3228; Waelewe watu.

Rafiki yangu mpendwa,
Tunaweza kusema kitu kimoja kwa uhakika kwamba biashara ni watu.
Kila kitu tunachofanya kwenye biashara kinahusisha watu.

Kila tunachofanya kwenye biashara, ni kupitia watu na kwa ajili ya watu.
Yaani tunawatumia watu kufanya vitu kwa ajili ya watu.

Hivyo basi, kama tunataka kupata mafanikio makubwa kwenye biashara, tunapaswa kuwaelewa watu.
Hiyo ni kwa sababu watu huwa wana changamoto zao mbalimbali.
Kama hutawaelewa watu, hujaelewa biashara.

Unaweza kuwa na ujuzi mkubwa wa kile kinachofanyika kwenye biashara.
Unaweza kuwa na miundombinu yote muhimu kwenye biashara yako.
Lakini kama huna mtandao sahihi wa watu wa kuutumia, vingine vyote vinakosa maana.
Ni sawa na kuwa na gari jipya na lenye nguvu kubwa, lakini linakosa mafuta, haliwezi kwenda popote.

Tunaposema biashara ni watu, ni kwa sababu;
Watu ndiyo wateja unaowalenga kwenye biashara.
Watu ndiyo wafanyakazi unaowahitaji kwenye biashara.
Watu ndiyo wabia wa kushirikiana nao kwenye biashara.

Hakuna namna unaweza kuwakwepa watu kwenye biashara.
Hivyo kuwaelewa watu ni jambo ambalo hakikwepeki kama unataka mafanikio kwenye biashara na maisha kwa ujumla.

Kitu kimoja tunachoweza kusema kwa uhakika ni kwamba ukiwaelewa watu, kamwe huwezi kulala njaa.
Kwa sababu chochote unachokitaka sasa, kipo kwa watu wengine.
Ni wewe kuweza kuwashawishi watu wengine wawe tayari kukupa vitu hivyo.

Katika vitu vingi unavyotakiwa kuwaelewa watu, kikubwa kimoja ni kwamba watu ni wabinafsi.
Watu huwa wanachukua hatua pale panapokuwa na maslahi binafsi kwao.
Hivyo pale unapoweka mbele maslahi ya wengine, inakuwa rahisi kutimiza maslahi yako pia.

Hii ni kanuni ya msingi kabisa ambayo unapaswa kuielewa na kuifanyia kazi mara zote ili uweze kupata kile unachotaka.

Waelewe watu, hicho ndiyo kilainishi chako kwenye hivi vyuma vya maisha.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe