3232; Umepanga kulipaje?

Rafiki yangu mpendwa,
Tunajua kwamba hakuna kitu cha bure.
Kwa chochote kile tunachotaka kwenye maisha, huwa kuna gharama ambayo lazima tuilipe.

Zipo njia mbili za kulipa gharama ya kupata kile tunachotaka.

Njia ya kwanza ni kulipa kwa fedha.
Hapa unatoa fedha na kuwalipa wale ambao wanakusaidia kupata kile unachotaka.
Njia hii japo inaweza kuonekana ya gharama kubwa, ndiyo njia bora ya kulipia mambo mengi kwenye maisha.
Kwani ni njia inayokuacha na muda wa kuweza kufanya yale unayoyafanya vizuri zaidi.

Njia ya pili ni kulipa kwa muda, machozi, jasho na damu.
Hii ni njia ambayo wewe mwenyewe unaingia kwenye kufanyia kazi kile unachokitaka.
Njia hii inaweza kuonekana ni ya gharama nafuu, lakini siyo iliyo bora. Kwa sababu mambo mengi unayohangaika nayo huna ubobezi wa kuweza kuleta matokeo mazuri unayoyataka.
Utaweka juhudi kubwa na kwa mateso, lakini utaishia kupata matokeo madogo na ya kawaida, ambayo hayakufikishi kule ulikotaka kufika.

Kama unataka kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako, tumia njia ya kwanza kwenye mambo yote ambayo hayahusiani moja kwa moja na shughuli zako kuu.
Yaani pale unapokuwa na kitu unachopaswa kufanya, kama siyo kile ulichobobea, basi walipe wengine wafanye.
Hilo litakuacha wewe ukiwa na muda, nguvu na umakini unaoweza kuutumia kwenye eneo ulilobobea na kuzalisha matokeo bora kabisa.

Lakini pia njia ya kwanza ndiyo unayoweza kuitumia kupata mafanikio unayoyataka.
Unachofanya ni kutatua tatizo kubwa ambalo linawakabili watu wengi, kisha kuwatoza watu fedha ili uweze kuwatatulia.

Kama unaanzia chini ambapo huwezi kumudu kulipa kwa fedha, lipa kwa muda, machozi, jasho na damu huku ukijijengea nguvu ya kuweza kulipa kwa fedha.

Kwenye maisha, unaweza kutumia muda ili kuokoa fedha au kutumia fedha ili kuokoa muda.
Kipi kipaumbele kwako inategemea ngazi yako ya mafanikio.
Unapokuwa unaanzia chini, unakuwa na muda mwingi na fedha kidogo, hivyo utatumia muda kuokoa fedha.
Unapokuwa umepiga hatua za mafanikio, unakuwa na fedha nyingi na muda kidogo, hivyo utatumia fedha kuokoa muda.

Mara zote hatua nzuri ni kutumia fedha kuokoa muda, kwa sababu muda una ukomo, lakini fedha hazina ukomo kabisa.
Pambana sana kufika hatua ambayo mambo mengi unayatatua kwa fedha ili ubaki na muda wa kutosha kuweka kwenye yale muhimu zaidi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe