3236; Dawa ya uraibu na usumbufu.
Rafiki yangu mpendwa,
Ni mwanafalsafa Seneca ambaye aliwahi kusema tatizo la muda siyo kwamba ni mchache, bali ni mwingi sana mpaka watu wanaamua kuupoteza.
Alichomaanisha Seneca ni kwamba tatizo la ufupi wa muda ambalo kila mtu analilalamikia, chanzo chake kikubwa siyo muda kutokutosha, bali matumizi mabaya ya muda.
Kuna vitu vingi ambavyo vimekuwa vinapoteza muda wa watu.
Lakini uraibu na usumbufu ndiyo vimekuwa vikubwa sana kwa zama hizi.
Uraibu ni pale mtu anapokuwa na uteja wa kufanya kitu fulani, yaani anashindwa kujizuia kufanya.
Na usumbufu ni pale mtu anapohangaika na vitu ambavyo havina manufaa yoyote kwake.
Kwa zama tulizopo sasa, kumekuwa na vitu vingi vinavyowapa watu uraibu, kuanzia matumizi ya vilevi mbalimbali mpaka mitandao ya kijamii.
Watu wamekuwa wanatumia muda wao mwingi kwenye uraibu kiasi cha kushindwa kufanya mengine makubwa.
Usumbufu pia umekuwa ni mkubwa sana kwa watu.
Watu na vitu vingi vinawinda umakini wa watu na kuwashawishi wahangaike na vitu ambavyo havina tija kwao.
Itaonekana kama ni vitu muhimu na vya haraka, lakini huwa havina mchango wowote kwenye kumfikisha mtu kule anakotaka kufika.
Uraibu na usumbufu ni vikwazo vikubwa, ambavyo vinaonekana ni vigumu kuvivuka na kupeleka muda na umakini zaidi kwenye mambo yanayokujengea mafanikio.
Ukweli ni kwamba, kitu chochote ambacho kinaonekana kuwa tatizo kwa mtu, tatizo hasa huwa siyo kitu hicho, bali mtu mwenyewe.
Hii inamaana kwamba pale mtu anapokuwa amekwama, hakwamishwi na kitu chochote cha nje, bali vile vilivyo ndani yake.
Na inapokuja kwenye uraibu na usumbufu, vinakuwa ni kikwazo kwa mtu pale ambapo anakosa kusudi kubwa linalomsukuma kufanikiwa.
Mtu anapokuwa anakwamishwa na uraibu na usumbufu ni kwa sababu anakuwa hajawa na KWA NINI kubwa inayomsukuma kwenye maisha.
Hivyo basi, dawa ya uraibu na usumbufu ni kuwa na kusudi kubwa kwenye maisha, ambalo linakusukuma kufanya makubwa zaidi.
Pale unapokuwa unakitaka kitu hasa, ambacho ni kikubwa na kinahitaji umakini wako mkubwa, utaachana na mengine yote ambayo hayahusiani na kitu hicho.
Chochote ambacho kunakuwa hakina mchango kwenye kile hasa unachotaka, hakipati nafasi yoyote kwako.
Kama bado unajiona unapoteza muda kwenye mambo yasiyokuwa na tija, jua tatizo siyo hayo mambo, bali tatizo ni unakosa kusudi kubwa kwenye maisha yako.
Anza kwa kutatua upande huo wa kusudi.
Jua kusudi lako kubwa, linalotoka ndani yako hasa kisha litumie kuondokana na yote yasiyokuwa na tija.
Kusudi sahihi na linalokusukuma kufanya makubwa huwa linaanzia ndani ya mtu na siyo nje.
Ni matokeo ya kutafakari kwa kina na kujisikiliza ni nini hasa unachotaka na unachoweza kufanya tofauti na wanavyofanya wengine.
Kisha unaamua kukifanya kwa namna ambavyo haijawahi kufanyika na kujitoa kweli kweli kwenye kukifanya.
Pale unapozama kwenye kulipambania kusudi kubwa la maisha yako, mengine nje ya kusudi hilo hayapati nafasi.
Huhitaji kusubiri mtu akuambie uache kupoteza muda, bali kusudi lenyewe linakuwa linataka muda wako mwingi kiasi cha kutokupata muda kwa mengine yasiyo na tija.
Kama bado hujalijua kusudi lako kubwa kwenye maisha, ni wakati sasa wa kujisikiliza na kulijua kusudi hilo.
Na kama umeshalijua kusudi lako, ni wakati wa kuachilia breki ili uweze kuliishi kusudi lako kwa ukubwa zaidi bila ya kujizuia.
Kadiri unavyoweka juhudi zako zote kwenye kusudi kubwa la maisha yako, ndivyo unavyokosa muda wa kupoteza kwenye mambo yasiyo na tija.
Kila unapojikuta unajilalamikia kwenye upotevu wa muda, rudi kwenye kusudi lako kuu na hakikisha hilo ndiyo kipaumbele pekee kwenye maisha yako.
Utapoteza muda kama unao mwingi na usiokuwa na matumizi.
Unapotumia muda wako wote kwenye kusudi lako kubwa, unakosa muda wa kupoteza.
Unalazimika kuwa na ufanisi ili kuweza kupata matokeo unayoyataka.
Jua na ishi kusudi lako, utatatua mengi yanayokuwa yanakukwamisha kwenye maisha yako.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe
Asante Kocha,
Nimeijifunza kuwa na kusudi kubwa na sahihi na kuliishi kunakujengea umakini na hivyo kudhibiti uraibu na usumbufu.
LikeLike
Vizuri sana.
LikeLike
Huhitaji kusubiri mtu akuambie uache kupoteza muda, bali kusudi lenyewe linakuwa linataka muda wako mwingi kiasi cha kutokupata muda kwa mengine yasiyo na tija.
Asante sana
LikeLike
Ndiyo
LikeLike
Jua na ishi kusudi lako, nitaendelea kutembelea humo humo, pamoja na changamoto zote ni kupambana na kuishi ndoto zangu mengine yote ni kuweka pembeni kabisa,najua siyo safari rahisi lakini ni kupambana.
LikeLike
Mapambano ndiyo njia pekee ya kufika tunakotaka.
LikeLike
Kusudi kubwa linapelekea mtu kuweka muda wote kwenye kusudi.
LikeLike
Ndiyo
LikeLike
Kadiri unavyoweka juhudi zako zote kwenye kusudi kubwa la maisha yako, ndivyo unavyokosa muda wa kupoteza kwenye mambo yasiyo na tija.
LikeLike
Hakika
LikeLike
Jua kusudi la Maisha yako , na litekeleze ipaswavyo
Kamwe hutopata muda wa kuchezea
Asante Sana kocha kwa makala Bora kabisa.
LikeLike
Kweli
LikeLike
Ukijua kusudi lako na kutekeleza kwa uhakika na kamwe huwezi kuhangaika na mambo mengine. Asante sana kwa ujumbe mzuri..
LikeLike
Karibu sana.
LikeLike