Siyo mara yako ya kwanza kusikia ukatili na umeshaona watu wengi sana wakifanyiwa ukatili.
Vitu vingi ambavyo unaona mtu anakufanyia kwenye maisha yako, jua anafanya hivyo kwa sababu na yeye alishawahi kufanyiwa hivyo. Anaona ni sehemu ya maisha yake kufanya hivyo. Kwa sababu tokea anakuwa anaona wengine wakifanyiwa ukatili na yeye kukufanyia wewe ni sehemu ya maisha yake.
Mwanafalsa Seneca aliwahi kunukuliwa akisema,
Ukatili wote huwa unatokana na udhaifu.
Nukuu; All cruelty springs from weakness
Hii ina maana gani? Hii ina maana kwamba ukatili unachangiwa na udhaifu wa mtu.
Mtu dhaifu anatumia ukatili wake kuficha udhaifu wake aliokuwa nao.
Watu dhaifu ni wale ambao hawataki kusamehe, hawataki kuelewa, hawataki kupongeza nk. Watu dhaifu wanataka kuthibitisha kwamba wana nguvu ya kuwafanyia wengine ukatili.
Mtu imara hana haja ya kuwa katili. Na udhaifu wa watu hauko kwenye mwili bali udhaifu wa mtu uko kwenye akili. Kwa sababu mchezo mzima unaanzia kwenye akili.
Kwa kuwa wanaudhaifu wa akili, wanatumia udhaifu wao kuwaumiza wengine kwa kuwafanyia ukatili.
Na sababu kubwa ya watu kufanya ukatili ni hasira. Mtu akishindwa kutawala hisia zake ni rahisi kufanya ukatili kwa watu wengine.
Kwa mfano, mzazi kumpiga kibao mtoto wake kwa kosa fulani akiwa na hasira. Wazazi wengine wanawafanyia ukatili watoto wao kwa sababu ya kuiba mboga, fedha , sukari, nk.
Kwa mfano, kitendo cha kuua wanyama bila sababu ya msingi. Udhaifu alikuwa nao mtu anautumia kuwafanyia ukatili wengine.
Sina uhakika kama itakufaa lakini hata maeneo ya kazi. Bosi akiwa ana udhaifu baada ya kuona msaidizi wake ana kitu ambacho yeye hana anaanza kutumia nafasi yake kumfanyia ukatili msaidizi wake.
Ukatili ambao watu wengi wanafanyiwa chanzo chake ni udhaifu wa mtu.
Mtu ambaye ametulia kiakili na kujitambua hawezi kumfanyia ukatili mwenzake.
Na hata ukichunguza sana watu wengi ambao wanafanya ukatili kwa wengine ni kwa sababu na wao walishafanyiwa. Anafanya kama kulipa kisasi kwa wengine.
Watu wengi wana udhaifu wa akili na wanaficha udhaifu huo kwa kuwa na ukatili wa kuwaumiza wengine.
Kila mmoja wetu ana udhaifu wake. Na unachopaswa kufanya ni kujua udhaifu wake ili usiwafanyie ukatili wengine.
Dhibiti hasira ambazo zitakupelekea kufanya ukatili kwa sababu ya udhaifu unaokuwa nao kwenye akili.
Jiepushe na mazingira au vitu ambavyo vinawasha hasira yako. Jicheleweshe kuchukua hatua na kila wakati jiulize hiki ninachotaka kufanya je ni sahihi? Kama siyo sahihi usifanye.
Udhaifu wa akili ni mbaya, kwa mfano, unaweza kuona watu wa pembeni wanaongea na kucheka na wewe ukihisi ni wewe wanakusema hivyo unazalisha hasira ndani yako inayokwenda kufanya ukatili.
Kitu kimoja zaidi, udhaifu huu unakuwa unaanza kutengenezwa kwenye akili ya mtu kwa sababu ya hofu alikuwa nayo. Huyu amekuja juzi tu na anafanya kazi sana, asije akachukua nafasi yangu, hofu inazalishwa na matokeo ya hofu inatengeneza udhaifu wa akili na akili ikishakuwa dhaifu ndiyo ukatili hapo unazaliwa.
Ukatili unaofanywa na watu chanzo chake ni udhaifu wa akili tu. Tunatengeneza udhaifu wa akili kisha udhaifu wa akili unatutengeneza.
Unapaswa kujiamini, kujipenda na kuepuka kufanya mambo kwa hisia kwa sababu ukatili wote hutokana na udhaifu wa akili.
Ni ngumu kuzuia hasira lakini unaweza kuidhibiti usifanye ubaya. Mara zote kuwa mwema na tenda mema.
Unachopaswa kujua ni kitu gani ukifanya kinapelekea ukatili na kisha kuepuka kufanya kitu hicho.
Rafiki na mstoa mwenzako,
Mwl Deogratius Kessy
ASANTE sana
LikeLike
Karibu sana Frank Mapunda.
LikeLike