3253; Magumu na ya msingi.

Rafiki yangu mpendwa,
Biashara nyingi zimekuwa zinashindwa kwa sababu waendeshaji wa biashara hizo wamekuwa wanahangaika na mambo magumu kabla hawajabobea kwenye yale ya msingi.

Ni vizuri sana kuanza biashara ukiwa na maono makubwa.
Lakini kwenye kutekeleza maono hayo makubwa, haimaanishi kuhangaika na mambo magumu mwanzoni.
Kinachotakiwa ni kufanya yale ya msingi kwa ukubwa na kuweza kupata matokeo mazuri na makubwa kabla ya kwenda kwenye mambo magumu.

Biashara yoyote ile inatakiwa kuanza na tatizo ambalo tayari watu wanalo na wanataka kulitatua.
Suluhisho ambalo biashara hiyo inatoa linapaswa kuwa ni ambalo wateja walengwa wanalitaka na wanalimudu pia.

Baada ya uhitaji kuwepo, hatua inayofuata ni biashara kuweza kutengeneza wateja wa uhakika ambao wananunua kwa msimamo.
Hawa hawahitaji kuwa wengi sana ndiyo biashara iweze kuwa imara, bali ni kuanzia 100 mpaka 1000 kulingana na aina ya wateja wanaolengwa na kile kinachouzwa.
Kama ni bidhaa za bei ya chini basi wanapaswa kuwa 1000.
Na kwa bidhaa za bei ya juu wanapaswa kuwa 100.

Tumeona hapo ya msingi kabisa, kuanza na uhitaji na kufikia mauzo ya uhakika ili biashara iweze kwenda.
Hatua inayofuata baada ya hapo ni kufanya kwa ukubwa zaidi.
Kuendelea kutatua tatizo kwa ukubwa na kuwafikia wateja wengi zaidi.
Biashara nyingi zimekuwa zinakwama kwa sababu mambo mengi hayafanyiki kwa ukubwa.
Hivyo zinaposhindwa, watu wanadhani hazikuwezekana, kumbe ni kiwango cha ufanyaji.

Mengine yote yatakayofuata kwenye biashara, yanapaswa kuongozwa na ukuaji unaotokana na kufanya hayo ya msingi kwa ukubwa.
Usikazane kufanya mambo mengi na magumu kwenye biashara.
Badala yake fanya hayo ya msingi kwa ukubwa, kisha ukubwa huo utaleta mahitaji mapya ambayo biashara itapaswa kuyatatua.

Hiyo ni kuanzia kwenye kuajiri na mifumo mingine muhimu kwenye biashara.
Ukianza kuhangaika na hayo kabla hujaweza kutatua tatizo la wateja na kuuza kwa uhakika, yatakukwamisha kwa ugumu wake.
Badala yake anza na ya msingi, yafanye kwa ukubwa. Hayo ndiyo yatazalisha matatizo mengine ambayo utalazimika kuyatatua na kukuza zaidi biashara.

Biashara inayokua kuelekea kwenye magumu kwa kuanza na ya msingi ndiyo inayokuwa imara na kuweza kuhimili kila aina ya mikiki mikiki.
Hiyo ni kwa sababu yale ya msingi yanakuwa yameiimarisha sana biashara kiasi cha kuweza kukabiliana na chochote.

Lakini biashara inapolazimishwa kukua kwa kuhangaika na magumu kabla yale ya msingi hayajaimarishwa, inakuwa rahisi kuanguka pale inapokutana na magumu au changamoto. Hiyo ni kwa sababu yale ya msingi yanakuwa hayajaleta uimara kwenye biashara hiyo.

Ukuaji wowote wa biashara unapaswa kuanzia kwenye yale ya msingi ili uweze kuwa na tija kwenye biashara hiyo.
Nje ya hapo ukuaji utaleta matatizo ambayo hayataiacha biashara salama.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe