3221; Nani anamiliki nani?

Rafiki yangu mpendwa,
Huwa kuna utani kwenye mabenki kwamba mtu akiwa anadaiwa bilioni na benki, basi mtu huyo anakuwa anamilikiwa na benki.
Lakini mtu akiwa anadaiwa trilioni na benki, mtu huyo anakuwa anaimiliki benki.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwa wateja na biashara.
Pale mteja mmoja anapokuwa anachangia chini ya asilimia 10 ya mauzo yote ya biashara, mteja huyo anakuwa anamilikiwa na biashara.
Lakini kama mteja mmoja anachangia zaidi ya asilimia 10 ya mauzo ya biashara, mteja huyo anaimiliki biashara.

Hataonekana moja kwa moja kuwa na umiliki kwenye biashara, lakini kwa namna ambavyo biashara inakuwa inamtegemea, anakuwa na nguvu ya kuathiri mipango ya biashara.

Pamoja na wajibu mkubwa ulionao wa kutengeneza wateja wakubwa na wa uhakika kwenye biashara yako ili kukuza mauzo, unapaswa pia kuhakikisha huwi na utegemezi mkubwa kwenye wateja wachache.

Kama una wateja wachache ambao ndiyo wanachangia mauzo makubwa kwenye biashara yako, ongeza zaidi aina hiyo ya wateja.
Chukua idadi ya wateja wakubwa ulionao sasa kisha zidisha mara kumi.
Hilo ndiyo linapaswa kuwa lengo lako la wateja wazuri wa kuhakikisha unakuwa nao.
Unapokuwa na mara kumi ya idadi ya wateja wazuri ulionao, unabaki na nguvu kubwa kwenye biashara yako.
Hata pale biashara inapopoteza mteja mmoja au wachache kwa sababu zozote zile, haitetereki sana.

Kumbuka umechagua kuingia kwenye biashara ili uweze kufanya kile unachotaka kufanya, kwa namna unavyotaka kufanya, kwa wakati na mahali unakotaka kufanya.
Mwanzoni unaweza usiwe na uhuru kwenye maeneo yote hayo, lakini kadiri unavyokuza biashara yako kwa namna ambavyo haikutegemei, ndivyo unavyopaswa kuwa huru zaidi.

Huwezi kupata uhuru wa kibiashara unaoutaka kama bado utakuwa tegemezi kwa wateja wakubwa wachache.
Kwa wateja wowote wakubwa ulionao, weka juhudi kutengeneza wengi zaidi wa aina hiyo, kwa kurudia kwa wingi na ukubwa yale yaliyokuletea wateja hao.

Jenga biashara yako kwa usahihi ili pia uweze kuikuza kwa usahihi na kupata uhuru unaoutaka.
Hakikisha biashara ndiyo inawamiliki wateja kwa kutoa thamani kubwa sana ambayo wateja hawawezi kuipata mahali pengine huku ikiwa na wateja wengi wakubwa kiasi kwamba wachache wakiondoka biashara haitetereki.

Hili litahitaji kazi kubwa,
Litahitaji uwe tayari kupoteza baadhi ya wateja.
Litahitaji uwe tayari kuacha fedha ambazo ni rahisi kupata.
Lakini litajenga msingi imara sana wa mafanikio makubwa ya kibiashara.
Lipambanie kwa uhakika.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe