo la tatu ni hamasa.
Huu ni msukumo wa kuchukua hatua kwenye yale yaliyopangwa.
Msukumo unaweza kuwa wa ndani au wa nje, ila wa ndani ndiyo wenye nguvu na unaodumu zaidi.
Kwenye eneo la kupiga simu, tayari unayo hamasa ya kufanya hivyo, kwa sababu ya mahitaji mbalimbali uliyonayo.
Unajua kupitia kupiga simu, utapata unachotaka.
Hivyo hamasa pia siyo tatizo kwako, hasa kama unasoma hapa.

Eneo la nne ni hisia.
Hizi ndiyo zinaamua ufanye au usifanye kitu.
Hisia zinaweza kuwa chanya, kama furaha, matumaini, upendo na hizo zinaruhusu mtu kuchukua hatua.
Pia hisia zinaweza kuwa hasi, kama huzuni, hasira, wasiwasi, chuki na kukata tamaa, hizo zinazuia mtu kuchukua hatua.

Inapokuja kwenye zoezi la kupiga simu, kitakachoamua kama utafanya zoezi hilo au hutafanya ni hisia ambazo utakuwa umeambatanisha na zoezi hilo.
Kama umeambatanisha zoezi hilo na hisia chanya za upendo, furaha na matumaini, utakuwa tayari kulifanya.
Unapopenda na kufurahia kitu, utakifanya, hata kiwe kigumu kiasi gani.
Lakini kama umeambatanisha zoezi hilo na hisia hasi za hofu, wasiwasi, chuki na kukata tamaa, hutakuwa tayari kulifanya.
Unapokichukia kitu na kukikatia tamaa, hutakifanya, hata iweje.

Turudi kwenye mfano wetu wa simu tuone jinsi hilo linavyoweza kwenda.
Pata picha nimekupa orodha ya wateja 100, ambao ni kwa uhakika wote watanunua, wanachosubiri ni wewe tu uwapigie simu ili waweke oda. Na oda ambayo kila mmoja ataweka ni ya Tsh laki 1.
Swali ni je utapiga simu ngapi?
Jibu unalo, utapiga simu 100, utasimamisha mengine yote na kipaumbele cha kwanza itakuwa ni kukamilisha zoezi la kupiga simu.
Uhakika wa matokeo unakupa matumaini na kukufanya upende na kufurahia zoezi zima.

Upande wa pili wa mfano huo huo, nimekupa orodha yenye wateja 100, ambapo kuna 10 watakaonunua na kila atakayenunua ataweka oda ya Tsh milioni 1.
Swali ni je utapiga simu ngapi?
Hapa sasa ndiyo pazuri, mpango wako itakuwa ni kupiga simu 100.
Sasa twende na zoezi;
Simu ya kwanza haijapokelewa.
Simu ya pili imepokelewa, lakini akakata.
Simu ya tatu amekuambia mtafute wakati mwingine.
Simu ya nne anakuambia, nyie watu wa mauzo mbona mnasumbua sana?
Simu ya tano anakuambia kamwe usije ukampigia tena simu.

Enhe, niambie, zoezi la simu litaendaje?
Bado mpango wa kupiga simu kwa wateja wote 100 utakuwa nao.
Lakini kwa hayo matokeo ya awali, mambo yataanza kubadilika.
Utaanza kupatwa na hofu kabla ya kila simu unayopiga, hofu ya kwamba utakataliwa.
Utakuwa na wasiwasi na baadaye hasira juu ya matokeo unayopata.
Na mwisho kabisa, utalichukia zoezi zima, kutokana na hofu na hasira unazokuwa nazo.

Lakini hutajiambia yote hayo, maana hutataka kukubali kwamba unachukia zoezi la kupiga simu.
Badala yake vipaumbele vyako vitaanza kubadilika.
Utajiambia, wacha niwatumie ujumbe kwanza, halafu watakaojibu ndiyo nitawapigia simu.
Au utajiambia, wacha niposti, wale wanaotaka wataona tu.

Kubwa zaidi ni pale majukumu mengine madogo madogo unapoyapa umuhimu mkubwa kuliko zoezi hilo muhimu.
Mfano unajiambia wacha uorodheshe kwanzs hayo majina vizuri.
Au upangilie vizuri meza yako.
Au usome kwanza kitabu cha mauzo eneo la simu.
Yote hayo ni mazuri, lakini hayapaswi kuingilia zoezi la simu.

Ambacho unakuwa hujiambii ni kwamba unalikwepa zoezi ambalo ni muhimu kufanya, kwa sababu ya hisia hasi unazokuwa nazo juu ya zoezi hili.

Hatua ya kuchukua ili kubadili hisia hasi unazokuwa nazo kwenye jambo lolote ni kutengeneza taswira ya tofauti kwa matokeo yoyote unayoyapata.
Badala ya kutumia matokeo unayopata kujipa hisia hasi na kukata tamaa, unayatumia kujipa hisia chanya na kuwa na matumaini.

Kwenye mfano wa wateja 100 wa kupigia simu ambapo kuna 10 watakaonunua, kwa kila anayekataa kununua hukati tamaa kwamba zoezi haliwezekani, bali unafurahia kwamba umeshampunguza mwingine ambaye hahusiki.
Kila unapokutana na ambaye hanunui, unafurahia kwamba hatakuwepo tena kwenye orodha yako na kwamba unazidi kuwakaribia wale wenye uhakika wa kununua.
Pia kwa kila hatua unayochukua, jipe dakika chache za kutafakari unawezaje kuifanya kwa ubora zaidi.
Usijiambie ni kitu huwezi kufanya vizuri, bali angalia ni jinsi gani unaweza kuboresha.
Kama wateja wanakukatia simu kabla hata hamjafika mbali kwenye mazungumzo, unajiuliza uboreshe vipi mazungumzo ya awali ili wateja hao wawe na shauku ya kuendelea kukusikiliza badala ya kukata simu.

Rafiki, naamini umeondoka na kitu kikubwa hapa.
Jenga hisia chanya kwenye kitu chochote unachopanga kufanya na utaweza kukifanya kama ulivyopanga.
Huo ndiyo wajibu wako mkubwa.
Ukiweza hilo, hakuna litakalokushinda.
Na hili ni kwenye maeneo yote ya maisha, siyo tu mauzo.
Si unamjua mtu ambaye anasema hana muda wa kusoma vitabu, lakini anaweza kutumia masaa kwenye mitandao ya kijamii au kuangalia tamthilia?
Huenda ni wewe pia.
Nachotaka ni uone tu kufanya au kutokufanya kitu kunaamuliwa na hisia unazokuwa nazo juu ya kitu hicho.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe