3223; Jipe dakika tano.

Rafiki yangu mpendwa,
Huwa ni kawaida kwetu binadamu tunaposikia kitu kipya kwa mara ya kwanza kukikataa na kukipinga kwamba hakifai au hakiwezekani.
Lakini mara nyingi hayo huwa ni maamuzi ya haraka ambayo pia siyo sahihi.
Unakuwa umefikia hitimisho la haraka kabla hata ya kutafakari kwa kina.

Kuepuka hali hiyo ya kufikia maamuzi ya haraka na ambayo siyo sahihi, jijengee utaratibu wa kujipa muda wa kutafakari kila jambo jipya kabla ya kufikia hitimisho.
Jipe angalau dakika za kukitafakari kitu kabla ya kufanya maamuzi juu ya kitu hicho.

Unafanya hivyo pia kabla hujakubaliana na kitu fulani unachoombwa.
Kwa sababu maamuzi yoyote ya haraka hayajawahi kuwa sahihi.
Kuna namna baadaye utakuja kujutia kwamba uliyaharakisha maamuzi hayo.

Ni sawa kukubali au kukataa kitu,
Kuona kinafaa au hakifai,
Kuchukulia ni rahisi au ngumu.
Lakini kwanza jipe muda wa kutafakari kitu kabla ya kufikia maamuzi hayo.
Dakika tano ni kiwango cha chini unachopaswa kujipa kutafakari jambo kwa kina kabla hujafanya maamuzi.
Na hapo ni kama maamuzi yanapaswa kuwa ya haraka.

Kama maamuzi hayana uharaka, jipe muda zaidi wa kutafakari jambo.
Tena hapa chukua zoezi la kuandika kabisa.
Andika pande mbili za jambo husika; upande wa kukubaliana na jambo husika na kuona manufaa yake na upande wa kukataa jambo hilo na kuona madhara yake.

Unapokaa chini na kuandika, unakuwa umeipa akili yako kazi ya kufikiri kwa kina juu ya kitu. Huwezi kuandika kama hujafikiri.
Na kwa kujipa wajibu wa kuandika kuhusu pande mbili za jambo, unakuwa umeliangalia kwa upana wake kabla ya kufikia maamuzi.

Kuna makosa mengi umeyafanya kwenye maisha yako kwa kukimbilia kufanya maamuzi juu ya jambo ulilosikia.
Kuna fursa nyingi umezikosa kwa kufanya maamuzi kabla hujatafakari kwa kina.
Usikubali kuendelea hivyo, bali jipe muda wa kutosha wa kutafakari kabla hujafikia maamuzi.

Na kama unalazimishwa ufanye maamuzi kwa haraka kabla ya kufikiri kwa kina shtuka, kuna kitu hakipo sawa.
Mara nyingi watu wanapokuwa wanataka kukuhadaa au kukutapeli huwa wanakushinikiza ufanya maamuzi ya haraka kabla hujafikiri sawasawa.

Jiwekee sera ya kufikiri kitu kwa angalau dakika 5 kabla ya kukifanyia maamuzi ya kudumu.
Na kama kitu hakiwezi kusubiri kwa dakika 5, siyo kitu sahihi kwako.

Na unapojipa dakika 5 za kufikiri kuhusu kitu, usikifikiri kwa mazoea ambayo tayari unayo. Badala yake jilazimishe kwenda nje ya mazoea hayo.
Ndiyo maana ni muhimu kuangalia pande mbili za jambo lolote kabla ya kulifanyia maamuzi.

Kufikiri kwa angalau dakika 5 kabla ya mufanya maamuzi kutakuepusha na makosa mengi ambayo umekuwa unayafanya kwa kukimbilia maamuzi ya haraka.
Kujifunza kufikiri haraka badala ya kujibu haraka ni hitaji muhimu kwa maisha ya mafanikio.

Hivyo basi rafiki yangu, wakati mwingine unaposikia kitu kwa mara ya kwanza, jipe dakika tano za kukifikiria kwa kina kabla ya kukifanyia maamuzi yoyote yale.
Kabla ya kukubali au kukataa kitu, hebu jipe muda wa kukitafakari kwa kina pande zake mbili.
Zoezi hili litakupa fursa ya kukielewa kitu kwa kina na kuona namna sahihi ya kwenda nacho.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe