3241; Kufanya na kupiga hatua.

Rafiki yangu mpendwa,
Ni wengi wanaokuwa na mipango mikubwa kwenye maisha yao.
Lakini wanaochukua hatua ya kufanya kwenye mipango waliyonayo ni wachache sana.

Watu wanaopanga lakini hawafanyi, siyo kwa sababu hawawezi kufanya, bali ni kwa sababu wanakosa mwongozo sahihi wa kufanya.

Ili wewe uweze kufanya na kupiga hatua kwenye maisha yako, unapaswa kuzingatia yafuatayo.

Fanya kila siku.
Ni rahisi kuendelea kufanya kuliko kuanza upya baada ya kuwa umeacha.
Hivyo kama unataka kufanya na kupiga hatua, fanya kila siku bila kuacha.
Usiruhusu sababu yoyote ikukwamishe kufanya.

Fanya hadharani.
Fanya kwa kuonekana na wengine kwamba unafanya.
Waambie wengine kile unachotaka kufanya na jinsi ulivyojitoa ili kukipata.
Kadiri wengi wanavyojua mipango yako, ndivyo wanavyokukumbusha pale unapoacha kufanya au unapofanya yasiyokuwa sahihi.

Fanya kwa kushirikiana na wengine.
Ukiwa unafanya mwenyewe ni rahisi kukubali sababu na kuacha kufanya.
Lakini unapokuwa unafanya kwa kushirikiana na wengine, unalazimika kufanya hata kama huna kwa sababu hutaki kuwaangusha wengine.

Fanya kwa lazima.
Kuwa na kitu kinachokulazimisha ufanye la sivyo unapata madhara au kuingia gharama kubwa.
Hii inaweza kuwa ahadi umetoa kwa wengine kama utaacha kufanya au kuyumba.
Hapa pia ndipo mtu wa kukusimamia ufanye anapoingia, ambaye anahakikisha unafanya hasa na hakubaliani na sababu zako kirahisi.

Fanya zaidi ya unavyofikiria.
Wakati unapanga kufanya, kuna picha fulani ulikuwa nayo.
Wakati unaingia kufanya, mambo yanakuwa tofauti na ulivyokuwa unafikiria.
Hapo ndipo wengi hukata tamaa na kuacha.
Lakini wewe unapaswa kuendelea kufanya hata kama mambo hayajaenda kama ulivyotarajia.

Anayefanya mara zote huwa anazalisha matokeo tofauti ukilinganisha na wasiofanya.
Wewe weka kipaumbele kwenye ufanyaji kwa kuzingatia hatua ulizojifunza hapa.

Ukawe na ufanyaji bora, unaokupa matokeo makubwa unayoyataka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe